24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NGELEJA ATANGAZA KURUDISHA MIL 40 ZA ESCROW

Waziri wa zamani wa Nishati na Madini na Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja ametangaza kurejesha shilingi milioni 40.4, fedha za mgawo wa Escrow alizopokea kutoka kwa Mfanyabiashara James Rugemalira.

Mbunge Ngeleja ameitoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Habari Maelezo.

Pamoja na mambo mengine, Ngeleja anasema sababu zakurudisha fedha hizo ni kwa vile sasa imedhihirika kwamba aliyempa msaada huu anatuhumiwa kwenye kashfa ya akaunti ya Escrow, amepima na kutafakari, na hatimaye ameamua, kwa hiari yake mwenyewe, kurejesha serikalini (TRA) fedha zote alizopewa kama msaada (TZS milioni 40.4) bila kujali kwamba alishazilipia kodi ya mapato, na risiti ya  ushahidi wa kurejesha fedha hizi serikalini ipo.

“Nimeamua kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa tu, kwa vile hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya kashfa/tuhuma hizo,” amesisitiza Ngeleja

Kwa mujibu wa Ngeleja, tarehe 12/02/2014 alipokea fedha kiasi cha shilingi milioni 40.4 za kitanzania kutoka kwa Ndugu James Rugemalira, mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd. Fedha alizipokea kupitia akaunti yangu namba 00110102352601 ya Benki ya Mkombozi.

“Fedha hizo nilizipokea, kwa nia njema, kama msaada/mchango kutoka kwa ndugu Rugemalira ili zinisaidie katika kutimiza majukumu yangu ya kibunge, hususan,kusaidiana na wananchi wa jimbo langu la Sengerema na Taifa kwa ujumla, kutekeleza shughuli za kijamii (mfano ujenzi wa makanisa, misikiti, kusaidia kulipia karo za wanafunzi wasiojiweza, n.k) na shughuli za miradi ya maendeleo ambayo haipo kwenye bajeti ya serikali,” alisema Ngeleja

Aliongeza kuwa, “Nilipokea Fedha hizo kutoka kwa ndugu Rugemalira bila kujua kwamba fedha hizo zilikuwa zinahusishwa na kashfa ya akaunti ya fedha za Escrow kama ilivyo sasa,”.

Zaidi ya hilo, tarehe 15/01/2015 alilipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiasi cha Shilingi 13,138,125/= ikiwa ni sawa na asilimia 30 (30%) ya msaada huo aliopewa, kama ilivyoelekezwa na TRA.

Aliongeza kuwa, “Leo nina zaidi ya miaka 12 nikiwa kiongozi wa Umma, na pia niliwahi kuitumikia Wizara ya Nishati na Madini kwa takribani miaka mitano na nusu ( Naibu Waziri/Waziri), lakini sijawahi kukumbwa na kashfa ya rushwa au ufisadi. Kwa hiyo nimesononeka na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma,”.

Mbunge Ngeleja amesisitiza kuwa amerudisha fedha hizo ili kulinda heshima na maslahi mapana ya nchi yake, chama chake (CCM), Serikali yake, Jimbo lake la Sengerema, familia yake na heshima yake mwenyewe.

Hata hivyo amesema kuwa kupokea msaada ni jambo la kawaida, ila ikibainika kuwa msaada unaopewa una harufu ya uchafu hata kama haujathibitishwa na vyombo husika ni vyema kujiepusha nao.

“Ninampongeza, kwa dhati kabisa, Rais wetu mpendwa Dr John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwa maslahi ya Taifa letu. Nami naungana na watanzania wenzangu wazalendo kumuombea kwa Mungu na namhakikishia nitaendelea kumuunga mkono kwa kupigania maendeleo ya nchi yetu,” alisema Ngeleja

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles