31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

BODI: WATOTO WA VIONGOZI HAWASTAHILI MIKOPO

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

SERIKALI  imesema wanafunzi  ambao wazazi wao ni viongozi  wanaotajwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma,   hawana sifa ya kuomba mkopo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru jana pia ilizitaja sifa 10 za msingi kwa muombaji wa mkopo huo.

“Waombaji ambao wazazi wao  ni wakurugenzi au mameneja waandamizi katika kampuni binafsi zinazotambuliwa na mamlaka za mapato na usajili hawahitajiki kuomba.

“Watoto ambao wazazi wao  ni viongozi wa umma au siasa wanatajwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma hawatarajiwi kuomba mikopo,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema mwombaji wa mkopo anatakiwa awe Mtanzania na awe ameomba kudahiliwa na chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na Serikali.

“Mwombaji asiwe mwanafunzi wa masomo ya jioni, asiwe na udhamini, ufadhili kutoka katika vyanzo vingine, awe ameomba mkopo kupitia mfumo wa mtandao.

“Pia anatakiwa awe amefaulu mitihani ya mwisho wa mwaka (wanaoendelea na masomo) na matokeo yake kuwasilishwa Bodi ya Mikopo na chuo chake.

“Awe amehitimu  kidato cha sita au awe na sifa linganishi kama diploma ndani ya miaka mitatu 2015/16-2017/18, awe na umri usiozidi miaka 30 wakati wa kufanya maombi,”ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo  ilisema mwisho wa kuomba mkopo ni Septemba 4, mwaka huu ikizingatiwa bodi  ilianza kupokea maombi Agosti mwaka huu.

Mwaka jana  bodi hiyo ilitangaza majina ya wadaiwa sugu ambao tangu wahitimu elimu ya juu  hawajalipa madeni yao.

Baada ya kutangaza majina hayo kwenye vyombo vya habari, mwitikio wa ulipaji madeni ukaanza, ilisema taarifa hiyo.

Wadaiwa hao  waliibuka ikiwa ni siku saba tu, tangu bodi hiyo itangaze kiama kwa wadaiwa wote sugu   walionufaika na mikopo ya bodi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao kwenye vyombo vya habari  na kuunda tume ya kuwasaka wadai hao.

Bodi pia  ilianza kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao wa sheria  kwa kuwatembelea kwenye ofisi zao   kukagua na kuwahakiki   kubaini kama wamewasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB.

Badru  alisema mwitikio wa wanufaika umeendelea kuwa   mkubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Mwitikio ni mkubwa, wengi wanajitokeza kulipa, wanufaika takriban 42,000 waliokuja kulipa hadi leo (jana) wameongezeka na kufikia 45,000,”alisema Badru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles