Na MWANDISHI WETU
-SIMANJIRO
WACHIMBAJI Wadogo wa madini wa Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara wamewalalamikia Jeshi la Polisi kutokana na kitendo cha kuwafyatulia mabomu ya machozi waliokuwa chini ya mgodi ‘ardhini’ katika machimbo ya Mirerani jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.
Wachimbaji hao saba wakiwa umbali wa takribani mita 240, katika mgodi namba P.M.L 0000049 kitalu D unaomilikiwa na Theresia Wapalila, walikumbwa na dhahama hiyo baada ya kuingia eneo la Delta Kitalu C linachomilikiwa na Kampuni ya Tanzanite One.
Walieleza kuwa kitendo kilichofanywa na Polisi cha kupigwa mabomu mawili ya machozi wakiwa chini ya ardhi, kuharibu mundombinu ya umeme, kunyang’anywa vifaa vya kazi vimewaathiri zaidi kisaikolojia pamoja na afya zao.
Wachimbaji waliokamatwa na Polisi kisha kufikishwa kituo cha polisi ili kupewa fomu ya matibabu ni Boxer Dennis, Phillipo Paul, Ramadhani Hamza, Hamis Hassan, Edmund Mosha, Benjamin Shakoti na Emmanuel Afred.
Kwa niaba yao Meneja wa Mgodi huo, Frank Mushi alisema vitendo hivyo vya kupiga mabomu na kutembea na silaha za moto chini ya migodi vimekuwa vikifanywa na askari polisi wanaotumiwa na mwekezaji wa Tanzanite One.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe aliliambia gazeti hili kuwa alipata taarifa na malalamiko hayo na kuwaambia askari wasiendelee kupiga mabomu chini ya ardhi kwani ina athari kwa walioko chini na linapotokea jambo hilo itumike njia nyingine ya kulitatua.
Alisema ili kumaliza mvutano wa wachimbaji wadogo na mchimbaji mkubwa ambaye ni Tanzanite One, kuna mazungumzo yatakayofanyika wiki ijayo yatakayohusisha pia Kamishna wa Madini wa Kanda hiyo ili kuona namna gani watamaliza tatizo hilo.
Naye Mkurugenzi mwenza wa Tanzanite One inayochimba kwa ubia na Serikali kupitia Shirika la STAMICO, Faisal Juma alisema, changamoto kubwa inayojitokeza ni kwa wachimbaji wadogo kushindwa kutambua mipaka na kuheshimu sheria.
“Mgodi ule si wa kwetu pekee pale tunachimba kwa ubia na Serikali kupitia STAMICO. Hivyo ni lazima vyombo vya Dola viwepo ili kusimamia maslahi ya umma na kuona yakilindwa.
“Sasa kwa eneo la Delta ambalo hawa wanalalamika kuwa lilikuwa halichimbwi hiyo si sababu sasa hivi limeanza uzalishaji na linamilikiwa kisheria na Tanzanite One. Ni kweli wachimbaji wadogo katika harakati zao za kuchimba wanapitiliza na kuingia eneo hili,” alisema
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma alisema licha ya sheria ya madini kutozungumizia suala la mabomu chini ya ardhi bado wao kama wizira hawaruhusu kufanyika kwa vitendo hivyo.
“Hatuhitaji kutumia nguvu kubwa ya kuwapiga Watanzania mabomu ya machozi chini ya ardhi kwa sababu tu ya mtobozano wa uchimbaji suala hili linahitaji mazungumzo zaidi
“Hata hao Tanzanite One tulishawapa maagizo ya maandishi kwamba hairhusiwi kutumia risasi za moto chini wala mabomu.Sisi tuna ofisi pale Mirerani wanatakiwa kwenda kutoa taarifa muda wowote na tumekuwa tukiwashauri kufanya mazungumzo badala ya kutumia nguvu,” alisema Juma