31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

JAJI ALIYEFUTA UCHAGUZI KENYA PASUA KICHWA

*Kenyatta amtisha, katiba yamnyima nguvu kumng’oa

*Aliwahi kumjibu kuwa yeye si mradi wa Serikali

 

NAIROBI, KENYA


BAADA ya Mahakama ya Juu nchini Kenya kutoa hukumu ya kihistoria katika bara la Afrika ya kufuta matokeo ya uchaguzi, yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta aliyekuwa akiwania kipindi cha pili, watu wengi wamejiuliza Jaji David Maraga ambaye aliongoza jopo la majaji sita hadi kufikia kutoa uamuzi huo, ni nani.

Baadhi ya Wakenya ambao wamekaririwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), wamemwelezea Maraga kama Jaji jasiri ambaye amethubutu kutoa hukumu dhidi ya mtu aliyemteua,  Rais Kenyatta.

Kwa sababu hiyo, Maraga kwa ujasiri wake huo, anaelezwa kurejesha imani ya uhuru wa mahakama, hasa ikizingatiwa kuwa kwa nchi za Afrika ni jambo ambalo halijawahi kuwezekana kwa upinzani kufanikiwa kushinda kesi ya kupinga uchaguzi wa rais.

Magazeti kadhaa ya nchini Kenya yamemwelezea Jaji Maraga kuwa mtu wa maadili kutokana na hatua yake ya kushika imani sana ya dhehebu lake la Sabato (Seventh Day).

Aliwahi kuripotiwa akiliambia jopo lililokuwa likimsaili aweze kushika nafasi ya Jaji Mkuu, kwamba iwapo atachaguliwa katika wadhifa huo, hatosimamia kesi siku ya Jumamosi, ambayo ni siku ya kupumzika kwa waumini  wa kanisa hilo.

Watu ambao walikuwa wakikumbuka maneno yake hayo, wamedai huenda hiyo ndiyo sababu ya siku ya kwanza ya kesi hiyo ya kupinga ushindi wa Rais Kenyatta kuanza kusikilizwa saa moja usiku Jumamosi baada ya siku ya Sabato kuisha.

Iliwahi kuripotiwa kuwa wakati akichunguzwa (vetting) kabla kupewa nafasi hiyo ya Jaji Mkuu, alikabiliwa na madai kwamba alikula hongo.

Hata hivyo, aliwashangaza wengi wakati wa hafla ya kula kiapo ambayo ilirushwa moja kwa moja na televisheni ya taifa, akiwa ameshikilia kitabu kitukufu cha Biblia na kuapa kwamba hajawahi kuchukua hongo katika maisha yake.

 

MRADI WA SERIKALI

David Kenani Maraga, mwenye umri wa miaka 66 ambaye ni mzaliwa wa Bonyamatuta katika Kaunti ya Nyamira nchini Kenya, ndiye Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Juu ya Kenya.

Alifuzu mafunzo ya uanasheria miaka 40 iliyopita kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na baadaye alipata shahada ya uzamili katika chuo hicho, kabla ya kuhudumu kama wakili wa kujitegemea.

Alichaguliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2003 na Rais mstaafu Mwai Kibaki, kisha alipanda na  kujiunga na Mahakama ya Rufaa mwaka 2012.

Mwaka mmoja baada ya kuwa jaji wa Mahakama ya Rufaa, aliwania nafasi ya urais wa mahakama hiyo, lakini alishindwa na nafasi hiyo kuchukuliwa na Jaji Kihara Kariuki.

Akiwa ameoa na baba wa watoto watatu, Mei mwaka 2012, Jaji Maraga aliteuliwa na Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga, kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kimahakama ya Maandalizi ya Uchaguzi wa Kenya (JWCEP).

Madhumuni ya kamati hiyo ilikuwa kujiandaa na migogoro yoyote au mapingamizi ya Uchaguzi Mkuu wa Machi mwaka 2013.

Mwaka 2013 Rais Kenyatta alimteua Jaji Maraga kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kimahakama ya Uchunguzi dhidi ya Jaji wa Mahakama Kuu, Joseph Mutava baada ya kuibuka malalamiko katika hukumu aliyotoa kwa Kamlesh Pattni kuhusu kashfa ya Goldenberg.

Tume hiyo ilitoa ripoti yake Septemba 2016 na kupendekeza kwa Rais Kenyatta kumwondoa Jaji Mutava kutokana na ukiukwaji wa hukumu iliyotolewa kwa Pattni licha ya Tume ya Huduma za Kimahakama kulichunguza jambo hilo.

Juni mwaka jana, baada ya Jaji Mkuu Mutunga kustaafu, Jaji Maraga akiwa na shahada ya uzamili tu aliwashinda majaji wengine 10, mawakili na wasomi waliomzidi visomo na hivyo kuteuliwa kuwa jaji mkuu.

Baadhi ya majaji ambao waliangushwa na Jaji Maraga katika kinyang’anyiro hicho ni Profesa wa sheria Makau Mutua, Jaji wa Mahakama ya Juu, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala, Jaji Aaron Ringera na Jaji Alnashir Visram

Maraga amekuwa Jaji Mkuu wa pili kuhudumu nchini Kenya tangu kuanza kutekelezwa kwa Katiba ya sasa, ambayo ilifanyia mabadiliko mfumo wa mahakama mwaka 2010.

Kama Jaji Mkuu, David Maraga anakuwa pia Rais wa Mahakama ya Juu ambayo husikiliza na kutoa uamuzi kuhusu kesi za matokeo ya uchaguzi wa urais.

 

AKATAA KUWA MRADI WA SERIKALI

Wakati sasa Jaji Maraga akitoa hukumu ya ‘kumkemea’ Rais Kenyatta mtu ambaye alimteua, kiongozi huyo alipofanya kampeni za uchaguzi ambao umefutwa nyumbani kwa jaji huyo alinukuliwa akisema kuwa wakazi wa eneo hilo wanapaswa kumpigia kura kwa sababu alimpatia kazi ‘mtoto wao’.

Hata hivyo, kauli hiyo ilionekana kupokewa vibaya na Jaji Maraga ambaye alisema yeye si mradi wa Serikali.

 

VIKAO NA ODINGA, KENYATTA

Wiki mbili baada ya kuapishwa kuwa Jaji Mkuu, Oktoba mwaka jana, Maraga alifanya mazungumzo na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga katika Mahakama ya Rufani kwa muda wa saa moja na nusu.

Mazungumzo hayo yalikuwa sehemu ya mpango wake kama rais mpya wa Mahakama ya Rufani kuzungumza na wanasiasa waandamizi. Kikao cha kwanza alifanya na Rais Uhuru Kenyatta.

Kwa mujibu wa gazeti la The Standard, katika kipindi hicho Jaji Maraga alikutana na wanasiasa wakubwa nchini humo na kuwahakikishia uwazi wa hukumu za kesi zote. Pia alisisitiza

kusimamia uwajibikaji na heshima ya Mahakama ya Rufani.

“Napenda kuwahakikishia wananchi, mahakama ipo tayari na inamudu kusikiliza mapingamizi yote yatakayotokea mwakani (uchaguzi wa mwaka 2017),” alisema Jaji Maraga alipokuwa akizungumza na Raila na wafuasi wake, ikiwa ni njia ya kujenga imani kwa mhimili huo.

Viongozi wengine walioambatana na Raila walikuwa Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula.

Kabla ya kikao hicho, Idara ya Mahakama ilikuwa na uhusiano mbaya na wanasiasa wa upinzani, hususani Raila baada ya uamuzi kuhusu uchaguzi wa urais wa mwaka 2013.

Katika uamuzi huo, Mahakama ya Juu ilithibitisha ushindi wa Kenyatta.

 

VITISHO VYA KENYATTA

Ingawa Rais Kenyatta hapo awali alisema ataheshimu uamuzi wa mahakama, hata hivyo baadae jana alikaririwa akihoji ni kwa nini watu sita wanaweza kutoa uamuzi unaokwenda kinyume na matakwa ya Wakenya wanaofikia milioni 40.

Kenyatta alikwenda mbali na hata kufikia kusema majaji hao walikuwa wamelipwa na “watu wa kigeni pamoja na wajinga wengine”.

Alisema kuwa awali alikuwa rais mtarajiwa, lakini sasa ni rais aliyekalia kiti,

“Maraga na wahahalifu wake wameamua kubatilisha uchaguzi. Sasa mimi sio tena rais mteuliwa bali rais aliye mamlakani. Maraga anapaswa kujua kwamba sasa mimi ni rais ninayehudumu… ajue kwamba sasa ana-deal na rais ambaye amekalia kiti,” alisema Kenyatta na kutamba kuwa wako tayari kwa raundi ya pili.

Licha ya vitisho hivyo vya Kenyatta, kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, rais hana uwezo wa kumfuta kazi Jaji Mkuu ambaye muhula wake mmoja unakamilika wakati atakapofikisha miaka 70.

 

JOPO LA MAJAJI SITA

Jopo la majaji lililoongozwa na  Jaji Maraga kutoa uamuzi wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 8, mwaka huu na kuamuru uchaguzi wa marudio ufanyike ndani ya siku 60 kuanzia siku iliyotolewa hukumu, liliundwa na majaji sita.

Majaji hao ni Philomena Mbete Mwilu  ambaye ni Naibu Jaji Mkuu, ambaye amekuwa jaji kwa miaka 32, Jaji Mohamed Khadhar Ibrahim, aliyekuwa wakili na kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu Juni 16, mwaka jana na Profesa Jackton Boma Ojwang, jaji wa kwanza anayehudumu kuwa na hadhi ya uprofesa.

Alikuwapo pia Jaji Dk. Smokin Wanjala, ambaye amesomea sheria vyuo tofauti nchini Kenya na nje ya nchi na Njoki Susanna Ndung’u, jaji wa pili mwanamke katika Mahakama ya Juu na mtetezi wa haki za kina mama na kijamii.

Wengine ni Jaji Isaac Lenaola, ambaye alijiunga na Mahakama ya Juu mwaka jana kuchukua nafasi ya Jaji mstaafu Philip Tunoi na Jaji mstaafu Kalpana Rawal.

Aidha, Jaji Lenaola alikuwa jaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Katiba na Haki za Binadamu kabla ya kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles