23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

CUF YAELEZA MBUNGE WAO ALIVYOWASALITI WANANCHI

ASHA BANI Na CHRISTINA GAULANGA-DAR ES SALAAM


CHAMA cha Wananchi (CUF) upande unamuunga mkono Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba, kimesema hatua ya aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia kujiuzulu ni sawa na kuwasaliti wananchi waliomchagua.

Kwa sababu hiyo kimewaomba radhi wananchi wa Kinondoni  ambao waliamini mbunge huyo anafaa kumbe amekuwa msaliti wa kwanza kwao.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Abdul Kambaya alisema   Mtulia alikihadaa chama na wananchi wakamuona anafaa kumbe alikuwa na lengo la kuwasaliti.

Kambaya alisema alichokifanya Mtulia, CUF hakikushtuka kulingana na historia yake kwa sababu  alikuwa na viashiria vya usaliti ikiwamo tukio la kukosea kujaza fomu za kugombea ubunge mwaka 2015 ambalo lilizua utata.

“Kwetu sisi jambo hili tunaona si fedheha kwa CUF bali ni kwa Mtulia na familia yake na kwa manung’uniko ya wapiga kura waliotegemea mabadiliko kupitia kwake, katu hayawezi kumuacha salama, Mungu atasikia kilio chao,” alisema.

Alisema utetezi alioutoa Mtulia kuwa anajiondoa CUF kwa sababu ya kuridhika na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano hauna uzito kwake wala jamii.

“Hatuoni sababu aliyoitoa Mtulia kama ina nguvu kwetu kwa sababu kumuunga mkono Rais Dk. John.Magufuli si lazima uhamie CCM,”  alisema Kambaya.

Mkurugenzi huyo wa Uenezi wa CUF alisema wanachokiona ni baadhi ya viongozi wanaochaguliwa hasa wanapopata umaarufu kujiweka sokoni kwa ajili ya kuvizia nafasi za uongozi.

“Katika mpango huu wa Mtulia pia tunaona hakuwa na mawasiliano mazuri na baadhi ya wana CCM hivyo Mungu atalipa malalamiko ya wapiga kura wake,” alisema Kambaya.

Alisema Mtulia anafahamu fika watu walivyokesha kwa siku tatu Viwanja vya Biafra kusubiri atangazwe katika wadhifa wake wa ubunge hivyo kujiondoa kwake, dhambi hiyo itamtesa.

Kambaya alisema historia ya chama hicho inaonyesha tukio la kujiuzulu   liliwahi kutokea   miaka iliyopita  kwa aliyekuwa Mwakilishi wa Mkunazini, Salum Msabaha ambaye aliachia jimbo hilo kwa kisingizio cha kutekwa lakini baadaye alijiunga na CCM.

“Uamuzi wa kujiondoa kwenye chama ni utashi wake na hatuamini kama ameshawishiwa na Serikali au CCM,” alisema Kambaya.

Alisisitiza CUF ipo imara katika kusimamia na kutekeleza ilani ya chama hicho kwa mgombea atakayeteuliwa na chama kwa kuhakikisha wanarejesha jimbo hilo katika himaya yao.

“Mwenye kununua utu wake tatizo lake ni dogo kuliko wewe unayekubali kuuza utu na heshima yako,” alisema Kambaya.

MTULIA RASMI CCM

Jana   Maulid Mtulia alijiunga rasmi na CCM na kukabidhiwa kadi ya chama hicho katika hafla iliyofanyika tawi la CCM Ali Maua A.

Mtulia alikabidhiwa kadi hiyo mchana kwa shamrashamara na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Aroun Maluma.

Baada ya kukabidhiwa kadi hiyo, Mtulia alisema ana sababu zake za msingi zilizomfanya kukihama CUF.

Aliitaja sababu ya kwanza ya kuhama CUF kuwa ni migogoro isiyoisha ndani ya chama hicho kiasi cha kwamba inamfanya kushindwa kuendelea kufanya mambo yake mengine ya kuwahudumia wananchi waliomchagua.

Mtulia alisema kwa yeye kuwa upinzani alishindwa kutumika kama daraja kwa wananchi wake kwa kuwa mambo mengi yaligoma kuendelea baada ya kushindwa kusaidiwa na Serikali inayoongozwa na CCM.

Alisema ndiyo maana hata Rais Dk. John Magufuli alipofika kutembelea wakazi wa Magomeni Kota waliobomolewa kupisha ujenzi wa nyumba bora, alimuomba kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa wakazi hao.

“Ningekuwa kama wapinzani wengine walivyo katika mkutano ule wa Rais nisingeweza kufika na kero za wananchi zisingeweza kuwasilishwa pale, mimi niko tofauti.

“Mimi nimeamua mwenyewe sina ugomvi na CUF kwa sababu  ndiyo chama changu cha kwanza, kimenilea vizuri, kimenitunza katika maadili mema, sikuwa na ugomvi na mtu lakini kutokana na hayo yanayoendelea nimeamua kukihama.

“Naahidi kwa waliokuwa CUF wananifahamu nidhamu niliyokuwa nayo nikiwa huko, nidhamu hiyo nitakuja kuiendeleza nikiwa huku na kama nitakuwa nimekosea basi mtanirekebisha na kuendelea kukijenga chama chetu,’’ alisema Mtulia.

Alisema awali upinzani walikuwa wakisema mambo hayaendi serikalini lakini kwa sasa kila kitu kipo shwari kutokana na  utendaji wa taasisi za serikali.

Hata hivyo alisema katika CCM hakufuata cheo bali  amefuata chama lakini hata kama kutakuwa na nafasi ya kufanya kazi serikali za mitaa atafanya na kama zimejaa atakwenda kwao Rufiji kuvua.

“Mimi sina shida kama mnafikiria, nimetoka CUF kwa ajili ya kuingia CCM kufuata vyeo siyo kweli.

Nikishindwa kila kitu ni bora nirudi zangu Rufiji   kuvua samaki,’’ alisema Mtulia.

Naye Mwenyekiti wa CCM Kata Tandale,  Tamimu Omari,   alidai Chadema na CUF vipo kama Saccos na si kuletea maendeleo kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles