Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
MANISPAA ya Kigamboni imeanzisha utaratibu wa uchangiaji ada ya taka ambapo kila kaya itatakiwa kulipa Sh 3,000 kwa mwezi.
Awali wananchi walikuwa wakitozwa kati ya Sh 5,000 hadi Sh 40,000, wakati wenye hoteli walikuwa wakitozwa Sh 100,000 kwa mwezi.
Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha uchangiaji ada ya taka, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Stephen Katemba, alisema kulikuwa na vikundi visivyo rasmi vilivyokuwa vikitoza ada hizo na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Tumeandaa utaratibu utakaoleta unafuu katika uchangiaji taka, tunaamini Sh 3,000 kwa mwezi kila kaya inamudu, na kwa wafanyabiashara kama wenye hoteli watalipa Sh 60,000,” alisema Katemba.
Mkurugenzi huyo alisema kupitia mradi huo, vijana 134 kutoka katika mitaa husika watapata ajira za kukusanya ushuru na kuhamasisha uchangiaji ada ya taka.
Alisema pia ujenzi wa dampo jipya katika eneo la Lingato uko mbioni kuanza na kwamba wanatarajia hadi Septemba mwaka huu litakuwa tayari.
Awali Ofisa Mazingira wa Manispaa hiyo, Sixbert Kyaruzi, alisema taka zinazozalishwa kwa siku ni tani 210 na zinazozolewa ni tani 70.
Alisema awamu ya kwanza ya mradi huo utahusisha kata za Kigamboni, Mji Mwema, Tungi, Kibada na Vijibweni, ambapo magari manne yatatumika kuzoa taka katika kata hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, alisema mazingira mengi ya wilaya hiyo si salama na hata usafi hauridhishi.
“Utupaji taka katika fukwe bado ni changamoto, mateja wamekuwa wakipewa Sh 500 na kwenda kutupa taka ufukweni. Tutunze taka katika mazingira salama na kulipa ada kwa wakati ili manispaa ifanye kazi kwa ufanisi,” alisema Mgandilwa.