30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

HATIMAYE MDEE ARUDI URAIANI

PATRICIA KIMELEMETA Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imempandisha kizimbani Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na kumsomea shtaka moja la kutumia lugha ya matusi.

Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema (Bawacha), alifikishwa mahakamani saa 4:30 asubuhi na kusomewa shtaka hilo saa 8:12 mchana.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga na Inspekta Hamisi Saidi, alidai kuwa Julai 3, 2017 akiwa katika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam, Mdee alimtukana Rais Dk. John Magufuli kwa kusema kuwa ‘anaongea ovyo ovyo anatakiwa kufungwa ‘breki’.

Alidai kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria na kwamba kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Wakili Katuga alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba bado wanasubiri taarifa muhimu za kisayansi na picha za video na mashahidi muhimu watakaopatikana.

Aliiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa kutajwa kesi hiyo.
Hakimu Nongwa alimtaka mshtakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa ahadi ya bondi ya Sh milioni 10 na kuwa na wadhamini wawili wenye anuani ya kuaminika, ambao kila mmoja atasaini bondi ya kiasi hicho cha fedha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 7, 2017 itakapotajwa tena.

Akizungumza nje ya mahakama, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema Mdee amesomewa mashtaka hayo baada ya kuteswa mahabusu kwa zaidi ya siku sita.

Alisema utamaduni mpya unaojengwa na Serikali unaweza kujenga chuki ndani ya nchi.
“Tunaamini kila Mtanzania ana haki ya kueleza hisia zake akiwa ndani ya nchi, Halima ni mbunge na Mwenyekiti wa Bawacha, si tu kiongozi, bali pia ni mwananchi mwenye hisia, ambaye anaweza kuongea hisia zake,” alisema Mbowe.

Alisema Mdee alizungumzia suala la wanafunzi wanaopata mimba kurudi shule kulingana na hisia zake, ndiyo maana alikuwa anadai haki za watoto kama kiongozi.

Alisema rais amekuwa na maamuzi yanayokinzana na Katiba ya nchi na kwamba kutokana na hali hiyo, wataendelea kuzungumza bila ya kujali polisi, wakuu wa wilaya na mkoa wanatumikaje.

“Rais wetu amekuwa akifanya uamuzi unaokinzana na Katiba ya nchi, kama chama tutaendelea kuzungumza bila kujali polisi au mkuu wa wilaya anayetumika kwa ajili ya kuchukua sheria mkononi,” alisema.

Aidha Mbowe alisema hawatakaa kimya bali wataendelea kuzungumza kwa sababu sheria ni potofu na kwamba Serikali inapoteza muda na kuisumbua mahakama, lakini muda utasema.

Awali kabla ya kufikishwa mahakamani hapo, Mdee alikuwa akishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) ambako alihamishiwa Jumamosi iliyopita akitokea Kituo cha Polisi Oysterbay.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alisema kuwa walikuwa wakimshikilia mbunge huyo kutokana na kutoa maneno ya uchochezi na kumdhihaki Rais Magufuli.

Alisema walimkamata Mdee Julai 4, mwaka huu, saa 12:30 jioni katika maeneo ya Ubungo Kibangu.
“Tulimkamata Mdee baada ya kutoa maneno ya uchochezi na kumdhihaki Rais Magufuli kuwa ana maamuzi na kauli za ovyo na anatakiwa afungwe breki,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles