33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MWANZO MWISHO SUGU ALIVYOTINGA BUNGENI NA BEJI YA MFUNGWA

Ramadhan Hassan, Dodoma

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Chadema), ametinga bungeni kwa mara ya kwanza tangu atoke jela kwa msamaha wa Rais John Magufuli huku akisimamisha shughuli za Bunge kwa saa kadhaa kutokana na wabunge kumshangilia.

Mbunge huyo ambaye alivalia suti ya rangi ya buluu illiyokooza na kubandika beji ya nambari ya mfungwa katika kola ya koti, lakini pia aliuliza swali la nyongeza ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka viongozi kuutumia mwezi Mtukufu wa Ramadhan kujitafakari bila ya kufafanua kujitafakari katika nini.

Mbunge huyo alitinga leo bungeni saa 3:20 asubuhi na kuibua shangwe, vifijo, makofi  kutoka kwa wabunge hususani wa upinzani walioshangilia kwa nguvu.

Mara baada ya kuingia Sugu alimpa mkono Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) na kwenda upande wa pili kwa Mnadhimu wa Serikali ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Ajira, Sera, Vijana, Walemavu, Jenista Mhagama.

Sugu akisalimiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adeldarus Kilangi.

Sugu pia alimpa mkono Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adeldarus Kilangi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika.

Sugu alirudi tena kwa Selasini na kisha kumkumbatia hali ambayo ilizidisha makofi na kushangilia ambapo Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ambaye alikuwa akiongoza kipindi cha maswali na majibu na kuwataka wabunge wawe na utulivu.

Sugu akikumbatiana na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini.

“Waheshimiwa wabunge naomba utulivu, mnakula muda wangu, sitawapa muda wa kuuliza maswali,” amesema Chenge.

Baada ya kukumbatiana na baadhi ya wabunge wa upinzani, sugu alikwenda kuketi kwenye kiti chake.

Sugu akiteta jambo na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe.

AULIZA SWALI KWA MARA YA KWANZA

Mara baada ya Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa  kujibu swali la msingi la  Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea (Chadema) lililohusu sheria za makosa ya mtandao.

Mwenyekiti wa Bunge, Chenge alimruhusu Sugu aulize swali la nyongeza ambapo alisema: “Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatakie mfungo mwema ndugu zangu Waislamu, ndani ya bunge na nchi nzima kwa wale ambao ni viongozi wautumie mwezi huu kujitathmini.

Kutokana na maelezo hayo ya Sugu, Chenge alimkatisha Sugu na kumtaka kuuliza swali moja kwa moja.

Sugu aliendelea kwa kusema: “Sheria hii pamoja na sheria nyingine mbovu za habari si tu zinawabana wananchi kupata habari bali zinatumika pia kufunga watu jela hovyo kisiasa…

“Mfano mimi nilifungwa kwa kujadilina na wananchi wangu taarifa za watu kupigwa risasi, watu kutekwa, maiti kuokotwa kwenye viroba, watu kutokuwa na uhuru wa kuongea….

Chenge alimkatisha Sugu kwa mara ya pili akimtaka kuuliza swali: “Mheshimiwa uliza swali.”

Sugu aliendelea: “Kitu ambacho si mimi tu najadili kwani kilishajadiliwa  ndani ya Bunge hili na pia Maaskofu wa Katoliki…

Chenge aliingilia tena: “Uliza swali,Uliza swali Mheshimiwa, hapana, hapana sina muda, uliza swali.”

Sugu: “Ni lini sheria hizi zitafutwa ili kulinda Katiba ya hususani Ibara ya 18 mfano maslahi  mapana ya demokrasia  nchini,”.

Chenge alimkatisha kwa kumwambia; “umeeleweka Mheshimiwa…”

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na  Mawasiliano, Kwandikwa alitumia muda huo kumkaribisha Mbunge huyo bungeni kwa mara nyingine.

“Kwanza nimkaribishe Mheshimiwa Sugu ndani ya nyumba Mheshimiwa karibu sana, lakini napenda kumjibu kuwa sheria zote Serikali inazitazama, na kama kuna maeneo yanahitajika marekebisho hufanya hivyo mara moja kwa kutumia Bunge.

“Labda kama kuna eneo mahususi kwa sababu Mheshimiwa Sugu umekuja tuonane ili na mimi nipate kwa upana kile ambacho unakizungumza, halafu sisi baadaye kama Serikali tutaangalia kwa nia nzuri ili sheria bora zaidi,” amesema.

mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles