23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

PANAMA WABUNI GEREZA LINALOTEMBEA BAHARINI

BINADAMU kila siku wanakuja na vitu ama ubunifu mpya kadiri wanavyojiwa na wazo.

Wakati mwingine ubunifu hutokea kufuatana na mazingira au tukio linalozaa wazo la kulifanyia kazi kisha kutengeneza kitu kinachofanana au kuakisi wazo hilo.

Ndiyo maana utakuta kuna ubunifu wa magari mfano wa viatu, mfano wa ndizi, mnyama na kadhalika.

Safari hii wabunifu nchini Panama wamekuja na wazo la kutengeneza meli kubwa itakayokuwa jela maalumu.

Ubunifu huo umetokana na mawazo mawili; Nyaraka za Panama na gereza linaloonekana katika filamu moja mashuhuri.

Wamelenga kukejeli wakwepa kodi, kwamba wale waliotajwa kukwepa kodi katika kile kinachojulikana kama Panama Papers (Nyaraka/karatasi za Panama) wafungwe ndani ya gereza hilo litembealo.

Mwaka juzi nyaraka za siri milioni 11 zinazohusu akaunti za fedha zilizoitwa Panama Papers zilivuja kutoka kampuni moja ya sheria.

Nyaraka hizo zilifichua maelfu ya watu mashuhuri duniani kuanzia wafanyabiashara, wafalme, viongozi na watoto wao hadi wale wa dini namna walivyoficha fedha ng’ambo.

Nyaraka hizo zilionesha rangi halisi ya baadhi ya matajiri duniani pamoja na watu wenye mamlaka wanavyozitendea nchi zao.

Fedha hizo haijalishi kuwa ni halali au haramu. Lakini lengo la kuficha fedha ng’ambo ni kukwepa kulipa kodi katika nchi zao au kuzificha kwa vile ni haramu au zimeibwa kutoka nchi zao.

Wabunifu wameichora meli hasa vyumba vya wafungwa vilivyo juu ya boti kwa kulitazama lile gereza alimofungwa mwigizaji mbilikimo Tyrion Lannister katika filamu ya Game of Thrones.

Gereza hilo litembealo baharini, linaloenda kwa jina la Jela ya Nyaraka za Panama, yaani Panama Papers Jail (PPJ) ina uwezo wa kuchukua hadi wafungwa 3,300 wanawake na wanaume.

Kila chumba cha mfungwa kina ukubwa wa mita za mraba tisa.

Wabunifu wamesema selo za gereza hilo zitatengenezwa kwa karatasi ambazo zitatumika kama tanga kuifanya meli hiyo kutembea.

Wabunifu Axel de Stampa, Sylvain Macaux na Guillaume Devaux kutoka Ecole d’Architecture de Paris-Belleville walisema: “Panama Papers’ Jail ni gereza lililotengenezwa kwa selo za karatasi.

Gereza linajengwa eneo la kuegeshea meli lililopo kwenye bahari ya kimataifa likiangalia Panama City. Litakuwa na pande mbili za selo; moja kwa wanaume na nyingine kwa wanawake.”

Meli hiyo itakuwa na ofisi za maofisa, kituo cha utawala na ukumbi wa chakula huku eneo la juu likiwa kwa ajili ya shughuli za kilimo, kadhalika ina maeneo ya mazoezi, karakana na uwanja wa michezo.

Meli hiyo imetengenezwa ikiwa ni sehemu ya mradi unaoitwa 1week1project, ambao ni tovuti inayotoa wazo la ubunifu kila wiki kuhusu maisha ya kila siku duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles