27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

NYUFA HOSTELI UDSM ZAZUA MJADALA

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


NYUFA za majengo ya hosteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), zimezua mjadala kuhusu ubora wa majengo hayo.

Taarifa za nyufa hizo zilianza kusambaa juzi jioni katika mitandao ya kijamii, hali iliyowafanya wataalamu wa Wakala wa Majengo (TBA) kuanza kufanya uchunguzi wa nyufa hizo zilizopo katika jingo la Block A.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Msanifu Majengo, Elius Mwakalinga, alisema nyufa hizo ni za kawaida kwa mujibu wa mwongozo wa wabunifu majengo.

Alisema nyufa hizo zilizopo Block A – moja kati ya majengo sita yaliyopo eneo hilo, zilitarajiwa na hazina madhara yoyote kwa binadamu.

Mwakalinga alisema kuna makosa yalifanyika ya kuziba nyufa zilizoachwa kwa kutumia saruji badala ya mbao au plastiki maalumu, hivyo kuruhusu kuonekana.

Mtendaji huyo wa TBA, alisema majengo mapana huwekewa nafasi ambayo hutenganisha na kuwa sehemu mbili ili kusaidia kuruhusu jengo kupumua inapotokea hitilafu ya udongo, kutanuka na kusinyaa kwa udongo kutokana na hali ya hewa.

“Kutokea kwa nyufa katika jengo letu hili la hosteli si kwa sababu ya upungufu wa ubunifu ujenzi, bali kumetokea katika maeneo yaliyokusudiwa na kitaaluma hutokea hivyo na tayari tumeanza kuchukua hatua kurekebisha,” alisema Mwakalinga.

Alisema katika ukaguzi wa awali uliofanywa na wataalamu wa TBA, ilionekana upande mmoja wa hilo eneo lenye nyufa uko vizuri kwani ule uwazi ulionekana kufunikwa na kipande cha ubao bila kujazwa udongo wa saruji.

“Upande wa pili wa ule uwazi ulijazwa kimakosa udongo wa saruji na kuondoa urahisi wa sehemu mbili za jengo hilo kupumua,” alisema Mwakalinga.

Alisema wataalamu hao wamebaini upande wa pili wa uwazi uliojazwa udongo ndio unaoonyesha dosari za nyufa zilizojitokeza kutokana na lipu kwenye ukuta mzima wa sehemu ile kuungana na ule udongo ulioingia kwenye maungio.

“Katika ukaguzi wa awali uliofanywa na wataalamu wa TBA, ilionekana upande mmoja wa ile ‘Expansion Joint’ uko vizuri, kwani ule uwazi (gap) umeonekana kufunikwa na kipande cha ubao bila kujazwa na udongo wa saruji,” alisema.

Alisema kitaalamu dosari hiyo ni ya kawaida kutokea, kwa hiyo TBA imeanza kuchukua hatua za haraka kusahihisha kwa kuhakikisha kuwa ule uwazi unakuwa huru bila kujazwa kitu kigumu.

“Sehemu za ukuta zinazopakana na hilo eneo nyufa zake zitarekebishwa na kwa majengo mengine yatahakikiwa ili kuwa huru bila kuingiliwa na kitu kigumu,” alisema Mwakalinga.

TBA imewatoa hofu watumiaji wa majengo hayo kuwa ni salama na kwa matumizi yaliyokusudiwa na maeneo yaliyotokea hitilafu yatarekebishwa.

 

WANAFUNZI KUTOHAMISHWA

Mwakalinga alisema kwa kuwa majengo hayo bado yapo chini ya TBA, waatanza kufanya marekebisho na hakuna haja ya kuwahamisha wanafunzi kuwapeleka sehemu nyingine.

Alisema katika majengo hayo kuna vyumba 960 vyenye uwezo wa kubeba wanafunzi zaidi ya 3,800 na kila chumba gharama yake ni sawa na Sh milioni 10.4.

Kwa upande wake, Meneja wa hosteli hizo, Joseph Buhenyenge, alisema hosteli hizo ziko salama na taarifa zilizoenea katika mitandao zina nia mbaya.

Alisema anachoamini wanafunzi wake wako salama na wataendelea kumsaka aliyesambaza taarifa hizo ili aeleze alikuwa na dhumuni gani.

 

MWANAFUNZI AKAMATWA

Taarifa zilizolifikia Gazeti la MTANZANIA zinadai kuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa chuo hicho, Kumbusho Dawson, alikamatwa na polisi jana mchana kwa tuhuma za kupiga picha katika hosteli hizo na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu, Mkurugenzi Mstaafu wa Haki za Wanafunzi (TSNP), Shitindi Venance, ambaye pia ni Waziri Mstaafu wa Mikopo UDSM, alithibitisha kukamatwa kwa mwanafunzi huyo ambaye alidai alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Alisema mwanafunzi huyo anatuhumiwa kupiga picha hosteli hizo.

Venance alisema kuwa kukamatwa kwake kunatafsiriwa kuwa ni mwendelezo wa ujenzi wa taifa bubu la wasio na hoja.

Kutokana na hali hiyo Venance alitoa wito kwa wanafunzi wote nchini kupaza sauti kwa lengo la kupongeza kunakostahili na wasilale usingizi wakajisahau.

Alisema Dawson awe chachu ya kuamka na kupaza sauti kwa wanafunzi wote nchini kama ambavyo mwanafunzi mmoja alivyouawa wakati wa maandamano mwaka 2015 kwa kupigwa risasi walipokuwa wakilalamikia uhaba wa hosteli.

 

POLISI

MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ili kupata ufafanuzi wa kukamatwa kwa mwanafunzi huyo, alisema bado hajapata taarifa hizo.

“Bado sijapokea taarifa kamili kuhusu tukio hilo na endapo nitazipata na kuzifanyia uchunguzi nitawajulisha,” alisema.

Hosteli hizo za JPM zilijengwa kwa miezi minane na ujenzi wake uligharimu Sh bilioni 10 hadi kukamilika na kuzinduliwa na Rais Dk. John Magufuli Aprili 15, mwaka jana.

 

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles