Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa tamko la kutaka kuwapo maridhiano ya taifa kuhusu mustakabali wa nchi.
Limetaka mazungumzo hayo yashirikishe makundi mbalimbali wakiwamo viongozi wastaafu, asasi za raia, vyama vya taaluma, makundi ya rika mbalimbali kuweza kufanya mjadala huo kama alivyofanya Rais Dk. John Magufuli, alipokutana na wafanyabishara Ikulu Dar es Salaam, hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema hivi sasa Taifa linashuhudia malalamiko mbalimbali kutoka kwa jamii jambo ambalo halileti afya kwa ustawi, umoja na mshikamano wa Watanzania.
Alisema tamko hilo ni maazimo ya wahariri wanachama wa TEF waliokutana juz.
Kwenye mkutano huo, pamoja na mambo mengine, walijadili na kutafakari kwa kina hali na mwelekeo wa nchi kwa sasa ambako malalamiko yamekuwa mengi kwa makundi ndani ya jamii.
Alisema malalamiko hayo ambayo baadhi yamekuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari yamekuwa yakigusa sehemu kuu tatu ambazo ni kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni hasa kupitia vyombo vya habari, kuzorota demokrasia nchini kwa ujumla wake na ukuaji wa uchumi ambao kwa sasa haulingani na hali ya maisha ya Watanzania.
Alisema kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni kimekuwa kikwazo kikubwa cha utendaji na ufanisi katika vyombo vya habari.
Balile alisema vyombo vya habari kwa sasa haviko huru kutoa taarifa mbalimbali kama mwanzo kutokana na hofu iliyojengeka miongoni mwa wananchi ambao wamekuwa wakisita kutoa maoni.
“Mazingira ya kazi kwa wanahabari yamekuwa magumu kutokana na baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola kuwabughudhi na kufanya uovu wa wazi dhidi yao wanapokuwa kazini.
“Matukio mbalimbali ya polisi kuwanyanyasa waandishi wa habari yakiwamo ya wanahabari kunyang’anywa simu zao, mfano yaliyotokea Dodoma kwa mwandishi kuporwa simu, kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda wa Mwananchi na kwingineko,” alisema Balile.
Mengine ni mauaji ya Kibiti, kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwiline, kuuawa askari wanane, kushambuliwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, vitendo ambavyo baadhi yake hadi sasa havijapata majibu wala wala wahusika kupatikana.
Alisema hali hiyo inawafanya waandishi na wananchi kwa ujumla kuwa na hofu hasa kwa wale wa habari za uchunguzi.
Balile alisema vyombo vya habari vilevile vimekuwa vikifanya kazi katika mazingira magumu na ya woga kutokana na watendaji wake kuitwa na kuhojiwa mara kwa mara na mamlaka kama vile Idara Habari (MAELEZO) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na hata wakati mwingine kupewa adhabu za kulipa faini au kufungiwa.
“Vituo vingine vitano vya televisheni kutozwa faini i na TCRA na kufungiwa kwa magazeti ni baadhi ya adhabu ambazo zimekuwa zikitolewa kinyume na Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016.
“Pia mitandao ya jamii ambayo ilikuwa njia mbadala ya umma au wananchi kujieleza na kupata habari nayo imeanza kuwekewa vikwazo baada ya kutungwa kanuni zinazotaka kusajiliwa kwa blogs na mitandao mingine, huku waendeshaji wake wakitakiwa kulipa ada,’’ alisema Balile.
Alisema suala la kuzuiwa mikutano ya vyama vya siasa ambavyo ilikuwa moja ya vyanzo vikubwa vya habari, kinyume na sheria ya nchi huku vyama vya upinzani vikionekana kuathiriwa zaidi, ikizingatiwa watendaji wa chama tawala (CCM) wanaonekana wakiendelea na shughuli za siasa katika sehemu mbalimbali nchini kwa hoja kuwa wanakagua utekelezaji wa ilani ya chama.
Kaimu Mwenyekiti huyo wa TEF alisema suala la kuzuia matangazo ya televisheni ya moja kwa moja kutoka bungeni kwa maelezo ya ukubwa wa gharama na kutoa fursa kwa wananchi kufanya kazi, huku kinyume chake yakiwapo matangazo mengi ya moja kwa moja katika muda uleule, yanayofanywa na taasisi nyingine za serikali.
Alisema kurushwa kwa matangazo hayo ya moja kwa moja na taasisi nyingine za hakujazuia wananchi kufanyakazi zao!
“Pia wanahabari wanashindwa kufanya kazi zao sawasawa kwa mfano uchaguzi mdogo mbalimbali uliofanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 uliambatana na matukio ya kuogofya yakiwamo mauaji ya watu na kujeruhiwa, hali ambayo iliwafanya waandishi washindwe kutekeleza wajibu wao inavyotakiwa,’’ alisema
Alisema vilevile kuna dalili za kuzorota kwa shughuli za uchumi kutokana na kufungwa kwa baadhi ya biashara na shughuli nyingine za uzalishaji mali, hali ambayo imesababisha ongezeko la ukosefu wa ajira.
“Baadhi ya vyombo vya habari kwa sasa vina hali ngumu na kushindwa kujiendesha kutokana na kuidai serikali na taasisi nyingine mamilioni ya fedha za matangazo ambazo endapo zingelipwa zingeweza kuvikwamua.
“Kufungwa kwa baadhi ya biashara au kushuka kwa mapato kwa baadhi ya kampuni kumeathiri biashara ya matangazo ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo cha mapato kwa vyombo vya habari,’’ alisema Balile.