30.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

MAWAZIRI WAMVURUGA JPM AWATUMIA SALAMU NZITO

ARODIA PETER NA AMINA OMARY – TANGA

RAIS Dk. John Magufuli ameonyesha hadharani kukerwa na utendaji kazi wa mawaziri wanne ambao wameshindwa kutekeleza vema majukumu yao  na maagizo anayowapatia.

Mawaziri hao ni wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, Waziri wa Maji na Umwagiliaji,   Gerson Lwenge, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango.

Rais Dk Magufuli alieleza wazi kukerwa na mawaziri hao kwa nyakati tofauti jana wakati akizindua viwanda mbalimbali jijini Tanga.

Akizungumza wakati wa  uzindua wa Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro kinachomilikiwa na wazawa, Rais Dk.Magufuli alisema anakerwa  na kigugumizi cha Waziri Mwijage kushindwa kuwanyang’anya wamiliki wa viwanda ambao wameshindwa kuviendeleza.

“Tanzania tuna viwanda 197 tulivyobinafsisha ambavyo vimelala, havifanyi kazi, hapa Tanga kulikuwa na viwanda 100, mmesema 12 vimesinzia kabisa, havifanyi kazi.

“Hivi Waziri Mwijage unapata kigugumizi gani, mpaka leo (jana), hujafuta kiwanda chochote licha ya kuwapo wawekezaji walionunua lakini hadi leo hawaviendelezi…nasema katika hili unanikwaza.

“Viwanda visivyofanya kazi vipo tu  kwa nini havifutwi? Waziri unamwogopa nani  wakati mimi ndiye niliyekuteua?

“Nikuombe waziri fumba macho usiangalie sura za marafiki   wenzako, viwanda vingi tuliwapa marafiki.

“Nimekueleza tukiwa ofisini kwenye cabinet (Baraza la Mwaziri), nilikuita wawili ofisini na hadharani kote hujanisikia, unataka nikueleze nikiwa kaburini?” alihoji Dk.Magufuli na kuongeza:.

“Waziri nakuagiza fungia viwanda vyote visivyoendekezwa, wengine ikibidi wakamatwe wapelekwe lokapu kidogo, wakitupeleka mahakamani tutajua namna ya kupambana nao.

“Sheria zipo tutawauliza wamechelewesha ajira ngapi za vijana wetu, kodi ngapi hatukuzipata, ikibidi tutawafungulia kesi ya uhujumu uchumi”.

Alisema wawekezaji wengine walionunua viwanda hivyo  walihamisha mitambo na kupeleka nchi jirani na kuacha magofu nchini.

 

MWIJAGE AJITETEA

Akitafuta njia ya kujinasua muda mfupi baadaye,  Waziri Mwijage alitumia nafasi ya uwekwaji wa jiwe la msingi katika upanuzi wa Kiwanda cha Maziwa cha Tanga Fresh uliofanywa na Rais Dk Magufuli.

Alipokaribishwa kuzungumza, alimwomba Rais asimkumbushe tena wajibu wake  kwa sababu  atamuumiza.

“Mheshimiwa Rais, naomba usinikumbushe tena wajibu wangu utaniumiza, nitayafanyia kazi maagizo yako mara moja.

“Nichukue nafasi hii kuwaagiza waliopewa viwanda vya dezo na kushindwa kuviendeleza waripoti wenyewe kwa wakuu wa mikoa wakieleza kwa nini wameshindwa kuviendeleza,” alisema.

Alisema kama wameshindwa kuviendeleza  waende kwake wakiwa na mwekezaji mpya  kwa sababu  Serikali haiwezi kuendesha viwanda bali sekta binafsi.

Kiwanda hicho cha maziwa kina uwezo wa kuzalishaji  maziwa   lita 50,000 kwa siku hadi 120,000  hatua ambayo inatarajiwa kuongeza idadi ya wafugaji kutoka 6,000 hadi 12,000.

 

WAZIRI WA MIFUGO

Wakati huohuo, Rais Dk. Magufuli  alimpa siku saba Waziri wa Kilimo na Mifugo, Charles Tzeba kwenda kiwanda cha Tanga Fresh kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kiwanda hicho.

Rais alitoa maagizo hayo baada ya kupokea taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi wa kiwanda hicho, Hamis Mzee ambaye alisema wamekwama kutoa maziwa  kwa wingi pamoja na kupanua kiwanda kutokana na kuwa na deni kubwa la kodi  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alisema licha ya kununua kiwanda hicho  mmiliki wa awali hakulipa kodi stahiki hivyo kusababisha wao kudaiwa kodi ambayo  haiwahusu.

“Mheshimiwa Rais, kiwanda hiki kinamilikiwa na wazawa asilimia 42 na nyingine mwekezaji kutoka Uholanzi. Tumeshindwa kukopesheka benki kwa sababu hatuna hati… mmiliki wa awali anadaiwa na TRA tumekwama tunaomba msaada wako,” alisema Mzee.

 

MAJIBU

Akijibu ombi hilo,   Rais Magufuli alianza kwa kuuliza kama waziri mwenye dhamana na mifugo amewahi kufika kwenye kiwanda hicho kujua changamoto kama hizo.

“Wakati mwingine huwa nakwamishwa na watendaji wangu serikalini, unawapa wizara kushughulikia matatizo yaliyopo, waziri anayehusika hatambui changamoto zilizopo.

“Sasa nampa siku saba Waziri wa Kilimo na Mifugo aje hapa atatue changamoto hizi. Kuhusu suala la hati nitawapatia mara moja,”alisema.

 

AKUMBUSHIA FLOW METER

Akiwa katika uzinduzi mwingine wa mradi wa matenki ya kuhifadhia mafuta uliofanywa na Kampuni ya GBP, Rais Dk.Magufuli alikumbushia kutokuwapo  mashine maalumu ya kupima wingi wa mafuta yanayoingia kutoka nje (Flow meter).

Alisema huenda kuna njama za rushwa kuhakikisha mashine hiyo haifungwi na kusababisha Serikali kukosa mapato yake.

“Ni mwaka sasa tangu Waziri Mkuu pale Dar es Salaam aagize watangaze tenda za flow meter na ifungwe pale bandarini, lakini cha ajabu hata kandarasi hajapatikana, anatafutwa kwa ujanja ujanja.

“Hata matatizo mengine yanashindwa kutatuliwa kutokana  na visheria vya ovyo na vya kijinga. Mawaziri mlioko hapa mpelekeeni salamu Waziri Mbarawa.

“Suala hili ukitaka kulitatua inabidi uhusishe Wizara ya Fedha na Mipango, Nishati na Madini, Maji, Viwanda na Biashara. Ni bahati mbaya  hawa watu mara nyingi hawawasiliani na kusababisha mambo mengi kukwama.

“Haingii akilini msimamizi wa Mamlaka ya Maji na Nishati (Ewura),hausiki na suala la umeme…kwa mfano, mafuta ya GBP kwenda mikoa jirani wanapanga bei kana kwamba mafuta hayo yametoka Dar es Salaam,” alisema.

Katika maagizo hayo, Rais alizitaka wizara zote zinazohusika kwa namna moja au nyingine na suala la mafuta, zikae pamoja kuhakikisha flow metre inapatiwa ufumbuzi wake.

“Hili ni la Profesa Mbarawa… hili mfikishieni ujumbe… kila kitu kinafanywa kwa ujanja ujanja, wale watakaokumbwa na huu mkumbo wakae wajiandae.

“Wawaziri wengine ni wapumbavu hawataki kufanyakazi maana hakuna njia nyingine za kupima mafuta zaidi ya flow meters.

Katika hatua nyingine, Rais aliiagiza Ewura kuangalia upya ukokotoaji wa gharama za mafuta yanayopitia Bandari ya Tanga ili yawe na bei tofauti na yanayopitia Dar es Salaam.

“Nikiangalia hapa sina hakika kama katibu mkuu wa maji yupo, mkurugenzi wa Ewura, siwezi kutoa instruction (maelekezo) juu ya suala hili.

“Walioko hapa watafikisha ujumbe wakitaka kuwasaidia kwamba  mafuta yote yanayotoka GBP hapa Tanga na kuuzwa katika mikoa jirani bei yake iwe  kwamba yanatoka Tanga.

“Nataka wafanyabiashara wengi waje hapa Tanga kuliko kwenda Dar es Salaam. Niombe Ewura walisimamie hili na kama kuna watu wa Ewura wanafanya mchezo katika suala la mafuta, wajiandae kwenda mahabusu,” alisema.

 

AISIFIA  GBP

Akizindua ujenzi wa matenki ya Kampuni ya Mafuta ya GBP, Rais Dk Magufuli alisifu uwekezaji na ulipaji wa kodi iliyolipwa.

GBP  imelipa kodi Sh bilioni 208 mwaka 2015/16 na Sh bilioni 293.2  mwaka 2016/17.

Alisema yeye ni rafiki wa wewekezaji wanaolipa kodi serikalini  kwa sababu  ndiyo inayoendesha nchi na muhimu kwa maendeleo.

Alisema  kuwapo bohari ya kuhifadhi kiwango kikubwa cha mafuta katika Jiji la Tanga kunasaidia kupunguza bei ya mafuta mkoani humo na akaiomba Ewura kukokotoa upya gharama za mafuta.

Bohari hiyo ya mafuta ina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 122.6 kwa wakati mmoja, huku matarajio yakiwa na kujenga matenki mengine yanayoweza kuhifadhi lita milioni 300.

Matenki ya GBP yanaelezwa kuwa ni hifadhi kubwa nchini ukiondoa yale ya Serikali ya TIPPER yaliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa GBP, Badar Sood alisema ujenzi wa matenki hayo umesaidia kupunguza foleni ya malori Dar es Salaam na uharibifu wa barabara.

Alisema malengo yake  ni kufanya uwekezaji mkubwa kwa kutumia meli kubwa   kupunguza gharama za usafirishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,212FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles