31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MUTUNGI AKILIMA BARUA CHADEMA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amekiandikia barua Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akihoji kwanini kisichukuliwe hatua kwa kufanya maandamano kinyume cha taratibu wiki iliyopita.

Februari 16, mwaka huu Chadema kupitia viongozi wake waandamizi, waliandamana kuelekea Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao ambao wangesimamia uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika Jumamosi iliyopita.

Maandamano hayo ndiyo yaliyosababisha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini kuuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliliambia MTANZANIA jana kuwa wamepokea barua ya msajili na kwamba watamjibu leo.

“Ni kweli tumepokea barua ya msajili leo (jana) akitutaka tujieleze kwanini tusichukuliwe hatua kwa kufanya maandamano Februari 16 mwaka huu.

“Pamekuwepo na jitihada nyingi sana za kukihusisha chama na viongozi wake kwenye jinai mbalimbali. Barua hii ni mwendelezo wa jitihada hizo.

“Maandamano ni haki ya vyama kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na kanuni zake, ni haki inayotolewa na Katiba yetu.

“Aidha, kama kuna jinai yoyote ni suala la polisi na si kazi za msajili wa vyama…kesho (leo) tutaijibu barua ya msajili,” alisema Mrema.

Jumatatu wiki hii, Chadema kilipokea barua kutoka Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ikiwataka viongozi saba walioongoza maandamano hayo kuripoti polisi.

Viongozi hao ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji, Manaibu Katibu Mkuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee, Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Mweka Hazina wa Bawacha, Esther Matiko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles