Na JANETH MUSHI-ARUSHA
WAKILI wa Serikali, Sabina Silayo, amemkataa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda, kuendelea kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kwa madai kuwa ni rafiki wa karibu wa mke wa mshtakiwa, Neema Lema.
Lema anayekabiliwa na kesi mbili za uchochezi, jana alipangiwa kusomewa hoja za awali katika mahakama hiyo.
Hata hivyo, Lema alishindwa kufika mahakamani hapo baada ya wakili anayemtetea, kuieleza mahakama hiyo kuwa mteja wake anaumwa.
Katika maelezo yake jana, Wakili Sabina alidai mahakamani hapo kuwa, wasingekuwa tayari kumsomea hoja za awali mshitakiwa huyo kwa sababu hawana imani na Hakimu Patricia kuendelea kusikiliza shauri hilo.
Kutokana na hali hiyo, alimuomba hakimu huyo ajiondoe katika shauri hilo kwa kuwa akiendelea nalo, hataweza kutenda haki.
“Jamhuri tuna ombi moja, kwamba hatuna imani na wewe hakimu, tunaomba ujiondoe kwa vile mke wa mshtakiwa ni rafiki yako wa karibu sana na ushahidi huo tunao na hauna pingamizi.
“Tunaona hautatutendea haki, tunaona itakuwa busara kwako kujitoa kuendelea na shauri hili kutokana na urafiki wako na mke wa mshtakiwa,” alisema Wakili Sabina.
Kwa upande wake, Wakili Sheck Mfinanga, anayemtetea Lema, aliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali ombi hilo la wakili wa Serikali kwa kuwa hawaoni sababu ya msingi ya hakimu huyo kujitoa katika kesi hiyo.
“Kimsingi, sioni sababu ya msingi ya wewe kujitoa kwani Watanzania wote ni marafiki na ndugu pia. Sababu yako hiyo lazima ipimwe uzito na haina msingi wa kumkataa hakimu.
“Lakini pia, hao wanaolalamikia hili, hawajaleta huo ushahidi wanaosema wanao, tunaomba kupangiwa tarehe nyingine ya kumsomea mteja wangu maelezo ya awali,” alidai Wakili Mfinanga.
Awali Wakili Mfinanga aliiambia mahakama hiyo kwamba mteja wake anaumwa.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Patricia aliahirisha kesi hiyo saa 5:03 hadi saa 5:22 kutoa uamuzi mdogo.