32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

NDUGULILE: WATAFITI TOENI SABABU WANAUME KUKWEPA KUPIMA VVU

Na MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM


 

 

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amewataka watafiti wa afya nchini kufanya utafiti, ili kubaini sababu na suluhisho kuhusu uwepo wa idadi ndogo ya wanaume wanaojitokeza kupima virusi vya Ukimwi (HIV).

Dk. Ndugulile alitoa wito huo Dar es Salaam jana wakati akifunga mkutano wa sita wa kisayansi, ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS).

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2016/17, ulioangalia maambukizi mapya na kiwango cha kufubaza VVU, wanawake wanaongoza katika maambukizi mapya, lakini ni wepesi kupima na kutumia dawa kikamilifu ikilinganishwa na wanaume.

“Lengo hasa tunahitaji kuona idadi kubwa ya wanaume ikijitokeza kupima VVU ili tuweze kupunguza kasi ya maambukizi mapya ifikapo 2030. Ili tuweze kufanikisha hili, ni lazima tuwe na majibu ya kitafiti yatakayotupa mwongozo kuhusu sababu za wanaume kukwepa kupima VVU na nini hasa kifanyike kuondoa changamoto hizo,’’ alisema.

Alisema kwa sasa Serikali ipo kwenye mchakato wa kuandaa sera ya afya, hivyo tafiti mbalimbali kuhusu masuala ya afya ni muhimu ili kuiwezesha sera hiyo kuakisi uhalisia wa masuala muhimu katika sekta hiyo.

Aliongeza kuwa kwa sasa taifa linakabiliwa zaidi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwamo kisukari, shinikizo la damu, kiarusi na figo, huku akitaja sababu kuwa ni pamoja na mfumo wa maisha usiozingatia miongozo ya lishe, matumizi ya pombe kupitiliza na uhaba wa mazoezi miongoni mwa wanajamiii.

“Upande wetu Serikali, tunaendelea kuboresha huduma za kibingwa kuhakikisha magonjwa kama figo na mengine ambayo tulikuwa tunatumia fedha nyingi kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, sasa yanatibiwa hapa nchini,’’ alisema.

Alitolea mfano matibabu ya figo ambayo kwa sasa yanafanyika ndani ya nchi kwa Sh milioni  21 badala ya milioni 100 zilizokuwa zikitumika nje ya nchi kwa kila mgonjwa.

Kuhusu suala la upatikanaji wa dawa hapa nchini, Dk. Ndugulile alisema; “Kwa sasa Serikali imetoa mwongozo wa utoaji wa dawa ambapo badala ya kuruhusu soko liamue dawa gani zitumike, kwa sasa Serikali ndiyo inaamua dawa ipi itumike kutibu ugonjwa upi, sehemu gani na kwa utaalamu gani.’’

Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Andrew Pembe, alisema nyingi kati ya tafiti zilizowasilishwa kwenye mkutano huo wa siku mbili, zilijikita katika vipaumbele vya taifa, yakiwamo masuala ya HIV/AIDS, kifua kikuu, afya ya uzazi na mtoto, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ajali na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika.

Aliishukuru Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Sida ambao kwa kushirikiana na wadau wengine wamewezesha mkutano huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles