29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

SHOLO MWAMBA AJIFUNZE VIZURI HISTORIA YA BONGO FLEVA

Na RAMADHANI MASENGA

MIAKA ya tisini Bongo Flavour uliokuwa ukionekana kama muziki wa kihuni. Wazazi waliogopa watoto wao kuingia katika muziki huu. Wasomi walikwepa kujihusisha na muziki huu. Kwa maana ulionekana kama muziki wa vijana waasi wa maadili.

Ila wakina Afande Sele na  wenzao hawakuacha muziki huu. Waliendelea kujituma wakiwa na lengo la kupindua mawazo ya wote waliokuwa wakiona muziki huu kama uhuni. Ila kazi haikuwa ndogo.

Mwanzoni wa miaka ya 2000,angalau jamii ikaanza kuona kuwa muziki huu sio uhuni. Walianza kuamini kuwa labda kulikuwa na wahuni wachache wakifanya muziki ila muziki wenyewe haukuwa wakihuni.

Ubunifu, mabadiliko katika muziki huo na hata mavazi yakachochea kufuta imani ya watu waliokuwa wakiamini kuwa muziki huo ni uhuni. Leo tunavyoongea tuna wabunge waliotokana na muziki huu. Leo tunavyoongea tuna matajiri katika Bongo Flavour. Ni mapinduzi makubwa.

Wakati muziki wa singeli ukichomoza, wengi waliamini ungeleta mapindizi makubwa hata kutishia uhai wa Bongo Flavour. Imani hiyo ilitokana na muziki huo kuonekana wa kitanzania zaidi huku Bongo flavour ukionekana umekuwa  muziki wa kimarekani na kinaijeria. Binafsi niliona kulikuwa na kazi ngumu mno kuifanya singeli kuwa muziki mkubwa.

Niliamini hivyo kutokana na wanamuziki wenyewe wengi wasingeli kubaki kuona muziki wao ni wa watu wachache wahuni na wakorofi. Sikiliza aina nyimbo nyingi za singeli utalewa ninachomanisha.

Waimbaji wanawaita mashabiki wao wahuni, mambo ya sirini wao hupenda kuyafanya hadharani. Katika namna hii kwa dhati kabisa niliona kulikuwa na mlima mkubwa sana wa kuupanda hata kuifanya singeli kuwa muziki wenye kukubalika na watanzania wengi.

Jumamosi iliyopita kulikuwa na tamaha la Fiesta. Miongoni mwa wahudhuriaji nami pia nilikuwamo. Leo sitoongelea mengine, nataka kuzungumizia shoo ya Sholo Mwamba na hatima ya muziki wa singeli.

Ni ukweli uliyo bayana kwamba Sholo Mwamba kwa sasa ni miongoni mwa wasanii watano wa singeli wenye kufanya vizuri katika uga wa muziki huo. Kwa maana hiyo, kupima singeli kwa namna fulani kwa kumuongelea Sholo Mwamba inaswihi.

Katika shoo ya fiesta Sholo Mwamba aliuvua nguo muziki wa singeli na kuuacha mtupu. Mbali na kuongea maneno mengi ya hovyo, ila pia hata namna alivyokuwa akihamasisha mashabiki wa muziki huo, ilikuwa ni fedhesha tu. Akiwa jukwani, alihamasisha urushaji wa vumbi, ukorofi na uhuni mwingine. Katika namna hiyo, mstarabu gani ataenda katika shoo ya Sholo Mwamba wakati mwingine?

Bongo flavour iliwahi kuitwa ya kihuni na kufanya wanamuziki wake wa mwanzo washindwe kupata mafanikio kwa sababu ya aina ya mashairi yao, mavazi na hamasa zao wakiwa jukwaani. Ila baadaye wakajibadili na kuamua kufanya muziki wenye malengo na akili. Leo tunaona Bongo Flavour ilivyopenya katika nafsi za watanzania na hatimaye kuingia katika soko la muziki wa kimataifa.

Singeli bado. Bado kwa sababu wanamuziki wake wengi hawaonekani kujielewa na kuwa na dhamira ya kuupeleka muziki huo mbele. Kama ipo siku muziki wa singeli utafanya vizuri zaidi hata kwenda kimataifa, basi ni baada ya kizazi hiki cha kina Sholo Mwamba kwisha.

Wanamuziki wa singeli wame ‘ubrand’ muziki wao kama muziki wa kihuni. Bongo flavour wameufanya muziki wao uwe biashara na elimu. Hapa kuna kichuguu na Mlima. Sholo Mwamba na wenzake inabidi kuelewa kuwa ili muziki ukubalike katika jamii inabidi wao wasanii waanze kuufanya muziki huo uwe wa kijamii zaidi na sio wa kikundi fulani cha wahuni ama cha vijana wanaosumbuliwa na ukuaji (balehe). Wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles