WASHINGTON, MAREKANI
WACHAMBUZI wa siasa mjini hapa juzi wameeleza wasiwasi wao kuhusiana na utayari wa utawala wa Rais Donald Trump kuitikia uwezekano wa machafuko wakati Kenya itakapoendesha uchaguzi mkuu mwezi ujao.
Balozi wa zamani wa Marekani nchini Kenya, Mark Bellamy aligusia kwamba Marekani na mataifa mengine wahisani wako njia panda kuhusu Kenya.
“Wanataka kusaidia kuzuia marudio ya machafuko ya uchaguzi wa 2007. Lakini haifahamiki iwapo ‘wana utashi wa kutosha kwa gharama ya kubariki kile kinachoweza kuwa uchaguzi uliojaa udanganyifu,” alisema Bellamy.
Wanasiasa wa Kenya wanatakiwa kuepuka kuchochea wafuasi wao kwa gharama yoyote, alisema Bellamy.
Mwingilio mzito wa kidiplomasia ulisaidia kusitisha umwagaji wa damu miaka 10 iliyopita na hivyo haupaswi kutokea kipindi hiki, alionya.
“Ni kwa vile hakuna uwezekano wa kutokea mwokozi kwa mazingira ya sasa— hakuna Kofi Annan,” Bellamy alisema akirejea upatanishi ulioongozwa na katibu huyo mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2008.
Iwapo machafuko yatatokea mwezi ujao, utawala wa Trump hauonekani kujiandaa kuitikia kwa namna, ambayo utawala wa Rais George Bush ulifanya mwongo uliopita.
Condoleezza Rice, waziri wa mambo ya nje kipindi hicho alipanda ndege kwenda Nairobi kuwahimiza viongozi wa Kenya kusitisha machafuko.
Aidha Jendayi Frazer, aliyekuwa msaidizi wa waziri huyo kwa upande wa Afrika alisafiri Kenya na kulaani mauaji yaliyohesabiwa ya utakasishaji kabila.”
Kwa kulinganisha, nyadhifa za juu kwa wawakilishi wa Afrika katika wizara hiyo na Ikulu zimebakia tupu tangu Trump aapishwe. Hakuna kiashirio kuonesha kuwa Trump mwenyewe anaipa uzito Kenya.