32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

FAMILIA YAMFUNGA MDOMO BABU SEYA

 

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


FAMILIA ya Mwanamuziki Nguza Viking maarufu kama ‘Babu Seya’ imeamua kumzuia yeye na   mwanae Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ kuzungumza na vyombo vya habari hadi katikati ya wiki.

Babu Seya na Papii waliachiwa huru juzi saa 12.08 jioni baada ya Rais Dk. John Magufuli kuwapa  msamaha.

Akizungumza na MTANZANIA jana,  Mwanamuziki ambaye yuko karibu na familia hiyo, Nyoshi El Sadaaty alisema familia imefanya uamuzi huo   kuwapa muda wa kutosha kupumzika.

Alisema kutokana na kuwa katika hali ya uchovu na mshangao huenda wakazungumza mambo ambayo hawastahili kuyazungumza.

“Familia iliamua wasizungumze na vyombo vya habari hadi Jumanne au Jumatano ili wapumzike na wajipange cha kuzungumza kwa jamii,” alisema Nyoshi.

Alisema kwa sasa Babu Seya na Papii wako katika nyumba yao mpya ya Tegeta ambayo walinunua baada ya kuuza ile ya Sinza.

“Nguza na Papii wako Tegeta kwa sasa lakini familia iko Kimara Stopover ambako nako walinunua nyumba,” alisema Nyoshi.

Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi, juzi Babu Seya na Papii hawakuzungumza chochote bali waliingia katika gari dogo la rangi ya fedha na kwenda katika Kanisa la Life Christ Ministry lililopo Segerea mwisho jijini Dar es Salaam ambako mtoto wake aliyeachiwa huru mwaka 2010 Nguza Mbangu ni mchungaji.

Walipofika hapo waliingia na kupiga picha kabla ya kuondoka huku wakiomba waachwe wapumzike na kuahidi kuzungumza  jana.

Akihutubia juzi katika kilele cha sherehe za miaka 56 ya Uhuru mjini Dodoma, Rais Magufuli alisema ameamua kutekeleza kwa vitendo Ibara ya 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema:

“Bila kuathiri masharti mengine   katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Rais anaweza kutenda yoyote kati ya mambo yafuatayo;

“A. kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote na anaweza kutoa msamaha huo ama kwa masharti au bila sharti lolote kwa mujibu wa sheria.

“B. Rais anaweza kumuachia kabisa mtu yeyote aliyehukumiwa au kuadhibiwa kwa kosa lolote ili mtu huyo asitimize adhabu hiyo wakati wa muda maalum.

“C.Kulinganisha adhabu na tahfif waswahili wanajua tafsiri yake vizuri kina Kikwete (Rais wa awamu ya nne) sisi wa bara ni ngumu.

“Ibara hii pia ninatoa msamaha kwa familia ya Nguza Viking jina jingine Babu Seya na mwanae Johnson Nguza ‘Papii Kocha, nao waachiwe huru,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha ni 666 kati yao wanaume ni 655 na wanawake ni 11.

Rais Magufuli alisema pia kuwa ameamua kuwasamehe wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa na kuwataka wahusika wafanye mchakato wa kuwatoa juzi ama jana.

“Kwa mujibu wa Ibara hii na hasa ukizingatia sisi ni binadamu nimeamua kuwasamehe wafungwa 8,157.

“Wafungwa 1,828 watatoka leo(juzi) na 6,329 wamepunguziwa muda wa kukaa gerezani  na watatoka kwa mujibu wa vifungo vyao.

“Lakini pia kwa mujibu wa ibara hiyo hiyo wapo waliohukumiwa kunyongwa wapo wenye umri wa zaidi ya 85 pia wapo waliotubu kweli dhambi zao,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles