26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JUKWAA LA WAHARIRI LATAKA MARIDHIANO YA KITAIFA

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


JUKWAA la Wahariri  Tanzania (TEF)  limetoa tamko la kutaka kuwapo maridhiano ya taifa kuhusu mustakabali wa nchi.

Limetaka mazungumzo hayo yashirikishe   makundi mbalimbali wakiwamo viongozi wastaafu, asasi za  raia, vyama vya  taaluma, makundi ya rika  mbalimbali kuweza kufanya mjadala huo kama alivyofanya Rais Dk. John Magufuli, alipokutana na wafanyabishara   Ikulu  Dar es Salaam, hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, alisema hivi sasa Taifa linashuhudia malalamiko mbalimbali kutoka kwa jamii jambo ambalo halileti afya kwa ustawi,  umoja na mshikamano wa Watanzania.

Alisema   tamko hilo ni maazimo ya wahariri wanachama wa TEF waliokutana juz.

Kwenye mkutano huo,  pamoja na mambo mengine, walijadili na kutafakari kwa kina hali na mwelekeo wa nchi kwa sasa ambako malalamiko yamekuwa mengi kwa makundi ndani ya jamii.

Alisema malalamiko hayo ambayo baadhi yamekuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari yamekuwa yakigusa sehemu kuu tatu ambazo ni kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni hasa kupitia vyombo vya habari, kuzorota  demokrasia nchini kwa ujumla wake na ukuaji wa uchumi ambao kwa sasa haulingani na hali ya maisha ya Watanzania.

Alisema kuminywa kwa uhuru wa kutoa  maoni  kimekuwa  kikwazo kikubwa cha utendaji na ufanisi katika vyombo vya habari.

Balile alisema vyombo vya habari  kwa  sasa haviko huru kutoa taarifa mbalimbali kama mwanzo kutokana na hofu iliyojengeka miongoni mwa wananchi ambao wamekuwa wakisita kutoa maoni.

“Mazingira ya kazi  kwa wanahabari yamekuwa magumu kutokana na baadhi ya watendaji wa vyombo  vya dola kuwabughudhi na kufanya uovu wa wazi dhidi yao wanapokuwa kazini.

“Matukio mbalimbali ya polisi kuwanyanyasa waandishi wa habari yakiwamo ya wanahabari kunyang’anywa simu zao, mfano yaliyotokea Dodoma kwa mwandishi kuporwa simu, kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda wa Mwananchi na kwingineko,” alisema Balile.

Mengine ni mauaji ya Kibiti, kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwiline, kuuawa  askari wanane, kushambuliwa kwa risasi  Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, vitendo ambavyo baadhi yake hadi sasa havijapata majibu wala wala wahusika  kupatikana.

Alisema hali hiyo inawafanya waandishi na wananchi kwa ujumla kuwa na hofu hasa kwa wale wa habari za uchunguzi.

Balile alisema vyombo vya habari vilevile vimekuwa vikifanya kazi katika mazingira magumu na ya woga kutokana na watendaji wake kuitwa na kuhojiwa mara kwa mara na mamlaka kama vile Idara Habari (MAELEZO) na Mamlaka ya  Mawasiliano Tanzania (TCRA) na hata wakati mwingine kupewa adhabu za kulipa faini au kufungiwa.

“Vituo vingine vitano vya televisheni kutozwa faini i na TCRA  na kufungiwa kwa magazeti ni baadhi ya adhabu ambazo zimekuwa zikitolewa kinyume na Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016.

“Pia mitandao ya  jamii ambayo ilikuwa njia mbadala ya umma au wananchi kujieleza na kupata habari nayo imeanza kuwekewa vikwazo baada ya kutungwa   kanuni zinazotaka kusajiliwa kwa blogs na mitandao mingine, huku waendeshaji wake wakitakiwa kulipa ada,’’ alisema Balile.

Alisema suala la kuzuiwa   mikutano ya vyama vya siasa ambavyo ilikuwa moja ya vyanzo vikubwa vya habari, kinyume na sheria ya nchi  huku vyama vya upinzani vikionekana kuathiriwa zaidi, ikizingatiwa   watendaji wa chama tawala (CCM) wanaonekana wakiendelea na shughuli za  siasa katika sehemu mbalimbali nchini kwa hoja kuwa wanakagua utekelezaji wa ilani ya chama.

Kaimu Mwenyekiti huyo wa TEF alisema suala la kuzuia matangazo ya televisheni ya moja kwa moja kutoka  bungeni  kwa maelezo ya ukubwa wa gharama na kutoa fursa kwa wananchi kufanya kazi, huku kinyume chake yakiwapo matangazo mengi ya moja kwa moja katika muda uleule, yanayofanywa na taasisi nyingine za serikali.

Alisema  kurushwa kwa matangazo hayo ya moja kwa moja na taasisi nyingine za hakujazuia wananchi kufanyakazi zao!

“Pia wanahabari wanashindwa kufanya kazi zao sawasawa kwa mfano   uchaguzi mdogo mbalimbali uliofanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015  uliambatana na matukio ya kuogofya yakiwamo mauaji ya watu na kujeruhiwa, hali ambayo iliwafanya waandishi washindwe  kutekeleza wajibu wao  inavyotakiwa,’’ alisema

Alisema vilevile kuna dalili za kuzorota kwa shughuli za  uchumi kutokana na kufungwa kwa baadhi  ya biashara na shughuli nyingine za uzalishaji mali, hali ambayo  imesababisha ongezeko la ukosefu wa ajira.

“Baadhi ya vyombo vya habari kwa sasa vina hali ngumu na kushindwa kujiendesha kutokana na kuidai serikali na taasisi nyingine mamilioni ya fedha za matangazo ambazo endapo zingelipwa zingeweza kuvikwamua.

“Kufungwa kwa baadhi ya biashara au kushuka kwa mapato kwa baadhi ya kampuni kumeathiri biashara ya matangazo ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo cha mapato kwa vyombo vya habari,’’ alisema Balile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles