ATWOLI AISHAURI IEBC IFANYE KAZI NZURI AGOSTI 8

0
356

NAIROBI, KENYA


TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imehimizwa iwajibike ili kuendesha uchaguzi kwa njia huru na ya haki.

Ushauri huo ulitolewa jana na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli, ambapo aliitaka IEBC iwe makini inapotekeleza wajibu wake ili kufanyia Wakenya haki ifikapo Agosti 8, 2017.

Alisema wanastahili kutekeleza wajibu wao kwa uwazi na uwajibikaji kwa vile ulimwengu mzima unaitazama Kenya, na kwamba inategemewa  kwa masuala mengi.

“Iwapo tume hiyo itafuata sheria zote zilizowekwa kuhusu uchaguzi, bila shaka hakutakuwapo na udanganyifu wa aina yoyote,” alisema Atwoli.

Aidha, aliwashauri viongozi kuheshimu Mahakama kwa vile ni kitengo huru katika katiba na kwa hivyo inastahili kupewa nafasi kutekeleza wajibu wake bila  vitisho vyovyote.

“Ningetaka kuwajulisha viongozi waelewe mipaka ya   uongozi wao na iwapo watazingatia kuikosoa Mahakama bila sababu maalum, watakuwa wamevuka mipaka yao,” alisema Atwoli.

Kauli hiyo kuhusu mahakama inakuja ikiwa siku chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuikoromea kuwa inawasaidia wapinzani, kitu ambacho kimeshutumiwa na wengi.

Atwoli aliyasema hayo juzi jioni katika mahojiano ya mbashara katika kipindi cha Jeff Koinange Live kinachorushwa na Kituo cha Citizen.

Kuhusu uongozi wa Jiji la Nairobi, alisema eneo hilo linastahili kiongozi mwenye maono kwani ni sharti ‘mambo yabadilike kabisa’.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here