30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI WAANDAMANA KWA KUKOSA CHAKULA, MASOMO

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Kibara, iliyoko Kata ya Kibara, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, wameandamana baada ya kukosa chakula na masomo.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya walimu wa shule hiyo waliozungumza na MTANZANIA kwa simu jana, zilisema wanafunzi hao waliandamana jana saa nne asubuhi baada ya malalamiko yao kutosikilizwa kwa muda mrefu.

Walimu hao waliotaka majina yao yasitajwe walisema, wanafunzi hao wamekuwa wakikosa chakula na masomo mara kwa mara kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa shule hiyo uliosababishwa na kutolipwa mishahara yao tangu Januari mwaka huu.

“Ni kweli, wanafunzi wetu zaidi ya 200 wa kidato cha kwanza hadi cha sita, waliandamana leo (jana), asubuhi na kuelekea katika Kituo cha Polisi Kibara kupeleka malalamiko yao.

“Baada ya kufika kituoni hapo, polisi waliona mambo hayo yako juu ya uwezo wao, hivyo wakapiga simu wilayani ambapo Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Rydia Bupilipili, alikuja na timu yake shuleni hapa kwa ajili ya kujua tatizo.

“Mkuu wa wilaya alipofika, tulikuwa na kikao naye na mambo mengi yalizungumzwa na hatimaye alipewa namba ya simu ya mkurugenzi ili amtafute mwenyewe.

“Lakini mwishowe mhasibu wa shule aitwaye Nyamweko Mganywa, alichukuliwa na kupelekwa polisi kwa mahojiano zaidi.

“Kwa kifupi, hali siyo nzuri shuleni hapa kwa sababu hata mkurugenzi wetu akipelekewa malalamiko, huwa hatoi ushirikiano wowote,” walisema walimu hao kwa nyakati tofauti.

Mhasibu Nyamweko alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, simu yake ilipokelewa na mwalimu ambaye alisema mfanyakazi mwenzake huyo amepelekwa polisi.

“Mimi siyo Nyamweko bali ni mwalimu. Nyamweko yuko polisi kuna mambo fulani fulani anayafuatilia,” alisema mwalimu huyo huku akikataa kuzungumza kwa undani kwa kile alichosema yeye siyo msemaji wa shule hiyo.

Mmoja wa wakurugenzi wa shule hiyo, Mutamwega Muganywa, alipozungumza na MTANZANIA kwa simu, alikiri kupata taarifa za malalamiko hayo, lakini akasema yeye siyo mmiliki wa shule ingawa ni mmoja wa waanzilishi wa taasisi ya TASECE inayomiliki shule hiyo.

“Hizo taarifa nimezipata ila mimi siyo mmiliki wa shule bali ni mshauri na mwanzilishi wa taasisi inayoimiliki.

“Kwa hiyo, sihusiki kabisa, sijawahi kufika shuleni hapo na ukitaka mtafute meneja atakwambia kinachoendelea,” alisema Mutamwega.

Mkuu wa wilaya alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakuujibu hadi tunakwenda mitamboni.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mara, Jafary Mohamed, alipozungumza na MTANZANIA kwa simu, alisema hana taarifa za wanafunzi hao kuandamana hadi Kituo cha Polisi Kibara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles