33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

UKARABATI MIUNDOMBINU YA SHULE WARUDISHA WANAFUNZI WALIOKACHA MASOMO

Na ELIUD NGONDO-CHUNYA


SERA ya Elimu bure inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, imechangia ongezeko la wanafunzi wa awali hadi darasa la kwanza, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba miundombinu inayotumika haina ubora.

Miundombinu mingi ya shule za msingi na sekondari hapa nchini imechakaa kutokana na baadhi ya wananchi kushindwa kuikarabati  na hivyo kuiachia Serikali jukumu hilo.

Shule ya Sekondari ya Isenyela iliyopo Kata ya Mbugani, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, ni miongoni mwa shule zilizokuwa zikikabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu yake ambayo baadhi ya wadau wa elimu wamejitokeza kwa ajili ya kuikarabati.

Miongoni mwa wadau hao ni mchimbaji mdogo wa madini ya Dhahabu wilayani humo, Leonard Manyesha ambaye amejitolea kukarabati miundombinu ya shule hiyo ambayo kwa sasa inavutia kwa wanafunzi

kujifunza.

Manyesha amekarabati jengo la utawala ambalo awali lilitelekezwa na wananchi kutokana na ukata wa fedha kwa kuliwekea sakafu, kuchapia nje na ndani pamoja na kupaka rangi.

Aidha, ameshirikiana na wananchi kujenga chumba cha maabara ya shule hiyo, mradi ambao Serikali iliwataka wananchi kuanza kuutekeleza kisha kuiachia hatua za mwisho kwa ajili ya kumalizia.

Manyesha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wachimbaji wadogo na wa kati mkoani Mbeya, anasema aliamua kufanya ukarabati huo baada ya kuona vyumba vya madarasa na jengo la utawala vikiwa na hali mbaya ambayo kwa namna moja au nyingine ingeweza kuwakatisha tamaa wanafunzi.

Anasema ukarabati huo wa vyumba vinne pamoja na jengo la utawala, umegharimu Sh milioni saba na kwamba gharama hiyo inajumuisha pia michango mingine.

Anasema fedha hizo ni sehemu ya faida anayopata kutoka kwenye shughuli zake za uchimbaji wa madini ya Dhahabu ambazo aliamua kuwasaidia watoto wa eneo hilo.

Anasema hakuna Taifa lolote duniani ambalo linaweza kuendelea bila kuwekeza katika sekta ya elimu, hivyo yeye ameamua kuwekeza fadhila zake kwa kuboresha miundombinu ya shule hiyo ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.

“Napenda kuona watoto wanasoma katika mazingira mazuri ili watimize ndoto zao hatimaye baadae wawe viongozi wazuri wa Taifa hili, walimu wakikaa katika ofisi zilizo bora hata moyo wa kufundisha wanakuwa nao, ndio maana nimeona nishiriki kuboresha miundombinu hii,” anasema Manyesha.

Manyesha anasema baadhi ya wananchi wa vijiji vyenye madini wilayani humo hawajishughulishi na shughuli za uchimbaji hivyo wachimbaji wakiboresha miundombinu hiyo itakuwa ni fursa ya kuwasaidia kunufaika pia na rasilimali hiyo.

Manyesha anasema asilimia kubwa ya ardhi ya Wilaya ya Chunya ina madini lakini miundombinu ya huduma za jamii zikiwamo nyumba za walimu na vyoo vya wanafunzi haiendani na utajiri huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Isenyela, Bereth Gerald, anasema licha ya mchimbaji huyo kukarabati miundombinu hiyo, pia alitoa Sh milioni 1.6 kwa ajili ya kusuka umeme baada ya mbunge wa Jimbo la Lupa, Victor

Mwambalaswa kutoa fedha kwa ajili ya kusogeza huduma hiyo.

Gerald anasema pamoja na hilo, Manyesha alishiriki katika ujenzi wa vyumba vya maabara ambapo alitoa zaidi ya Sh milioni mbili ili kuhakikisha wanafunzi wanajifunza masomo ya sayansi kwa vitendo.

Changamoto nyingine ilikuwa ni uchakavu wa vyoo vya walimu na wanafunzi, ambapo anasema mchimbaji huyo amejitolea kuhakikisha zoezi

hilo la ukarabati linakamilika pamoja na jengo la utawala.

“Katika mahafali ya kidato cha nne mwaka 2016 aliahidi kuhakikisha anakamilisha ukarabati wa jengo la utawala ambalo lilikuwa ni

changamoto na alitoa kiasi cha Sh milioni 1.6 ili kusaidia nguvu ya halmashauri,” anasema Gerald.

“Hata mimi nilipohamishiwa katika shule hii nilishangaa kuona miundombinu si rafiki kwa watoto kutokana na kuchakaa, jengo la utawala nalo lilikuwa bado halijakamilika lakini Manyesha ametia nguvu hadi kukamilika kwake,” anesema Gerald.

Mwalimu huyo anaitaja changamoto nyingine kuwa ni uchache wa meza za walimu ambapo wanalazimika kutumia madawati ya wanafunzi kitu ambacho anadai ni kinyume na utaratibu.

Hata hivyo, anasema katika kuwatia moyo walimu wa shule hiyo, Manyesha ameahidi kuwalipa Sh 300,000 kwa mwalimu ambaye wanafunzi watafanya vizuri somo lake katika mtihani wa kidato cha nne

mwaka huu.

Baadhi ya wanafunzi wameeleza kuwa kuwapo kwa miundombinu mizuri kwa sasa katika shule hiyo imekuwa ni kivutio kikubwa cha wao kukaa darasani na kuhamasisha wengine kuacha tabia ya utoro waliyokuwa nayo awali.

Mwanafunzi Irene Mwakoma,kutoka Shule ya Sekondari Isenye, anasema awali miundombinu ilikuwa si rafiki, walikuwa wakikatishwa tamaa hata kuhudhuria vipindi darasani ilikuwa shida, lakini kwa sasa wanavutiwa na mazingira ya shule hivyo wanahudhuria masomo bila kushurtishwa.

“Ilikuwa ni aibu kwa wanafunzi kwenda haja kutokana na ubovu wa vyoo, yaani ukienda haja basi aliyeko nje ni lazima akuone.

“Kuna wenzetu ambao waliamua kuachana na shule kutokana na miundombinuilivyokuwa mibaya, wakaanza kufanya shughuli za uchimbaji wa madini ya Dhahabu lakini tangu ilivyokarabatiwa wanatamani

kuja kuendelea na masomo,” anasema mwanafunzi huyo.

Naye mwanafunzi Shalim Adam, anaeleza kuwa wachimbaji wengine wilayani humo wanatakiwa kujitolea katika kukarabati miundombinu ya shule mbalimbali zilizowazunguka ili kuzidi kuboresha elimu nchini.

“Wachimbaji wengine wilayani humo wanatakiwa waige mfano wa mchimbaji huyo kwa kujitoa kuendeleza shughuli za kijamii ili ziweze kuimarika katika maeneo yao na si kuacha jukumu hilo kwa Serikali pekee,” anasema Adam.

Anasema wachimbaji ambao wamekuwa wakifanya shughuli hiyo, wanatakiwa kuwekeza zaidi katika elimu ili kuwafanya watoto wanufaike na madini hayo kupitia elimu.

Kwa upande wa wananchi wa maeneo hayo, wanasema kuna baadhi ya wachimbaji walionufaika na madini hayo huenda sehemu nyingine kwa ajili ya kuendelea na shughuli zao kitu ambacho si haki.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wengine, Isaya Adam anasema wachimbaji wakiwa na umoja wa kuweza kujitoa katika kuchangia shughuli za kijamii, wilaya hiyo itabadilika na kuwa mji wa kitalii tofauti na sasa ambapo yamekuwa yakiachwa mashimo na dhahabu kuondolewa.y

Anasema katika kijiji hicho kumekuwapo na watu wengi ambao ni wachimbaji lakini suala la miundombinu ya shule imekuwa mibovu.

“Wanafunzi wanakaa kwenya vyumba vya madarasa vilivyo chakaa wakati

kuna wachimbaji wengi ambao wakichangishana na kujitoa kwa moyo wote wanaweza kujenga, kukarabati shule zote na wanafunzi wakaacha

kupata shida.

 

“Wachimbaji wanatakiwa kuwekeza kwenye elimu zaidi kwani hawa watoto ni taifa letu na wanahitaji kupata elimu ambayo itakuwa ni mkombozi

kwa vizazi vijavyo, pia inakuwa ni njia moja wapo ya kurudisha fadhila kwa wananchi,” anasema Adam.

 

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Chunya, Hebo Kibona anasema wilaya hiyo kwa sasa haina upungufu wa vyumba vya madarasa isipokuwa vilivyopo vinakabiliwa na uchakavu

mkubwa.

Anampongeza Manyesha kwa moyo wake wa kujitolea akidai kuwa ni watu wachache wenye fedha huwa wanajitolea kwenye shughuli za

kijamii.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles