NAIROBI, KENYA
MGOMBEA urais wa Nasa, Raila Odinga amesema atakubali kushindwa katika uchaguzi wa urais wa Agosti 8 iwapo tu utaendeshwa kwa uhuru, uwazi na haki.
Odinga alitoa sharti hilo, akisema ni muhimu kuhakikisha matokeo ya kura yanakubalika kwa washindani wote.
Alikumbushia pia kuhusu uwapo wa wapiga kura wafu pamoja na walioajiandikisha mara mbili.
“Sisi ni wanamichezo, ambao tunajua kwamba katika mechi yoyopte kuna kushindwa au kushinda.
“Iwapo tutashindwa uchaguzi kihalali, tutakubali,” alisema wakati wa mahojiano nyumbani kwake huko Karen, ambayo yalirushwa usiku wa alhamisi.
Lakini alisisitiza mwenye wajibu wa kuhakikisha chaguzi zinakuwa halali ni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.
Kauli hiyo ya Raila inakuja baada ya uongozi wa juu wa chama tawala cha Jubilee kumtaka atoe msimamo wake kuhusu suala hilo.