32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAJANGA 11 YA MANJI

Na MWANDISHI WETU


KATIKA kipindi cha takribani mwaka mmoja na miezi minane baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, huenda mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, akawa mtu pekee maarufu anayeongoza kwa mikasa kwa sasa.

Manji ambaye anasota mahabusu kwa takribani siku 58 sasa, akisubiri upelelezi ukamilike kutokana na tuhuma zinazomkabili za uhujumu uchumi na sheria ya usalama wa taifa, baada ya kudaiwa kukutwa na sare na mihuri miwili ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amejikuta kwenye mfululizo wa majanga mbalimbali yanayofikia takribani 11.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba katika kipindi hicho cha zaidi ya mwaka mmoja, miongoni mwa majanga ambayo amekumbana nayo, yapo ambayo yamezaa kesi zinazomkabili mahakamani.

Upekuzi uliofanywa na MTANZANIA Jumapili, umebaini kuwa majanga tisa kati ya 11 yanayomkabili, yalimkumba kabla ya kesi ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa yenye mashtaka saba kufunguliwa Julai 5, mwaka huu, ambayo inamkabili na wenzake watatu.

Ukiachilia mbali kesi hiyo, majanga mengine yaliyomkumba Manji tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, ni uendelezaji wa Coco Beach, tuhuma za matumizi ya dawa za kulevya, umiliki wa hisa za Kampuni ya Tigo, sakata la jengo la Quality Plaza, Kiwanda cha Ngozi cha Mwanza Tanneries  na kusudio la kufutwa kwa leseni ya kampuni yake ya simu ya Mycell.

Mengine ni sakata la kiwanja cha Kigamboni, kuikodi timu ya Yanga, uhamiaji na tishio la kuvuliwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 

COCO BEACH

Sakata la Coco Beach licha ya kuanza kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, ndilo linaloonekana kuwa tukio la mwanzo kuanza kumtikisa Manji.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Manispaa ya Kinondoni ilitangaza zabuni ya kuendeleza ufukwe huo na Kampuni ya Q-Consult inayomilikiwa na Manji ilishinda.

Lakini manispaa hiyo ilivunja mkataba na kampuni hiyo kwa kile kilichodaiwa kuwa ilishindwa kutimiza masharti iliyowekewa.

Uamuzi huo uliifanya Q-Consult kufungua kesi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi mwaka 2009 na baada ya miaka sita, uamuzi ulitolewa kwa manispaa kutakiwa kutekeleza ahadi ya mkataba wake na kampuni hiyo.

Wakati sakata hilo likiendelea, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, Desemba 3, 2015, Rais Dk. John Magufuli alitangaza kusudio la Serikali yake kufanya eneo hilo kubaki kwa matumizi ya wananchi kama ambavyo linatumika hivi sasa.

Ni agizo hilo la Serikali ndilo lililomfanya Manji siku mbili baadaye kumwandikia barua Rais Magufuli, kumwelezea mchakato wa zabuni na alivyoshinda kihalali kuendeleza ufukwe huo.

Juni 23, mwaka huu, bila kueleza kilichomsukuma, Manji alitangaza kuachia kwa hiari yake uendelezaji wa eneo hilo na zaidi akiomba radhi.

“Ninaomba radhi binafsi kwa Rais Dk. John Magufuli, Serikali na wadau wote ambao tuliwakwaza kwa sintofahamu yoyote iliyojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa jambo hili.

“Tumewaagiza mawakili wetu wawasilishe taarifa rasmi, kwamba tunajitoa kama wapinzani katika rufaa iliyowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pia hatutadai gharama zozote zilizoingiwa au hasara ya mapato tuliyoipata kwa vile masilahi yetu ya kifedha ni pungufu na si halali ukilinganisha na manufaa ya jamii,” lilisomeka tangazo la Manji.

 

QUALITY PLAZA

Kampuni zake tano kuondolewa ndani ya Jengo la Quality Plaza linalomilikiwa na Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), ni miongoni mwa mambo ambayo yanaingia katika orodha ya matukio yaliyomkumba Manji.

Kampuni hizo ziliondolewa ndani ya jengo hilo baada ya kutimia saa 24 alizopewa na PSPF, Desemba 2, mwaka jana.

Inadaiwa kampuni hizo tano za mfanyabiashara huyo, zilipangisha ndani ya jengo hilo ambalo lipo Kitalu Na. 189/2, mkabala na Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.

Sababu kuu ya kampuni hizo kuondolewa ndani ya jengo hilo, ni deni la kodi ya pango ambalo lilidaiwa kufikia Sh bilioni 13.

Makampuni yaliyoondolewa ni Quality Group Company Limited, Gaming Management Limited, Q-Consult Limited, Quality Logistics Company Limited na International Transit Investment Limited.

 

DAWA ZA KULEVYA

Sakata jingine kwa Manji ni tuhuma za kutumia dawa za kulevya zinazomkabili mahakamani, na wiki iliyopita mahakama ilimwona ana kesi ya kujibu.

Msingi wa kesi hiyo ni Februari 8, mwaka jana baada ya jina lake kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika orodha ya watu 67 waliodaiwa kujihusisha na matumizi au biashara ya dawa za kulevya.

Manji aliingizwa katika orodha hiyo na watu wengine maarufu wakiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Askofu Josephat Gwajima na Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan ambao wote hao wamefanikiwa kukwepa kesi hiyo.

TISHIO LA KUFUKUZWA CCM

Siku chache baada ya Manji kutajwa katika orodha hiyo, kuliibuka taarifa zinazodai kuwa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umenuia kumfukuza uanachama.

Baada ya taarifa hizo kuibua mjadala mkubwa katika jamii, Februari 20, mwaka jana, uongozi wa CCM Wilaya ya Temeke, uliibuka na kusema kuwa hautamjadili Manji ambaye ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, hadi kesi yake kuhusu madai ya kutumia dawa za kulevya itakapomalizika mahakamani.

 

UHAMIAJI

Hatua ya Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, kuwakamata wafanyakazi wa kigeni 25 wa Kampuni ya Quality Group ambayo inadaiwa kumilikiwa na Manji, Februari 15, mwaka huu, nayo ilitoa taswira ile ile ya mfanyabiashara huyo kukumbana na vihunzi vingi ambavyo hatima yake ni mapema kutabiri.

Wafanyakazi hao walikutwa hawana vibali vya kufanya kazi nchini, hivyo Uhamiaji ilimtaka Manji ambaye ndiye mwajiri mkuu na mmiliki wa kampuni hiyo, kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuajiri wafanyakazi wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.

 

HISA ZA TIGO

Manji kupitia Kampuni yake ya Golden Globe kuwa na umiliki wa asilimia 99 za hisa za Kampuni ya simu ya Tigo, ni miongoni mwa mambo ambayo yamejulikana hivi karibuni baada ya habari hiyo kuchapishwa na gazeti moja la kila siku la Kiingereza hapa nchini.

Ukweli wa jambo hilo bado unakanganya na kuna kesi mahakamani.

Inaelezwa ni mkanganyiko huo ndio ulioilazimisha Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kusimamisha mchakato wa kuingiza hisa za Tigo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Kampuni ya Golden Globe inadaiwa  kuinunua Tigo Novemba 5, mwaka 2014 katika mnada uliofanywa na mahakama baada ya mdai mmoja aliyeishtaki kampuni hiyo ya mawasiliano kushinda kesi.

Kwa sasa Golden Globe ambayo inadaiwa kumilikiwa na Manji, inaelezwa kuwa na umiliki wa hisa 34,479 kati ya 34,480 za Tigo. Hisa moja iliyobaki inamilikiwa na Kampuni ya Shai Holdings.

Hata hivyo, Kampuni ya Milcomn Tanzania NV inayoelezwa kuimiliki Tigo, imefungua kesi mahakamani ikihoji utaratibu uliotumika kuinunua kampuni hiyo.
Pia taarifa iliyotolewa na Tigo mapema mwaka huu, ilitoa ufafanuzi kwamba bado ipo chini ya umiliki wa Milcomn.

 

KIWANDA CHA MWANZA TANNERIES

Hatua ya Serikali kutangaza kukifungia Kiwanda cha ngozi cha Mwanza Tanneries kinachodaiwa kumilikiwa na moja ya kampuni za Manji, Agosti 10, mwaka huu, ilionekana kama pigo jingine kwa mfanyabiashara huyo.

Serikali ilifikia uamuzi huo wakati Manji akiwa tayari ameanza kusota mahabusu, baada ya kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Agizo la kufungwa kwa kiwanda hicho lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, baada ya siku 10 alizozitoa kwa wamiliki wake kuondoa vyuma chakavu kiwandani hapo kupita bila kufanyiwa kazi.
Inaelezwa kuwa kiwanda hicho awali kilikuwa kikimilikiwa na Kampuni ya Afrika Tanneries kisha kubadilishwa umiliki kwenda kwa Kampuni ya Kasco ambayo yenyewe inadaiwa imehamishia umiliki wake kwa Kampuni ya Quality Group inayotajwa kumilikiwa na Manji, iliyoshindwa kukiendeleza.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema Quality Group inadai kiwanda hicho ni mali yao na kampuni ya Kasco inadai kuwa ndio wamiliki halali, kitendo ambacho kimesababisha mgogoro wa muda mrefu na hivyo Serikali kuamua kukifunga hadi pale mwafaka utakapopatikana.

 

KAMPUNI YA MYCELL

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutangaza kusudio la kufuta leseni ya Kampuni Mycell inayomilikiwa na Quality Group Limited (QGL), ni uamuzi mwigine wa hivi karibuni ambao nao umejenga taswira ya Manji kuandamwa na mapigo.
Uamuzi huo wa TCRA wa Agosti 18, mwaka huu, unatokana na sheria ya mamlaka hiyo ya mwaka 2003 ambayo ina jukumu la kusimamia, kutoa na kufuta leseni za mawasiliano kwa kampuni yoyote ambayo imeshindwa kutekeleza majukumu iliyoyabainisha.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TCRA, Januari 27, mwaka jana ilitoa amri kwa kampuni hiyo kutekeleza majukumu yake baada ya kubainika kukiuka masharti ya leseni walizopewa na kushindwa kutoa huduma kinyume cha kifungu 21 (a) na (b) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca) ya mwaka 2010.

 

KIWANJA CHA KIGAMBONI

Kitendo cha Manji mwenyewe Septemba 28 mwaka jana kuipa Klabu ya Yanga – akiwa mwenyekiti wake, eneo la ukubwa wa ekari 715 lililopo kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi, Geza Ulole, Kigamboni, Dar es Salaam ili kujenga uwanja na kisha kuzuiwa na Kampuni ya Lake Oil Limited iliyodai kuwa ni lake, ni miongoni mwa mambo ambayo watu wanaomfuatulia mfanyabiashara huyo wanasema huwezi kukiacha katika orodha ya mitihani inayomwandama.

Kampuni ya Lake Oil ilidai kuuziwa eneo hilo na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO).

 

KUKODISHA KLABU YA YANGA

Watu wanaofuatilia michezo, wanasema huwezi ukazungumzia vihunzi vinavyomkabili Manji kwa sasa ukaliacha sakata la Agosti 6, mwaka jana, alipowaomba wanachama wa Klabu ya Yanga wamkodishie timu hiyo aingoze kwa miaka 10.

Manji alitoa ombi hilo ikiwa ni miezi michache imepita tangu achaguliwe kwa mara nyingine kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo.

Kumbumbuku zinaonyesha kuwa aliomba apewe asilimia 75 ya hisa za kuendesha klabu hiyo huku akiwaachia wanachama asilimia 25.

Hata hivyo, ombi lake liligonga mwamba baada ya wazee wa klabu hiyo wakiongozwa na Ibrahim Akilimali kuibuka na kupinga mchakato huo.

Sakata hilo la kupinga maombi ya Manji liliibua mvutano ndani ya klabu hiyo baada ya wanachama kugawanyika makundi mawili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles