Na JANETH MUSHI-ARUSHA |
HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Desderi Kamugisha, ametishia kufuta kesi  ya makosa ya usalama barabarani inayomkabili mmiliki wa Shule ya Msingi Lucky Vincent, Innocent Moshi.
Akizungumza mahakamani hapo jana, Hakimu Kamugisha alisema atalazimika kuchukua uamuzi huo iwapo upande wa Jamhuri utashindwa kufanya marekebisho kwenye hati ya mashtaka kwa wakati.
a Hakimu Kamugisha alitishia kufuta kesi hiyo baada ya Wakili wa Jamhuri, Alice Mtenga, kuiomba mahakama iahirishe kesi hiyo ili akafanye marekebisho kwenye hati ya mashtaka baada ya kugundua ina kasoro.
Mei 3, mwaka huu, alipokuwa akiahirisha shauri hilo, hakimu alisema kwa kuwa limekaa mahakamani muda mrefu, atalisikiliza kwa siku tatu mfululizo kuanzia Mei 7 hadi 9, mwaka huu kwa upande wa Jamhuri kutoa ushahidi.
“Kama nilivyowaambia, mara ya mwisho nilipanga  siku tatu mfululizo za kusikiliza kesi hii ili upande wa Jamhuri wawe wamemaliza wiki hii.
“Kwa hiyo, naahirisha leo na tutaendelea kesho na kama kutakuwa na cha kukwamisha tena, nitachukua hatua maana sikatazwi kuifuta kama upande wa mashtaka hautakuwa tayari,”alisema Hakimu Kamugisha.
Awali, Wakili Mtenga alidai upande wa Jamhuri ulikuwa na shahidi mmoja ambaye ni shahidi wa nne, Alen Mwanry ila kutokana na kasoro ziliopo kwenye hati ya mashtaka usingeweza kuendelea na kesi hiyo hadi yatakapofanyika marekebisho. Ombi hilo lilikubaliwa na Wakili wa Utetezi, Method Kimomogoro.
Katika kesi hiyo namba 78 ya mwaka jana, Moshi pamoja na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Longino Nkana, wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kusafirisha wanafunzi bila vibali maalum.