Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Spika wa Bunge, Job Ndugai amerejea bungeni na kuongoza Kikao cha Tano cha Mkutano wa 11 wa Bunge Mjini Dodoma leo, ikiwa ni mara ya kwanza tangu arejee nchini kutoka nchini  India alikokuwa akitibiwa.
Spika Ndugai ameingia bungeni hapo saa tatu kamili asubuhi huku akishangiliwa na wabunge mbalimbali ambapo baada ya kuketi ameongoza kikao hicho kama kawaida bila kusema neno la ziada.
Hii ni mara ya kwanza kwa Spika Ndugai kuongoza Kikao cha Bunge kwa mwaka huu, baada ya kuwa nje ya nchi kwa matibabu huku vikao vilivyopita vya bunge la Januari mwaka huu vilikuwa vikiongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson na wenyeviti Andrew Chenge na Najma Murtaza.
Spika Ndugai amekuwa nchini India kwa miezi kadhaa na hivyo kukosa kikao hicho cha bunge la Januari ambapo amerejea bunge likiwa linaendelea kujadili Bajeti ya Mwaka ujao wa fedha (2018/19) katika Ofisi ya Waziri Mkuu, iliyowasilishwa wiki iliyopita.