27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MKAPA ASIMULIA ALIVYOMUIBUA JPM

Na WAANDISHI WETU-DAR/GEITA


RAIS wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amesimulia jinsi alivyomwibua Rais Dk. John Magufuli hadi akamteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi katika uongozi wake.

Alitoa kauli hiyo jana wakati wa hafla ya makabidhiano ya hati za nyumba 50 zilizojengwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia (Global Fund) wilayani Chato, Mkoa wa Geita.

“Katika utawala wangu nilivutiwa na Magufuli kutokana na utayari wake, nguvu zake, ari yake, upendo wake na moyo wake wa kujitoa na kutumikia, ndiyo maana mwaka 1995 nikamteua kuwa Naibu Waziri na baadaye kuwa waziri kamili.

“Lakini vile vile ushirikiano wenu na upendo wenu wananchi wa Chato ndio uliomfanya Magufuli ang’ae mbele ya chama chake CCM na kuthaminiwa kubeba mzigo wa nchi hii.

“Kwa hiyo shukrani msinitupie mimi bali mshukuruni Magufuli, anafanya kazi vizuri na ataendelea kufanya kazi vizuri.

“Walionitangulia kuzungumza wamenishukuru mimi, lakini kwa kweli shukrani na sifa hizo zinatakiwa zielekezwe kwa Mwenyezi Mungu na Magufuli hadi mlipomchagua kuwa mbunge wenu.

“Mafanikio haya katika sekta moja tu ya afya ni matunda ya uongozi wake na chama chake,” alisema Mkapa.

Pamoja na mambo mengine, Mkapa aliwananga wapinzani ambao aliwaita wapumbavu.

Alisema kutokana na juhudi hizo katika sekta ya afya, sasa upumbavu wao utapungua.

“Binafsi nimefarijika na baadhi ya mafanikio ya sekta ya afya. Wale ambao Mwenyekiti Msukuma (Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Joseph Msukuma) ambaye ameniunga mkono kuwaita wapumbavu, natumaini kwamba kwa takwimu hizi zilizotolewa na Waziri wa Afya zitapunguza upumbavu wao,” alisema.

Alisema bado Tanzania ina uhaba wa wataalamu wa afya, hivyo akawataka wale wachache waliopewa dhamana hiyo kujituma na kufanya kazi kwa tija, kufuata taaluma zao na kuheshimu haki za binadamu.

“Hakuna budi kila mmoja wetu kujituma, kujikinga na maradhi mbalimbali. Natambua kwamba bado nchi yetu ina uhaba wa wataalamu wa afya, lakini wale wachache waliopewa dhamana hiyo, wajitume na kufanya kazi kwa tija na ufanisi kwa uchache wenu kufuata taaluma zenu na kuheshimu haki za binadamu.

“Imekuwapo mikataba baina ya nchi yetu kupitia Serikali yetu na asasi zisizo za Serikali, jumla ya dola za Marekani bilioni 1.9 (Sh trilioni 3.8) hadi kufikia Machi, mwaka huu.

“Mfuko wa Dunia umechangia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha huduma za Ukimwi, malaria, kifua kikuu… nasema asanteni sana Mfuko wa Dunia, nina imani mtaendelea kushirikiana na Serikali,” alisema Mkapa.

Naye Rais Magufuli alisema yeye ndiye anapaswa kumshukuru Mkapa kwa sababu kwa mara ya kwanza alimnadi na kuweza kuwa Mbunge wa Chato mwaka 1995.

“Nakumbuka mwaka 1995 katika uwanja huu huu mzee Mkapa ulinisimamisha pale.

“Nakumbuka wakati ukininadi ulikuwa umevaa viatu vyekundu, ukaniinua ukasema ‘mchagueni huyu mleteni huyu’.

“Wananchi wa Chato wakakusikiliza na wakakuamini na wakati huo mimi nikawa nashangaashangaa.

“Mungu akakusikia na wananchi wa Chato wakakusikia, wakanichagua kuwa mbunge na kwa mshangao mkubwa ukaniteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

“Kwa hiyo anayepaswa kushukuriwa ni wewe mzee wangu kwa sababu usingenichagua ningejishukuruje?

“Nakushukuru sana kwa sababu ni wewe ndiye ulitangaza, mimi sikustahili chochote. Mungu alikugusa nikachaguliwa na ukaniteua kuwa Naibu Waziri na baadaye waziri kamili.

“Najua mzee Mkapa wewe hupendi sifa, lakini kama utaikataa hii shukrani basi iende kwa Anna Mkapa, pengine ndiye aliyekushauri… mama Mkapa upokee shukrani hizi maana ulimshauri vizuri mzee.

“Lakini pia napenda kumshukuru sana mzee Jakaya Kikwete (Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne), ambaye katika kipindi chake alipokuja, kwanza wewe ukanipitisha kugombea ubunge kwa mara nyingine nikachaguliwa bila kupingwa.

“Lakini katika kipindi hicho mzee Kikwete aliniteua kuwa katika wizara mbalimbali nikiwa kama waziri.

“Pia nawashukuru sana viongozi wa awamu ya kwanza na ya pili ambao walitengeneza kuwa katika mazingira mazuri ya uongozi ndani ya CCM, Mkapa kwa kuwa uko hapa ninakushukuru sana,” alisema Rais Magufuli.

Alisema anamwomba Mwenyezi Mungu asimfanye kuwa na kiburi na kusahau alikotoka, bali awatumikie Watanzania.

“Ninamwomba Mwenyezi Mungu asinifanye nikawa na kiburi, pia asinifanye nikasahau nilikotoka.

“Mimi nimeuza maziwa na niliokuwa ninawauzia maziwa wengine bado wapo, nimeuza furu na nimechunga ng’ombe, kwa hiyo maisha ninayafahamu.

“Ndiyo maana ninapokuwa kwenye ‘level’ kubwa kama rais, sitaki kusahau nilikotoka na sitaki Watanzania wa maisha ya chini waonewe katika kipindi changu,” alisema.

Aliwataka watendaji wote katika sekta ya afya kuhakikisha wanatumia ipasavyo fedha zilizotolewa kwa huduma hiyo   na kuepuka ubadhirifu.

Alimpongeza Waziri wa Afya na Maendelelo ya Jamii, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa kutekeleza maelekezo yote aliyoagiza kuyafanyia kazi, ikiwamo kutonunua dawa kutoka kwa wafanyabiashara, badala yake zinunuliwe kutoka kwa watengenezaji wenyewe.

“Sitaki kusikia fedha za huduma muhimu kama za afya zinatumika vibaya kwa sababu kwa kufanya hivyo mtawaumiza wananchi ambao wengi ni masikini, jambo ambalo mimi sitaki tabia ya kuonea watu kwa kuwa nimetokea huko, ninajua shida wanazopata,” alisema.

Dk. Magufuli alionya dhidi ya ubadhirifu wa fedha za umma unaofanywa katika miradi na huduma mbalimbali zinazotolewa.

Alisema Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa pembejeo za ruzuku na hadi sasa katika mikoa 11 iliyowasilisha madai ya Sh bilioni 50, imebainika madai halali ni Sh bilioni nane.

Alisema umekuwapo utozaji ovyo kodi kwa wananchi, hasa wakulima kwenye pembejeo, jambo ambalo ni uonevu, hususan kwa wakulima wadogo.

Rais alisema uchunguzi dhidi ya wabadhirifu katika utoaji wa pembejeo kwa wakulima unaendelea.

“Sasa cha kushangaza eti hata mama yangu aliwekwa kwenye orodha ya waliojiandikisha kuchukua pembejeo. Nilipomuuliza akaniambia alifikiri alisainishwa vocha za simu,” alisema.

Taasisi hiyo ya Benjamin Mkapa pia imesaidia sekta ya afya katika kutoa mafunzo na ajira kwa watoa huduma wapatao 96 katika miaka 11 tangu ianzishwe.

Pia imekabidhi nyumba 50 kwa mikoa ya Geita (20), Simiyu (20) na Kagera (10).

 

HABARI HII IMEANDALIWA NA ELIZABETH HOMBO (DAR) Na HARRIETH MANDARI (GEITA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles