25 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

HATIMILIKI ZA KIMILA KUTODAIWA KODI YA PANGO LA ARDHI

Na CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAM

SERIKALI kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kutekeleza Programu ya Kuwezesha Umilikishaji Ardhi (Land Tenure Support Programme – LTSP) katika Wilaya 3 za Kilombero, Ulanga na Malinyi.

Jumla ya vijiji 160 vitanufaika na utekelezaji wa Programu hii. Programu hii inafadhiliwa na Serikali za Uingereza kupitia UK Aid, Denmark kupitia Shirika la Maendeleo la DANIDA na Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la SIDA.

Utekelezaji wa Programu ya LTSP ni miongoni mwa jitihada za Serikali katika kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi kinapimwa na kumilikishwa kisheria. Katika zoezo linaloendelea Kilombero Zoezi la utambuzi ardhi Hati 2,111  zatolewa Kilombero

Katika utekelezaji wa Programu ya LTSP, Serikali imejikita katika masuala ya kupima mipaka ya vijiji, kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji; kuhakiki na kupima vipande vya ardhi katika maeneo ya makazi na mashamba pia kutoa Hati kwa kuzingatia makundi maalumu (wanawake, watu wenye ulemavu, wafugaji wa asili, wazee na vijana).

Pia kubaini mbinu na teknolojia sahihi itakayotumika kurasimisha ardhi na kutoa Hati za Hakimiliki za kimila katika eneo la Programu ili mbinu na teknolojia hiyo itumike kurasimisha ardhi katika maeneo mengine ya nchi.

Kuimarisha mfumo wa kisera, kisheria na kitaasisi unaolenga kuleta ufanisi kwa kupunguza gharama za kutoa hati, kujenga uwezo wa wataalam kuanzia ngazi za kijiji hadi taifa pamoja na kujenga masijala za ardhi za vijiji na Ofisi za Ardhi za Wilaya.

Mratibu wa Mradi, Godfrey Machabe anasema; mafanikio yamekuwa yakionekana tangu walipoanza utekelezaji wa programu Julai, mwaka jana.

Anasema utekelezaji wa programu unaendelea vizuri ambapo mipango ya matumizi ya ardhi ya wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi imeandaliwa na kukabidhiwa kwa Halmashauri kwa hatua za utekelezaji.

“Jumla ya alama za msingi za upimaji  54 zimesimikwa katika eneo la Programu, mipaka ya vijiji 50 imepimwa, vyeti vya Ardhi ya Kijiji 57 vimeandaliwa, vijiji 30 vimeandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji,”anasema Machabe.

Anasema pia vipande vya ardhi 22,324 vimehakikiwa na kupimwa kwa ajili ya kuandaa Hati za Hakimiliki ya Kimila (CCROs).

Anaongeza kuwa hati za Hakimiliki ya Kimila 9,112 zimeandaliwa na Ujenzi pia ukarabati wa masjala za ardhi na ofisi za vijiji upo katika hatua mbalimbali katika vijiji 61.

Machabe anasema changamoto za Mradi; zinazoikabili programu katika utekelezaji wake ni pamoja na idadi kubwa ya migogoro ya ardhi katika eneo la programu na hivyo kuchelewesha kasi ya urasimishaji wa ardhi.

Anasema hata hivyo programu inafanya tafiti kuhusu migogoro ya ardhi iliyopo ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kutatua migogoro hiyo ili kuharakisha kasi ya utekelezaji wa Programu.

“Kiwango kikubwa cha mvua zinazonyesha katika eneo la Programu hususan kipindi cha masika, hivyo kuathiri utekelezaji wa baadhi ya kazi za uwandani (site) kwa wakati. Ili kukabiliana na changamoto hii, tumejipanga kutekeleza kazi nyingi za uwandani wakati wa kiangazi,”anasema Machabe.

Anasema Machabe changamoto nyingine ni upungufu wa wataalam katika ngazi ya Halmashauri hususan Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi.

Anasema hali hiyo imesababisha kuchelewa kuanza kwa baadhi ya kazi za Programu katika Wilaya hiyo.

“Ili kukabiliana na changamoto hii, mawasiliano yamefanyika kati ya Wizara na Ofisi ya Mkoa wa Morogoro ili Halmashauri ya Malinyi iweze kupatiwa wataalam kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa Programu,”anasema Machabe.

Anasisitiza Machabe kuwa katika kuhakikisha programu inatekelezwa kwa ufanisi, mikakati imewekwa kuongeza kasi ya utekelezaji kwa kuongeza idadi ya timu kwa ajili ya kuharakisha zoezi la kuhakiki na kupima  vipande vya ardhi na kuandaa Hati za Hakimiliki ya Kimila (CCROs); Kuimarisha mfumo (automation) utakaolenga kupunguza gharama na kuongeza kasi ya uandaaji wa hati.

Pia kuimarisha ofisi za Programu uwandani ambapo ramani kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Ardhi za Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi zimeandaliwa na hatua za kumpata mkandarasi wa kujenga ofisi hizo zinaendelea.

Anasema pia wamejipanga kutoa elimu na uhamasishaji kwa wanavijiji ikiwemo makundi maalum (wanawake, wafugaji wa asili, watu wenye ulemavu, wazee na vijana) kuhusiana na Sera na Sheria zinazohusu utawala wa ardhi.

“Mikakati mingine ni kufanya tathmini ya idadi na aina ya migogoro ya ardhi katika eneo la Programu pamoja na kuweka mbinu za kusuluhisha migogoro hiyo kwa haraka ili kuepusha kukwama kwa mazoezi ya urasimishaji”, anasena Machabe.

Anaongeza kuwa hilo linawezekana kwa kutumia rasilimali watu kutoka katika eneo la Programu na Vyuo vya Ardhi vilivyopo chini ya usimamizi wa Wizara kutumia teknolojia rahisi ya upatikanaji wa picha za anga kwa ajili ya utambuzi wa mipaka inayohusiana na vipande vya ardhi na kuongeza idadi ya vitendea kazi hususan magari na pikipiki ili kurahisisha na kuongeza kasi ya utekelezaji wa kazi za uwandani.

Anasema programu hiyo ya kuwezesha umilikishaji Ardhi, ni ya miaka mitatu ambapo utekelezaji wake ulianza Julai, mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Juni, 2019.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,William Lukuvi amewataka wananchi wa Nyange na wengine wenye Hati za Hatimiliki za Kimila wachangamkie fursa ya kutumia Hati hizo kukopa benki ili kujipatia Maendeleo mbalimbali.

Anasema kuhusu suala la kuwezesha Utekelezaji, amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe kuwezesha utoaji wa  wataalamu zaidi kutoka kwenye Halmashauri za Wilaya kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa kazi za urasimishaji wa ardhi katika maeneo ya programu.

Lukuvi anasema wataalam hao watawezesha programu kuwa endelevu hata mradi utakapofikia ukomo wake.

Naye,Kebwe anawataka wanavijiji kushiriki kikamilifu katika mazoezi ya urasimishaji wa programu, hususan Maandalizi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kijiji; ujenzi wa masjala za ardhi za vijji; na uhakiki na upimaji wa vitalu vya ardhi.

Faida za urasimishaji wa ardhi

Ni kupunguzamigogoro ya ardhi kwani kila kipande cha ardhi kitakuwa kimeanishwa na kuwa na mwenyewe na hivyo mahusiano yatakuwa ya kisheria zaidi  badala ya uzoefu na historia.

Ardhi iliyorsimishwa hupewa hati amabayo inaweza kutumika katka shuguli za kiserikali na mabenki kama djhamana ya mikopo au  mahakamani. Hivi basi hali  ya uchumi wa ardhi hiyo huongezeka thamani na inakuwa rahisi kuhamishika katika misingi mingine ya kisheria.

Mpango mzima wa urasimishaji umezingatia haki  za watu wote bila kujali jinsia au ulemavu wa mhusika na hivyo hutoa fursa sawa kwa wote katika jamii kwa kuweza kumiliki mali ambayo ni msingi wa uzalishaji katika jamiii.

Ardhi iliyorasimishwa huwa rahisi kutumika kwa uwekezaji kwani kila upande hujua misingi ya mahusiano hayo na nirahisi kuaminika katika uwekezaji huo kwani mradi hujidhamini wenyewe.

Hali inaonesha kuwa baada ya kukamilika zoezi la urasimishaji uchumi wa watu katika jamii za wilaya hizi tatu zitafaidika na zoezi hilo kwa kufanya mengi ambayo yasingewezekana bila mradi huo. Inawezekana ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles