Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MWANDISHI wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, aliyekuwa akiripoti kutoka Rufiji mkoani Pwani, amepotea kwa siku tisa sasa, huku mkewe akisema mara ya mwisho alionekana katika gari nyeupe aina ya Toyota Land Cruiser ikiwa na watu wengine wanne ambao pia walipekua nyumba yake.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi (MCL), Francis Nanai, ilisema kampuni hiyo ilipokea taarifa za kutoweka kwa mwandishi wake Novemba 30, mwaka huu.
Katika taarifa hiyo, Nanai alisema kwa mujibu wa Anna Pinoni (35), ambaye ni mke wa Gwanda, Novemba 21 mwaka huu, watu wanaokadiriwa kuwa wanne wakiwa na gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe walifika katikati ya mji wa Kibiti.
Alisema baada ya gari hilo kumchukua Gwanda, lilielekea shambani kwake majira ya saa 4:00 asubuhi na kumkuta mkewe Anna akiwa shambani.
“Gwanda aliyekuwa amekaa siti ya nyuma katika gari hilo, alimwita mkewe kutokea upande huo wa gari na kumwuliza alikokuwa ameweka ufunguo wa nyumba yao.
“Mkewe alisogea katika gari na kuongea naye kutokea dirishani na kumwelekeza mahali alipoficha ufunguo, huku Gwanda akimwambia kuwa amepata safari ya dharura na kwamba kama asingerudi siku hiyo (Jumanne ya Novemba 21, 2017), basi angerudi siku inayofuata (Jumatano ya Novemba 22, 2017).
“Gari hilo liliondoka kwa kurudi kinyumenyume hadi njiapanda na kuelekea nyumbani kwa mwandishi huyo. Mkewe aliporudi nyumbani aligundua kuwa kuna upekuzi ulikuwa umefanyika kwa sababu alikuta vitu viko shaghalabaghala.
“Tangu siku hiyo, Gwanda hajaonekana tena, namba zake tatu za simu za mkononi hazipatikani. Tayari mkewe Anna amekwisharipoti tukio hilo tangu Alhamisi ya Novemba 23 katika Kituo cha Polisi Kibiti na kupewa RB namba Kibiti/RB/1496/2017,” alisema Nanai.
Aidha alisema polisi wameahidi kufanya uchunguzi, lakini hadi sasa hakuna taarifa zozote zilizotolewa.
Nanai alisema kwa mara ya mwisho, Gwanda aliwasiliana na ofisi za Mwananchi Jumatatu ya Novemba 20 mwaka huu kwa majukumu ya kikazi.
Kutokana na hali hiyo, Nanai alisema MCL inafuatilia suala hilo kwa ukaribu kwa kushirikiana na familia yake, huku wakitoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa haraka kuwezesha kupatikana kwa mwandishi huyo.
Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Rufiji, Kamishna Onesmo Lyanga alisema: “Niko nje ya ofisi hivyo siwezi kufahamu hiyo taarifa vizuri.”