29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MKUU AWAJIBU KINA FATMA KARUME

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM


JAJI Mkuu Profesa Ibrahimu Juma, amesema Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kinafanya kazi za umma, hakipaswi kujiingiza katika siasa wala uanaharakati, kwani kwa kufanya hivyo kinaweza kukosa ushirikiano.

Kauli hiyo ya Jaji Mkuu, imekuja siku moja baada ya Rais wa TLS, Fatma Karume, kusema chombo chao si mali ya Serikali na hakuna mwenye uwezo wa kukiingilia kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Profesa Juma, alisema na kusisitiza kutokana na majukumu ya TLS, bado ni taasisi ya umma licha ya kuwa ni chama huru cha kitaaluma.

“TLS ukiangalia kazi zake huwezi kuona siasa wala uanaharakati, TLS wasikubali kuingia katika siasa wala uanaharakati, ukiingia huko wengine hawatatoa ushirikiano.

“Kama wanataka kushirikiana na mahakama, wabaki katika kazi zao, wakitaka kuwa huru wataachwa wawe huru, lakini hawatapata ushirikiano kutoka kwetu, sababu wengine haturuhusiwi kuingia katika siasa.

“Ada za wanachama wa taasisi hiyo zinabakia katika chama, kwa sheria ya fedha lazima kila mwaka zikaguliwe na mtu anayetambulika na Waziri wa Fedha… ingekuwa mtu binafsi asingekaguliwa,” alisema Profesa Juma.

Alisema TLS ni taasisi ya umma, inafanya kazi za umma na wanapaswa kumuheshimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) sababu hawawezi kumkwepa.

“Jaji Mkuu ana mamlaka ya kutunga sheria ndogo ndogo, lakini akitunga lazima ziende kwake apitie, chombo chochote kikitengeneza kanuni kikasema hawapitishi kwa AG, kinajidanganya, mtu huyu huwezi kumkwepa,” alisema.

Profesa Juma, alisema TLS ina majukumu ya kitaifa, inatakiwa kuisaidia Serikali, Bunge na Mahakama katika masuala ya sheria.

Alisema huwezi kuisaidia Serikali kwa kulumbana, TLS si binafsi, inatakiwa kurudi katika malengo ya kuanzishwa kwake.

Aliyataja baadhi ya majukumu ya TLS ni kuboresha taaluma ya sheria na hiyo si kazi binafsi ni kazi ya umma.

“Hatuwezi kukubali chama kikasema wao binafsi… Haiwezekani, jukumu lao jingine ni kuendeleza wanachama ili waendane na mabadiliko ya sheria… hii dhana ya ubinafsi haipo.

“Jukumu lao jingine ni kuisaidia Serikali na Mahakama kuhusu mambo ya kisheria na kazi za sheria… huo mtiririko wa umma si binafsi,” alisema.

Alisema wajumbe waliokaa miaka ya 1961 walifanya mabadiliko ya sheria, ada zikabakia kwenye chama na majibu yalikuwa chama hicho kinafanya kazi za umma.

Profesa Juma aliwaomba viongozi wa TLS washirikiane katika mistari ya kisheria, na kwamba malumbano yasiyo na tija katika magazeti hayasaidii.

Wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli, alimtaka Jaji Mkuu kuidhibiti TLS, kauli ambayo ilimwibua Rais wa chama hicho, Fatma Karume aliyesema hakuna wa kuwadhibiti.

Akizungumza na MTANZANIA juzi, Fatma, alisema TLS inajiendesha yenyewe na kwamba wanachama wake ambao ni wanasheria, wanalipa ada ya kila mwaka, fedha ambayo inawalipa mishahara wafanyakazi 40 bila msaada kutoka chombo chochote.

“TLS inaendeshwa na wanachama kwa fedha zao wenyewe, kila mwaka wanachama wanatoa ada na tunawalipa wafanyakazi 40 mishahara yao bila msaada kutoka kokote, tunawahudumia wananchi kwa fedha zetu wenyewe.

“Mahakama ni mhimili ambao uko huru na Serikali ni mhimili mwingine ambao nao uko huru. Kama wanasheria sisi tuko chini ya Mahakama.

“Hivyo hakuna mtu wa kuidhibiti TLS kwa sababu hakuna binadamu anayeweza kumdhibiti binadamu mwenzake, kwa mujibu wa katiba yetu kila binadamu ni huru, lakini unapovunja katiba na sheria za nchi hapo hauko huru,” alisema Fatma.

Mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles