26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

GWIJI WA HABARI MUHINGO RWEYEMAMU AFARIKI DUNIA

Na Waandishi Wetu – dar es salaam


TASNIA ya habari imekumbwa na majonzi baada ya kuondokewa na gwiji wake wa muda mrefu, Muhingo Rweyemamu.

Muhingo alifariki dunia saa tatu asubuhi jana katika Hospitali ya Aga Khan ya Dar es Salaam alikokuwa anatibiwa.

Enzi za uhai wake akiitumikia tasnia ya uandishi wa habari, Muhingo alitambulika vyema kama mwalimu mbobezi na kiongozi mahiri katika masuala ya habari kwa waandishi wengi ambao wanaendelea kuitumikia tasnia hiyo, pia ni mmoja wa waanzilishi wa gazeti la Mwananchi.

Umahiri wake ndani ya tasnia ya habari ulijitanua na kufahamika vyema kuanzia mwaka 1993 alipoanza kuripoti kwenye magazeti ya Mwananchi na The Express.

Mazingira ya kubobea zaidi kiuandishi yalimpandisha hadhi mwaka 1995 na kuwa mwandishi mwandamizi, Mhariri wa Makala, Mhariri na Mkuu wa Kitengo cha Picha katika Gazeti la Mtanzania.

Ndani ya utumishi wake katika ngazi ya uhariri, Muhingo, alitumikia magazeti mbalimbali hapa nchini na baadaye kuwa  Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.

Mbali na ubobezi wake katika tasnia hiyo, pia Muhingo amepata kutumikia nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga na anakumbukwa zaidi baada ya kuanzisha kampeni ya “niache nisome” ambayo wanafunzi wengi wa kike walioachishwa shule na wazazi wao na kwenda kuozeshwa walirudishwa shuleni kuendelea na masomo yao alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Makete (Njombe) na baadaye Morogoro Mjini.

Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa familia na kaka wa marehemu, Elisa Muhingo, alisema Muhingo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Myelofibrosis ambao hudhoofisha uwezo wa kinga za mwili kutengeneza damu.

“Kwa kipindi kirefu takribani miaka 11 iliyopita, Muhingo alikuwa anaumwa na kuwekewa damu mara kwa mara na mwaka jana ndipo alizidiwa na tulimpeleka katika vituo vya afya zikiwemo hospitali kubwa kwa matibabu,” alisema.

Elisa alisema baadhi ya hospitali alizowahi kutibiwa ni pamoja na Muhimbili, India na Agha Khan na kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wanampatia matibabu, maradhi hayo hayana tiba.

Pia alisema familia bado inaendelea na taratibu za mazishi kwa kufanya vikao vya wanandugu wa karibu ili kupanga mahali pa kuzika na siku rasmi ya kuaga mwili wake.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited, Absalom Kibanda, alisema tasnia ya habari nchini imepoteza silaha kubwa kwa sababu Muhingo alikuwa na uwezo mkubwa katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

“Ni siku ya huzuni na maombolezo, tumepoteza mmoja wa wanahabari mwenye maarifa mengi na kiwango chake si cha kutilia shaka, ameacha urithi mkubwa kwa sababu mimi mwenyewe ni zao lake.

“Muhingo alikuwa mfuatiliaji mzuri wa matukio makubwa ya kihabari yaliyopata kutikisa taifa kama vile kifo cha Kardinali Rugambwa na kile cha Mwalimu Nyerere.

“Alikuwa mmoja wa waandishi na wahariri wenye vipaji vingi adhimu na adimu, mwalimu mzuri, msikivu, mbunifu na mahiri kwa lugha za simulizi za matukio ya mikasa.

“Nikisema kuwataja wahariri wangu watano Muhingo lazima atakuwapo kwa sababu ndiye aliyetambua kipaji changu kuwa kimepevuka, hivyo hatuna budi kuendeleza kazi zake pamoja na maarifa aliyotuachia,” alisema.

Kibanda alisema Muhingo alikuwa na uwezo mzuri wa kuandika makala mbalimbali na ulipotokea msiba wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliandika makala akasema: “Mwalimu hawezi kufa, lakini wa kuvaa viatu vyake bado ni kazi kubwa.”

Kibanda alisema nje ya taaluma ya uandishi wa habari, Muhingo aliwahi kuwa mwanasiasa aliyeshirikiana na wanasiasa wakubwa na wachanga.

Naye mwandishi wa habari mkongwe, Nyaronyo Kicheere, alimwelezea Muhingo tangu walivyofahamiana kuanzia miaka 1980 wakati walipokuwa walimu wa shule za msingi hadi walipokuwa waandishi wa habari.

“Magazeti binafsi yalipoanzishwa alienda Mtanzania, kutoka magazetini tukaenda vyuoni, yeye Tumaini, mimi Mlimani, yeye anasoma uandishi, mimi sheria, kutoka vyuoni tukakutana Mwananchi,” alisema Nyaronyo.

 

WASIFU

Mwaka 2004 Muhingo alihitimu masomo ya Shahada ya Kwanza ya Uandishi wa Habari (BAJ) katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa.

Mwaka 1993 alihitimu Stashahada ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha TSJ.

Mwaka 1989 alihitimu Stashahada ya Elimu katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dar es Salaam.

Mwaka 1983 alihitimu Astashahada ya Elimu katika Chuo cha Ualimu cha Tukuyu na mwaka 1977 alihitimu Elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Nyakato.

 

UZOEFU KAZINI

Mwaka 1984-1985 alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Igwata, Geita.

Mwaka 1985-1987 alikuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makongo, Dar es Salaam.

Mwaka 1989 alikuwa Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Morogoro.

Mwaka 1989-1992 alikuwa Katibu Uenezi Taifa wa Chama cha Wanataaluma ya Uenezi.

Mwaka 1993-1995 alikuwa mwandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi na The Express.

Mwaka 1995-1998 alikuwa Mwandishi Mwandamizi , Mhariri wa Makala, Mhariri na Mkuu wa Kitengo cha Picha katika Gazeti la Mtanzania.

Mwaka 1999 alikuwa Mhariri Mkuu wa Jarida la Wiki Hii.

Mwaka 1999-2001, alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi.

Mwaka 2003, alikuwa Mwakilishi wa Jarida la habari za mazingira la ENS la nchini Marekani.

Mwaka 2004-2005, alikuwa Mhariri Mshiriki akihusika na mambo ya kisiasa katika Gazeti la Citizen.

Mwaka 2006-2008 alikuwa Mhariri wa Gazeti la Rai.

Mwaka 2008-2010, alikuwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.

 

USHIRIKI

Alishiriki kuripoti habari zote za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995-2000. Pia mwaka 2004 alifanya utafiti wa masuala ya Ukimwi wilayani Makete.

Mwaka 1996, alishiriki kuripoti habari za vita nchini Zaire sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa upande wa Jeshi la Laurent Kabila na mwaka 1994 aliripoti kikamilifu habari za mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda.

Mwaka 2005 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu alisimamia vyombo vya habari katika kuripoti habari za mgombea urais wa CCM.

 

UONGOZI

Mwaka 2001-2002, alikuwa Spika wa Baraza la Uongozi wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini.

Mwaka 2003-2004, alikuwa Waziri wa Habari  wa Baraza la Uongozi wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini.

Mwaka 1992, alikuwa Katibu Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha TSJ.

 

MAFUNZO YA ZIADA

Mwaka 1996 alishiriki mafunzo ya umahiri wa matumizi ya kamera katika Taasisi ya Uandishi wa Habari Picha ya nchini Msumbiji.

Mwaka 1997 alishiriki mafunzo ya Uandishi wa Habari za Mazingira katika Taasisi ya Samso ya nchini Zimbabwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles