25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AZITAKA MAMLAKA ZIJITATHMINI AJALI BARABARANI

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli, amelitaka Jeshi la Polisi, Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa na wilaya na mamlaka zote zinazohusika na usalama wa barabarani kujitathmini, na kutafuta majawabu ya kwanini ajali zinaendelea kutokea kwa kusababishwa na uzembe na uvunjaji wa sheria za barabarani.

Kauli hiyo aliitoa jana katika salamu zake za pole kutokana na ajali ya basi la Kampuni ya City Boy iliyosababisha vifo vya watu 12 wilayani Igunga mkoani Tabora juzi usiku.

“Viongozi wa idara hiyo wanapaswa kujitafakari kwanini ajali nyingi zimekuwa zikitokea katika maeneo yaleyale na kutafuta ufumbuzi, ili kuepusha madhara ya watu kupoteza maisha, kupata ulemavu wa kudumu na kupoteza mali,” alisema katika taarifa yake iliyotolewa na Ikulu.

Basi hilo lililokuwa linatoka Karagwe mkoani Kagera kuelekea Dar es Salaam, liligongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso lililokuwa linatoka Njombe kwenda Mwanza.

“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 12 iliyotokea Wilaya ya Igunga. Nawapa pole wafiwa wote, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mkubwa,” alisema Rais Magufuli.

Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote, na amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wote 46 wapone haraka ili waungane na familia zao katika ujenzi wa taifa.

 

MWIGULU

Akitoa taarifa jana bungeni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, ameagiza dereva yeyote atakayekamatwa akiwa kwenye mwendo kasi, pamoja na kutozwa faini, awekwe mahabusi na kisha mahakamani.

Hayo aliyasema wakati akijibu mwongozo ulioombwa asubuhi na Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlanga (CCM), akihoji kama dereva akikutwa kwenye mwendo kasi anatozwa faini, je ajali ikisababishwa na ubovu wa barabara kama Wakala wa Barabara (Tanroads), itozwe fani ama laa.

Akijibu mwongozo huo, Mwigulu alisema: “Taarifa za awali tulizopewa, chanzo cha ajali hiyo siyo mashimo ya barabarani peke yake, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi.

“Dereva yule alikuwa anaenda mwendo kasi sana, alipokutana na shimo lile gari likakata kifaa kimoja cha kwenye matairi, gari ikapoteza mwelekeo ndipo likaenda kugonga lile basi la abiria.

“Kwa maana hiyo, kama alikuwa anaenda kwa mwendo unaostahili, yale hayakuwa mashimo ya kusababisha ajali, kwa sababu magari yalipita siku nzima yeye akaja kupata ajali baadaye, kwahiyo tatizo lilikuwa lilelile, mwendo kasi.

“Kwa kuwa watu wameshazoea mambo ya kutozwa faini na anaona sisi tunatafuta fedha, naelekeza Jeshi la Polisi popote pale watakapokamata dereva anaenda mwendo kasi pamoja na kutoza faini, wamuweke ndani mpaka watakapompeleka mahakamani ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa,” alisema Dk. Mwigulu.

 

POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa, alisema ajali hiyo ilitokea Aprili 4, mwaka huu saa 2 usiku, chanzo kikiwa ni lori aina ya Mitsubishi lenye namba T 486 ARB kupasuka tairi ya kulia na kuathiri mfumo wa usukani na kupoteza mwelekeo, hivyo kugongana na basi hilo lenye namba za usajili T 983 DCE aina ya Scania lililokuwa likitokea Karagwe mkoani Kagera kwenda Dar es Salaam.

Alisema dereva wa basi hilo, Emmanuel Chitemo (39) mkazi wa Dar es Salaam, alifariki papo hapo na dereva wa lori hilo lililokuwa likitokea Njombe kwenda Mwanza likiwa limebeba shehena ya viazi nviringo, Salum Abdallah (25) mkazi wa Ruvuma ametoroka na polisi wanaendelea kumsaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles