Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZEE wa Mkoa wa Dodoma, wamempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa hatua anazochukua dhidi ya wabadhirifu wa rasilimali za nchi.
Pamoja na hayo, madhehebu mbalimbali mkoani hapa, yamepanga kuwa na ibada maalumu ya kumuombea Rais Dk. Magufuli.
Akizungumza juzi mjini hapa, Mwenyekiti wa Wazee wa Mkoa wa Dodoma, Balozi Job Lusinde, alisema Rais Dk. Magufuli amethubutu kikamilifu kuirejesha nchi katika heshima yake.
Balozi Lusinde alisema kwamba, kutokana na uwazi wa Rais Dk. Magufuli, ni wajibu wa kila Mtanzania kumuunga mkono kwa sababu analenga kuboresha maisha ya Watanzania.
[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=3aUsY3f2w7A[/embedyt]
“Hayati Baba wa Taifa alisema ni muhimu kupata kiongozi mwadilifu katika kuchagua viongozi, sasa tunaona maneno yake yanaanza kutuonyesha kuwa tumepata kiongozi mwsadilifu na mwenye uwezo wa kuthubutu.
“Hilo halina ubishi kwani Magufuli ameweka Watanzania mbele na nafsi yake nyuma katika uongozi wake ndiyo maana sisi kama wazee wa Mkoa wa Dodoma, tumefurahishwa na hatua aliyochukua na hata hii ya juzi ya kuzuia mchanga kutoka nje ya nchi na tupo pamoja naye,” alisema Balozi Lusinde.
Lusinde alimuomba Rais Dk. Magufuli kuendelea na kazi hiyo ya kufichua maovu huku akimweka mbele Mungu katika kila uamuzi anaoufanya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Mkoa wa Dodoma, Askofu Damas Mukassa, alisema umoja wake umejipanga kufanya ibada ya pamoja kumuombea Rais Dk. Magufuli kwa kazi nzuri anazofanya.
“Tumeibiwa vya kutosha ila tulikuwa hatujui na sasa Magufuli ametuonyesha wazi ni jinsi gani nchi hii ilikuwa inaibwa,” alisema Askofu Mukassa.