NA ASHA BANI
-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba amesema fukwe zote za Mkoa wa Dar es Salaam zitaimarishwa kuweza kuwa kivutio cha utalii na kuongeza pato la taifa.
Amewataka wanaojenga pembezoni mwa fukwe na vyanzo vya maji bila kufuata sheria ya mazingira kuondoka haraka iwezekanavyo kabla ya hatua hazijachukuliwa.
Makamba alitoa kauli hiyo Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa uzio pembezoni mwa mito na bahari.
Alisema ujenzi huo umefikia asilimia 75 na mkataba wake ni wa miezi saba.
“Hatua ya ujenzi huu ni uimarishaji wa fukwe katika jiji hili na utakamilika Novemba kuchochea vivutio vya utalii na kuongeza pato la taifa,”alisema.
Akiwa katika mfereji mkubwa unaonganisha eneo la Buguruni Malapa na Bungoni, alisisitiza mmiliki wa gereji kuondoka mara moja kutoa nafasi kwa ujenzi huo unaoendelea.
“Sitaki kujua nani anamiliki hiyo gereji hapo nataka kuiona haipo kwa maana hapa tunatekeleza Sera ya Mazingira katika ofisi ya Makamu Wa Rais,” aliongeza Makamba.
Makamba pia alikagua ujenzi wa uzio wa bahari ya Hindi ambao umeanzia ufukwe wa Coco Beach hadi pembezoni mwa Hospitali ya Ocean Road na kuelezea kuwa eneo hilo litakuwa la utalii zaidi.
Alisema eneo hilo litakuwa na kitega uchumi cha kutosha kwa kuwa litatumiwa kwa utalii na watu kupumzika.
Akiwa katika kingo zilizopo pembezoni mwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, alisema hata wanafunzi na wakazi wa hapo wataishi kwa amani kutokana na kingo za kuta kuacha kuliwa na maji.
Msimamizi wa mradi huo, Noela Shayo alisema ukuta wa Malapa utakua na uimara kwa miaka 50 huku ufukwe wa Bahari ya Hindi utadumu miaka 70.