Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
LIGI Kuu Tanzania Bara imeendelea kushika kasi, timu zote zikionyesha upinzani mkali katika mbio za kuwania taji hilo linaloshikiliwa na Yanga.
Vita hiyo inaongozwa na timu tatu za Simba, Azam na Yanga, ambazo hadi sasa hazijapoteza mchezo wowote katika michezo 11 ambayo wamecheza.
Simba inaongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 23, sawa na Azam, wakitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, nafasi ya tatu ikishikiliwa na Yanga yenye pointi 21.
Ligi hiyo inakwenda mapumziko kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inayotarajiwa kuanza kesho Kenya.
Wakati timu zikienda mapumziko hayo ya zaidi ya wiki mbili, ikumbukwe hiki ni kipindi cha dirisha dogo la usajili, hivyo viongozi wa timu hizo watakuwa na kazi ya kusajili wachezaji muhimu waliopendekezwa na makocha ili kuviongezea kasi vikosi vyao.
MTANZANIA linakuletea orodha ya wachezaji waliosajiliwa katika kipindi cha dirisha kubwa la usajili Juni, mwaka huu, ambao baada ya kutua kwenye timu zao wamefanya vizuri, ikiwa ni pamoja na kuzisaidia timu zao.
Razack Abarola-Azam FC
Azam FC ilimsajili Abarola kutoka katika klabu ya WAFA ya Ghana, ili kuziba pengo la Aishi Manula, aliyetimkia Simba, baada ya mkataba wake na timu hiyo kumalizika.
Baada ya kutua Azam, Abarola amejihakikishia namba ya kudumu kikosi cha kwanza mbele ya Mwadini Ally na Benedict Haule na kuwa mchezaji tegemeo kwenye timu hiyo ambayo inashika nafasi ya pili nyuma ya Simba.
Abarola amefanikiwa kuanza katika michezo yote ya Azam tangu msimu ulipoanza, akiifanya timu hiyo kuruhusu mabao machache zaidi, ikiwa imefungwa mabao matatu katika michezo 11 ya ligi hiyo hadi sasa, huku ikiweka rekodi ya kucheza michezo minane bila kuruhusu bao.
Emmanuel Okwi-Simba
Simba ilimsajili Okwi katika kipindi cha dirisha la Juni akitokea klabu ya Sports Club Villa inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uganda, huku akisaini mkataba wa miaka miwili wa kiutumikia timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.
Si mara ya kwanza Okwi kujiunga Simba, aliwahi kuichezea kwa mafanikio miaka michache iliyopita kabla ya kwenda Yanga, kisha kurudi tena Simba ambapo ilimuuza kwenda Denmark.
Okwi amerejea Simba kwa kishindo msimu huu baada ya kuisaidia timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kuifungia mabao manane kati ya 23 waliyofungwa na kikosi hicho.
Mshambuliaji huyo ndiye kinara wa ufungaji wa mabao kwenye msimamo wa ligi hiyo, kwa mabao hayo manane, mabao hayo yamechangia Simba kuvuna pointi 23.
Ibrahim Ajib-Yanga
Ajib alijiunga na Yanga Juni, mwaka huu, kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea kwa watani zao, Simba. Yanga ilimsajili Ajib ili kuziba pengo la Haruna Niyonzima aliyetimkia Msimbazi.
Baada ya kutua Jangwani, Ajib amefanikiwa kujihakikishia namba ya kudumu kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Mzambia George Lwandamina.
Ajib amefanikiwa kuifungia Yanga mabao matano ambayo yameisaidia timu hiyo kuvuna pointi tisa kati ya 21 ilizokusanya hadi sasa baada ya kushuka dimbani mara 11.
Asante Kwasi-Lipuli
Beki huyo wa kimataifa wa Ghana alijiunga na Lipuli Juni, mwaka huu akitokea Mbao FC ya Mwanza.
Tangu ajiunge na Lipuli, Kwasi ameibuka kuwa nguzo muhimu ya timu hiyo ambapo ameingia moja kwa moja kwenye kikosi hicho akitengeneza ukuta imara sambamba na Joseph Owino.
Kwasi ndiye kinara wa ufungaji ndani ya kikosi hicho, akiwa amepachika mabao manne na kuchangia kikosi chake kuvuna pointi 14 na kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Erasto Nyoni-Simba
Simba ilimsajili beki huyo baada ya kumaliza mkataba wake na Azam, huku akiwa hana nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha Wanalambalamba hao.
Baada ya kutua Msimbazi, beki huyo mkongwe amefanikiwa kuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Joseph Omog, akitumikia upande wa kulia au kushoto.
Hadi sasa Nyoni ameichezea timu hiyo karibia michezo yote, huku akifunga bao moja na kutoa pasi nane za mabao zilizochangia timu hiyo kuvuna pointi 23 na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.