KAMPALA, Uganda
WIZARA ya Afya nchini Uganda, imesema kwamba mishahara ya wafanyakazi wote wa Sekta ya Afya iitapanda kuanzia mwaka wa fedha ujao.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi mjini hapa na Waziri wa Afya , Jane Ruth Aceng, wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa sekta hiyo kupitia Ilani ya Chama tawala Cha NRM kuanzia mwaka 2016-2021.
Kwa mujibu wa kiwango cha marekebisho ya mshahara, mshauri mwandamizi ambaye kwa sasa anapata Sh. 3,447,065 atapata sh 4,500,000, mshauri wa ngazi ya kati ambaye kwa sasa anapata sh3,059,079 atapata Sh 4,200,000 na muuguzi ambaye mshahara wake ni Sh.413,158 kuanzia mwaka huo wa fedha ujao atapata Sh.613,158
Mbali na nyongeza hiyo ya mishahara, kwa mujibu wa waziri huyo, pia wahudumu hao wa Sekta ya Afya watakuwa wakipewa udhamini kwenda kusoma ambao utakuwa ikigharamiwa na Benki ya Dunia.
“Serikali itakuwa ikitoa udhamini katika ngazi mbalimbali kuanzia shahada, stashahada hadi ngazi ya vyeti,”alisema Acen.
Alisema kuwa pia maofisa hao watanufaika kwa kupewa nyumba za bure, baada ya 68 zinazojengwa katika Mkoa wa Karamoja chini ya msaada wa Serikali ya Italia kukamilika Desemba mwaka huu.