MWIGULU KUONGOZA DUA MAALUMU

0
544

NA CHRISTINA GAULUHANGA -DAR ES SALAAMWAZIRI wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuongoza viongozi wa Serikali, kidini na wananchi katika maombi maalumu ya kumwombea Rais Dk. John Magufuli, ili aweze kuendelea kufanya kazi zake kwa weledi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maombi hayo, Askofu Mkuu Dk. David Mwasota, amesema maombi hayo yatafanyika Julai 15, mwaka huu, katika Uwanja wa Uhuru.

Alisema katika maombi hayo, yaliyoandaliwa na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali, ‘I Go Africa For Jesus’ na wananchi, yatatoa fursa ya kuiombea amani nchi.

“Hadi sasa kuna wenzetu kutoka nje ya nchi, Marekani wameomba kushiriki nasi na tutakuwa pamoja nao, wametaka waje wengi, lakini imebidi tuweke ukomo,” alisema Mwasota.

Alisema lengo kuu la maombi hayo pia ni kumuunga mkono Rais Dk. Magufuli, ambaye amekuwa akiomba Watanzania wamwombee mara kwa mara.

Mwasota alisema kabla ya maombi hayo kutakuwa na semina kwa siku mbili ya viongozi hao kama maandalizi ya siku hiyo maalumu ya maombi.

Kwa upande wake, mjumbe wa kamati hiyo, Askofu Flaston Ndabila, alisema pia kila mkoa utawakilishwa na mjumbe mmoja katika maombi hayo.

Alisema baada ya maombi hayo, kila mkoa utaendelea na maombi yake kulingana na ratiba zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here