25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ASHTUKA MWENYEKITI UVCCM KUNASWA KWA RUSHWA

Bakari Kimwanga na Ramadhan Hassan-DODOMA


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli, ameeleza masikitiko yake jinsi baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Vijana wa Chama hicho (UVCCM), walivyoshindwa kuenzi misingi ya chama hicho baada ya  mwenyekiti wa umoja huo, Sadifa Juma Khamis kutiwa mbaroni na Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Sadifa alikamatwa juzi jioni mjini hapa na maofisa wa Takukuru kwa tuhuma za kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa UVCCM akidaiwa kuwashawishi wamchague mmoja wa wagombea aliyekuwa akimuunga mkono.

Kamanda wa Takukuru  Mkoa wa Dodoma, Emme Kuhanga, alithibitisha kukamatwa kwa kiongozi huyo wa UVCCM.

Akifungua mkutano huo   mjini hapa jana, Rais Dk. Magufuli alisema  baadhi ya vijana wamepoteza dira tofauti na viongozi wa zamani ambao walikuwa wakiandaliwa vema kuwa viongozi wa baadaye.

“UVCCM ya zamani siyo sawa na hii ya sasa. Vijana wa sasa wanakwenda kwenye mikutano wanapigana, wengine wanatoa rushwa.

“Ninavyozungumza hapa, mwenyekiti wenu (Sadifa Juma Khamis) yupo lock-up kwa kushikwa na rushwa. Huo ndiyo umoja wa vijana tuliokuwa tunakwenda nao, sitaki kusema sana.

“Mimi nina imini sana na vijana, mkiamua jambo mnaweza ila bahati mbaya kuna wachache mlipotezwa na watu fulani fulani hapa kati.

“Ningependa ieleweke kwamba ujana pekee haukufanyi uwe hazina kwa chama au taifa. Ni lazima uwe mzalendo, mchapakazi, muadilifu na kadhalika, hizo ndizo baadhi ya sifa za kijana.

“Kijana ambaye ni fisadi, mvivu, mla rushwa, tapeli, mtumia dawa za kulevya na kadhalika, ana mchango mdogo kwa taifa. Nimeanza kueleza kwa kutaja sifa hizo za kijana kwa makusudi kabisa,” alisema Rais Magufuli

Kutokana na kukamatwa kwa Sadifa  leo ndipo itajulikana hatima yaka kama atafikishwa mahakamani au la.

Rais alisema   pamoja na kusaidiwa na vijana wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, lakini alishangazwa  na umoja huo kushindwa kumpa orodha ya vijana wanaofaa katika uongozi.

“Niwaeleze ukweli, vijana walinisaidia sana wakati wa kampeni lakini nashangaa nimekuwa nikiletewa majina ya wanaopendekezwa kwa nafasi mbalimbali ila sikuletewa hata jina moja kutoka UVCCM.

“Vijana wengi wa UVCCM walikosa nafasi mbalimbali za uteuzi. Lazima wajumbe mumtangulize Mungu mbele kwa kutambua wajibu wenu kwenye uchaguzi huu kwa sababu  mtakaowachagua ndiyo watakuwa washauri wangu,” alisema.

KIONGOZI BORA

Rais Dk. Magufuli aliwashangaa wanaotoa rushwa ili wachaguliwe wakati yeye hakutoa hata senti moja kuwahonga wajumbe  wamchague.

“Mimi nasema ukweli hata Mungu ananisikia, sikutoa hata senti moja ili nichaguliwe.

“Nitashangaa sana kama mtamchagua mwenyekiti aliyewahonga. Kila mwenye uwezo kwenye umoja wa vijana amewekewa vigingi vya kila aina, nawaomba wajumbe tuanzishe ukurasa mpya UVCCM.

“Kuonyesha ni kiasi gani ninavyowaamini vijana, kwenye Serikali yangu nimeteua vijana wengi na hawajaniangusha. Msichague mtu kwa sababu ya dini yake, kabila lake, mnatoka ukanda mmoja au fedha zake  ila chagueni mtu sahihi mwenye sifa za kuwa kiongozi.

“Ninahitaji mchague viongozi wazuri watakaofanya kazi kuliko ilivyo sasa ambako umoja wetu una vitega uchumi, lakini fedha hazijulikani zinakokwenda.

“Pale wana jengo kubwa la UVCCM, lakini wameishia kugawana vyumba tu. Ila kwa dhati ninampongeza Shaka (Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM), amefanya kazi kubwa,” alisema.

VIJANA NA KUJITAMBUA

Akizungumzia eneo hilo  aliwataka vijana wajitambue kwa kuwa huu ni wakati wao wa kushika uongozi.

“Ninawaomba vijana wa UVCCM mjitambue kwa sababu huu ni wakati wenu wa kushika dola.

“Nisingependa kuona sisi tunaondoka halafu anachukua kijana anayepokea rushwa, tutakuwa tumeliuza taifa na kukiuka misingi tuliyoachiwa na waasisi wetu.

“Kwa sababu kama kiongozi anapokea rushwa, hata akiteuliwa kuwa waziri, atapokea rushwa tu na anaweza kumuuza hata mshikaji wake kwa rushwa.

“Mimi siyo rais wa maisha, muda wangu utaisha kama itakavyokuwa kwa Dk. Shein (Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar),” alisema Rais Dk. Magufuli.

Aliwaomba vijana wa CCM wajiamini kwa kujibu hoja wala wasisubiri kuambiwa.

“Bahati nzuri mimi huwa nasoma, nimemuona Msando akitumia taaluma yake ya sheria kujibu hoja kuhusu ibara ya 45 jana (juzi) na sikumtuma ila alisukumwa na profession yake ya sheria.

“UVCCM ilikuwa ni jumuiya ya watu wenye uwezo ambao baada ya kukatishwa tamaa waliamua kuhama na kwenda kwenye vyama vingine, lakini leo wanarudi walikotoka.

“Hata Profesa Kitila (Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Umwagiliaji), alijaribu kugombea, lakini akazuiwa na kwenda alikokuwa, lakini sasa amerudi,” alisema.

AVUNJA BODI UVCCM

Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo wa CCM alihoji kazi za bodi ya wadhamini ya UVCCM kwa kuwa haiwanufaishi vijana.

“Leo ndiyo uchaguzi na bodi nayo iondoke … hii hata kama wapo kina Lukuvi (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) iondoke tu.

“Na nyie viongozi mliopita ndani ya umoja kama kina Mavunde, muwe mnakuja kuzungumza na viongozi angalau hata kwa kunywa maji na kushauriana, kumbukeni mlipotoka, hilo ni jambo jema,” alisema.

Awali, akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa wajumbe wa mkutano mkuu huo, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema wanachama wameongezeka kutoka 200,000 hadi kufikia milioni 1.7.

Kwa mujibu wa Shaka, UVCCM imetoa asilimia ipatayo 75 ya watu kwenda kufanya kazi kwenye jumuiya nyingine ikiwamo serikalini.

“Kuanzia mwaka 2012 hadi sasa, UVCCM ngazi ya taifa imefanya ziara kwenye mikoa yote nchini na imeendelea kushiriki na kuwa chachu ya ushindi kwenye uchaguzi mbalimbali wa Serikali.

“Jumuiya imeendelea kufanya uhakiki wa mali zake, tumenunua magari mawili mapya na tumeruhusu jumuiya ifanyiwe ukaguzi wa hesabu.

“Kwa hiyo, Dk. Magufuli tunakuomba utupatie eneo mkoani Dodoma tuwekeze kisasa ikiwamo kujenga jengo la kudumu litakalozinduliwa mwishoni mwa mwaka 2018.

WANACHAMA WAPYA

Katika mkutano huo, wanachama wapya waliojiunga na CCM walizungumza.

Aliyekuwa wa kwanza ni aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF).

Katika maelezo yake, alisema  ameacha kila kitu na kujiunga CCM kutokana na kuridhishwa na utendaji wa Serikali.

Naye aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini, kupitia NCCR-Mageuzi, Moses Machali, alisema alilazimika kuhamia CCM kwa kuwa kuna timu ya ushindi.

Aliwataka UVCCM kutumia mitandao ya  jamii kwa kuwa vyombo vya habari vinaweza kuyafanya mambo mazuri yaonekane ni mabaya na mabaya yaonekane ni mazuri.

Naye  aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia NCCR-Mageuzi, David Kafulila,  alisema aliamua kuhamia CCM kwa sababu ajenda ya ufisadi imehama.

“Sasa kuna utu na usawa nchini. Tanzania ya sasa imebadilika. Tunashuhudia matajiri wakilazwa mahabusu.

“Hii imesababisha  kiwango cha ufisadi kupungua nchini. Dhamira ya Dk. Magufuli haina shaka na uzalendo wake ni wa kuigwa,” alisema Kafulila.

Aliyekuwa Mwanasheria wa ACT-Wazalendo, Albert Msando, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuwachagua viongozi wasafi.

Wakati hao wakisema hayo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Chadema, Patrobas Katambi, aliwataka UVCCM kutoruhusu watu wengine kutumia nafasi nyingine za demokrasia kuvuruga amani ya nchi.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles