Na CLARA MATIMO
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku halmashauri zote nchini kuwatoza wanunuzi wa mazao ushuru wa huduma kabla ya kununu mazao hayo.
Agizo hilo alilitoa juzi alipozungumza na wadau wa zao la pamba wakiwamo wakulima, wataalamu wa kilimo, wanunuzi na wamiliki wa vinu vya kuchambua pamba.
Wengine ni watendaji kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Waziri wa Fedha, taasisi za fedha na viongozi mbalimbali wakiwamo na wakuu wa mikoa ya Mwanza, Geita Tabora, Simiyu na Mara.
Alisema kuanzia msimu huu wa kilimo cha pamba, kila mfanyabiashara anayenunua zao hilo hapaswi kulipa fedha taslimu kama ilivyokuwa zamani ambako wanunuzi walikuwa wakilipa fedha taslimu hivyo kuleta mgogoro baina ya wafanyabiashara na halmashauri hizo.
Majaliwa alisema katika utaratibu wa zamani wafanyabiashara walikuwa wakilipia fedha lakini wakati mwingine walikuwa wanaweza kukwama kununua pamba.
Alisema wafanyabiashara wamekuwa wakikwama kurejeshewa fedha zao hivyo ameamua kufuta utaratibu huo na badala yake watalipa wanaponunua kulingana na kiasi walichonunua.
“Mfanyabiashra anaweza kulipa kiasi fulani cha fedha, lakini akienda kununua anakosa kufikia kiwango alichokuwa anakitaka na fedha zote za serikali huwa zina matumizi, zikiingia wakurugenzi huzipangia matumizi tayari,” alisema.
Waziri Mkuu alisema ushuru wa mazao anaopaswa kulipa mfanyabiashara ni asilimia tatu ya kile alichonunua.
Kwa sababu hiyo aliwaonya wakurugenzi kutoendelea na utaratibu wa zamani akisema serikali italisimamia hilo kwa lengo la kulinda mitaji wa wafanyabiashara.
Hata hivyo aliwataka wakurugenzi wote ambao wanadaiwa ushuru huo na wanunuzi wa zao hilo katika msimu uliopita, wafanye utaratibu wa kuwalipa fedha zao kuondoa migogoro.
Waziri Majaliwa alisema atakutana tena na wanunuzi na wadau wa zao hilo kabla ya msimu kuanza Mei Mosi mwaka huu ili wapange bei.