IBRAHIM AJIB AVUTA MIL 50 YANGA, ASAINI MIAKA MIWILI

0
1049
Ibrahim Ajib
Ibrahim Ajib

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

MATAJIRI wa klabu ya soka ya Yanga, wameanza kufanya kufuru ya usajili kwa kukibomoa kikosi cha mahasimu wao Simba, baada ya kukubali kumpa dau la Sh milioni 50 mshambuliaji wao, Ibrahim Ajib.

Licha ya kufanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo, Yanga ilikuwa ikiwania saini ya straika huyo kwa muda mrefu ili aweze kuichezea msimu ujao pamoja na michuano ya kimataifa.

Tangu hekaheka za usajili zimeanza baada ya Ligi Kuu kumalizika, Yanga ilikuwa kimya kutokana na kukosa jeuri ya kuwanasa wachezaji waliotakiwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia George Lwandamina.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka chanzo chetu ndani ya Yanga, zinadai kuwa jana Ajib alikutana na matajiri hao na kufanya mazungumzo ambayo yalifikia hatua nzuri na kukubali kusaini miaka miwili kucheza mitaa ya Jangwani.

Inadaiwa kuwa licha ya vigogo hao kukataa kujihusisha na masuala ya soka kwa sasa, wameamua kurudi kundini kuisaidia klabu hiyo baada ya kukwama katika mchakato wa usajili ili kukiimarisha kikosi hicho.

“Ajib amefikia hatua nzuri ya kujiunga na Yanga baada ya mazungumzo yao ya jana kwenda vizuri, hivyo tutegemee mambo mazuri,” kilieleza chanzo hicho.

Wakati Yanga ikifikia hatua nzuri na nyota huyo wa Simba, chanzo chetu kimedai kuwa kiungo mahiri wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima, anatarajia kutua nchini leo kwa ajili ya kusaini mkataba mpya wa kuichezea timu hiyo.

Niyonzima ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Yanga kutokana na uwezo aliouonyesha kwa kipindi alichoichezea timu hiyo, pia anawindwa vikali na Simba ambao wanadaiwa kufanya naye mazungumzo kwa nyakati tofauti.

Kama kiungo huyo atasaini Yanga, ni wazi kwamba watani wao wa jadi Simba watakuwa wamekwamishwa katika juhudi zao za kutaka kumnasa.

Wakati huo huo, Yanga imefanikiwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili beki wa timu ya Jang’ombe Boys, Abdallah Haji Shaibu ‘Ninja’.

Yanga imemnasa mlinzi huyo anayeimudu vyema kucheza kama beki wa kushoto ili asaidiane na Mwinyi Haji, kwani mkongwe Oscar Joshua yupo mbioni kutemwa.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here