27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MWENDOKASI VURUGU TUPU DAR

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM


MABASI ya Mwendokasi vurugu tupu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya abiria wanaotumia usafiri huo  Dar es Salaam kutoka sehemu mbalimbali za jiji  kusafiri bure jana baada ya kukosekana mashine za  eletroniki za kutolea tiketi.

Hiyo ilitokana na  uongozi wa UDA-RT, katika hali ya kushangaza jana, kukatisha  tiketi za mabasi hayo kwa mikono kama ilivyo kwa usafiri wa daladala, huku walinzi na maofisa wanaokatisha tiketi hizo wakishindwa kuwazuia watu kupita hali iliyozua vurugu vituoni.

Vurugu hizo zilizuka katika vituo vya Kimara Mwisho, Kimara  Korogwe, Kivukoni, Morocco na Gerezani, jambo lililofanya walinzi washindwe kuwathibiti wananchi waotumia usafiri huo.

Katika vurugu hizo, abiria  wengi walipanda bure magari hayo bila kukata tiketi za mkono ambazo zilikuwa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Vurugu hizo pia zilisababisha magari hayo kujaa kupita kiasi ikizingatiwa kwenye  baadhi ya vituo abiria walikuwa wamesongamana kuliko ilivyo kawaida   kutokana na kukosekana  magari hayo.

Huduma ya mabadi hayo Dar es Salaam imekuwa ikitolewa  kwa miaka takriban  miwili sasa.

Wafanyakazi waliokuwa wakikatisha tiketi hizo kwa mikono, ambao ni wajiriwa wa   UDA-RT nao waliingia kwenye mgomo baridi jana asubuhi,   wengine wakiwa wamepiga kambi katika ofisi za kampuni hizo Jangwani.

Mmoja wa abiria wa usafiri huo aliyejitambulisha kwa jina la Thomasi Kilima, aliiambia MTANZANIA kuwa hali hiyo ilisababisha  shida na adha kubwa kwao.

Naye Ramadhan Issa, aliliambia MTANZANIA kuwa tiketi za UDA zilizoanza kutumika  jana zinajenga mazingira ya wizi kwa sababu  zinakuwa hazina udhibiti wa fedha unaotakiwa kama ilivyokuwa kwa tiketi za elektroniki.

“Hizi tiketi za UDA nilikuwa naziona usiku  unapokata, lakini jana naona ndiyo zimepamba moto.

“Hata wanaotukatia unaona kuna mazingira ya ujanja ikiwamo kukosema udhibiti wa fedha za Serikali.

“Hapa  ndipo kuna ulaji … ni vema Serikali iamke sasa na kuliangalia suala hili kwa jicho la tatu.

“Usafiri huu ni mzuri ila kilichokosekana ni udhibiti na si ajabu tukaja kusikia usafiri huu nao umekufa kama ilivyokuwa UDA ya zamani.

“Serikali amkeni tiketi hizi ni wizi mtupu,” alisema na kuonya.

Meneja Uhusiano wa UDART, Deus Bugaiywa alipotafutwa,  alisema wapo kwenye operesheni na  watakapomaliza angelitolea ufafanuzi suala hilo.

Hata hivyo Ilipofika saa 10 jioni na kupigiwa simu tena, simu yake iliita bila kupokewa.

MAXCOM  YARUKA

Wakati wakazi wa jiji hilo wakikumbwa na adha hiyo, Kampuni ya Maxcom Afrika (Maxmalipo),  imesema  haihusiki tena na utoaji wa huduma ya tiketi za  elektroniki kwenye mradi huo.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma,  Deogratius Lazari, ilieleza kuwa kampuni hiyo ilikuwa ni mmoja wa wabia walioshiriki kutoa huduma katika mradi huo kuanzia Mei 16, mwaka 2016 baada ya kuzinduliwa kwa kipindi cha mpito.

Alisema kuanzia Aprili 13, mwaka huu, imekuwapo hali ya sintofahamu katika vituo vya mabasi hayo, ikiwa ni pamoja na uuzwaji wa tiketi za karatasi (za vishina) ambazo hazipiti kwenye mfumo wa tiketi za  elektroniki ulioidhinishwa na wasimamizi wa mradi huo.

“Pia kumekuwapo na nyakati ambazo abiria wanasafirishwa bila kulipa nauli. Tunaomba ifahamike kwamba haya yanayoendelea yanaratibiwa na kampuni ya UDA-RT ambayo mbia wake mkubwa ni Simon Group ambao wanamiliki mabasi haya ya Mwendokasi.

“Maxcom Africa PLC waliingia mkataba kutoa huduma ya tiketi za elektroniki katika mradi huu wa Mwendokasi chini ya kampuni ya UDA-RT kutokana na maagizo yaliyotolewa na Serikali,” alisema Lazari.

Alisema katika mkataba wao Maxcom ilihusika kuweka mifumo, rasilimali watu, teknolojia na wasimamizi katika mradi huu.

“Februari  mwaka huu tuliamua kufungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania, kesi ambayo mpaka sasa inaendelea kusikilizwa.

“Kwa zaidi ya miaka miwili sasa, UDA-RT wamekua wakikwepa kulipa stahiki hizi za  wafanyakazi ingawa Maxcom iliendelea kutoa huduma ili kulinda heshima ya mradi na nchi yetu.

“Aprili 13 mwaka huu UDA-RT walitangaza kuiondoa Maxcom kwenye mradi na kuipa kazi kampuni ya TTCL Corporation bila kufuata taratibu zozote za  mkataba, bila kutoa notisi wala kurasimishana makabidhiano ya mradi,” alisema

Alisema hivi karibuni UDA-RT walitumia nguvu kuwatisha na kuwaondoa wafanyakazi waliokuwa wanatoa huduma ya tiketi za  elektroniki katika vituo vya Mwendokasi, bila kufuata taratibu zilizoainishwa kwenye mikataba ya ajira zao.

Lazari alisema yanayofanywa na UDA-RT hayana nia njema na mradi huo na  maendeleo ya taifa kwa ujumla.

“Ni dhahiri haya yanaweka doa katika mradi huu na yanaweza kuleta mazingira ya ufisadi na dhuluma hasa ikizingatiwa kesi ya madai ipo mahakamani.

“Tunawaomba Watanzania na umma kuelewe kwamba huduma inayotolewa katika vituo vya Mwendokasi isiyohusisha tiketi za elektroniki inatolewa na UDA-RT  na siyo Maxcom Africa PLC,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles