NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
SERIKALI imesema wanafunzi ambao wazazi wao ni viongozi wanaotajwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, hawana sifa ya kuomba mkopo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru jana pia ilizitaja sifa 10 za msingi kwa muombaji wa mkopo huo.
“Waombaji ambao wazazi wao ni wakurugenzi au mameneja waandamizi katika kampuni binafsi zinazotambuliwa na mamlaka za mapato na usajili hawahitajiki kuomba.
“Watoto ambao wazazi wao ni viongozi wa umma au siasa wanatajwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma hawatarajiwi kuomba mikopo,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema mwombaji wa mkopo anatakiwa awe Mtanzania na awe ameomba kudahiliwa na chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na Serikali.
“Mwombaji asiwe mwanafunzi wa masomo ya jioni, asiwe na udhamini, ufadhili kutoka katika vyanzo vingine, awe ameomba mkopo kupitia mfumo wa mtandao.
“Pia anatakiwa awe amefaulu mitihani ya mwisho wa mwaka (wanaoendelea na masomo) na matokeo yake kuwasilishwa Bodi ya Mikopo na chuo chake.
“Awe amehitimu kidato cha sita au awe na sifa linganishi kama diploma ndani ya miaka mitatu 2015/16-2017/18, awe na umri usiozidi miaka 30 wakati wa kufanya maombi,”ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema mwisho wa kuomba mkopo ni Septemba 4, mwaka huu ikizingatiwa bodi ilianza kupokea maombi Agosti mwaka huu.
Mwaka jana bodi hiyo ilitangaza majina ya wadaiwa sugu ambao tangu wahitimu elimu ya juu hawajalipa madeni yao.
Baada ya kutangaza majina hayo kwenye vyombo vya habari, mwitikio wa ulipaji madeni ukaanza, ilisema taarifa hiyo.
Wadaiwa hao waliibuka ikiwa ni siku saba tu, tangu bodi hiyo itangaze kiama kwa wadaiwa wote sugu walionufaika na mikopo ya bodi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao kwenye vyombo vya habari na kuunda tume ya kuwasaka wadai hao.
Bodi pia ilianza kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao wa sheria kwa kuwatembelea kwenye ofisi zao kukagua na kuwahakiki kubaini kama wamewasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB.
Badru alisema mwitikio wa wanufaika umeendelea kuwa mkubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
“Mwitikio ni mkubwa, wengi wanajitokeza kulipa, wanufaika takriban 42,000 waliokuja kulipa hadi leo (jana) wameongezeka na kufikia 45,000,”alisema Badru.