Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amezindua matumizi ya gesi asilia majumbani na kwenye magari.
Mradi huo wa matumizi ya gesi uliogharimu Sh trilioni 1.2, ulizinduliwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuwasha mitambo yake katika kituo cha Ubungo, jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema gesi hiyo itauzwa kwa gharama nafuu tofauti na ile ya sasa iliyopo kwenye mitungi.
Alisema gharama za gesi hiyo tofauti yake ni asilimia 40 ukilinganisha na gharama ya mtungi wa gesi kutoja nje ambao ni kati ya Sh 50,000 na 60,000 kwa sasa.
Alisema zaidi ya wananchi 1,000 wa awali tayari wameanza kutumia gesi hiyo baada ya kuunganishiwa.
Alisema tayari wamefungulia gesi kutoka bomba kubwa linalotoka Madimba, mkoani Mtwara kuingia kwenye bomba dogo ambalo litasambaza gesi majumbani jijini Dar es Salaam.
“Maeneo ya awali ya mradi wa usambazaji wa gesi asilia majumbani, jijini Dar es Salaam, wanufaika wake ni wakazi wa Ubungo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Survey, Makongo juu, Samnujoma, Shekilango , Sinza , Mikocheni Cocacola na Mwenge,” alisema Dk. Kalemani.
Kalemani alisema hatua ya pili itahusisha Mwenge, Tegeta hadi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo usambazaji umeenda sambamba na usambazaji wa gesi hiyo majumbani katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambako wananchi 850 wameunganishiwa.
Alisema shughuli zote za usambazaji gesi asilia majumbani itafanywa na Kampuni ya Ges Co ambayo itakuwa na dhamana ya kusambaza gesi hiyo kama ilivyo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Majisafi na Majitaka(DAWASA) na mengineyo.
“ Tumejiwekea mkakati kuhakikisha miundombinu ya usambazaji gesi ya majumbani inawafikia watanzania wote na kwamba kasi ya usambazaji miundombinu hiyo ni kubwa,” alisema
Waziri huyo alisema gesi hiyo ya majumbani ina ujazo wa futi trilioni 57.4 ambapo serikali imeyagawa katika sehemu tatu ambazo ni uzalishaji, matumizi ya majumbani na viwandani.
“Katika uzalishaji umeme tuna mradi wa umeme wa Kinyerezi II ambao unagharimu sh. trioni 8.8, Kinyerezi III utazalisha Megawati 300 na Kinyerezi IV utazalisha Megawati 330,”alisema Kalemani.
Alisema kwa matumizi ya viwanda Petrol Chemicals serikali ilitenga Sh trilioni 4.6 ambapo viwanda 37 kati ya 41 vitanufaika.
“Kwa mradi huu wa usambazaji gesi asilia majumbani na katika magari zimetengwa sh.trilioni 1.2,”alisema Kalemani.
Kalemani alisema kuanza kutumika kwa gesi hiyo majumbani kutasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na matumizi ya mkaa ambapo asilimia 90 ya wananchi wa Mkoa wa Dares salaam wanatumia mkaa.
Awali akitoa taarifa kwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba , alisema wamejipanga kuweka bomba lingine la gesi ambalo litaanzia Mwenge mpaka Tegeta kwenda Bagamoyo ambayo thamani yake ni Sh bilioni nne.
Alisema bomba lingine litasambaza gesi asilia katika eneo la Keko Gerezani na Mbagala ili wakazi wa maeneo hayo waweze kufaidika na rasilimali yao.
Kimu Mkurugenzi huyo wa TPDC alisema bomba lingine litajengwa Kusini Magharibi ya Ubungo ambalo litasambaza gesi eneo la Tabata mpaka Kimara.
Alisema kuwashwa kwa mitambo hiyo ya gesi majumbani itaunganishwa pia na viwanda viwili vya Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Ubungo, Kisare Makori alipongeza hatua hiyo ya serikali kuanza usambazaji wa gesi hiyo majumbani na kusema itasaidia kuondoa changamoto ya upatikanaji wa nishati.
Hata hivyo wakati TPDC wakiwasha mitambo hiyo na kuanza matumizi, baadhi ya wananchi walijitokeza katika eneo hilo wakidai fidia ya mali zao pamoja na nyumba kwa madai hawajalipwa chochote.