WARAKA WANGU KWA MPENZI BIA

0
710

WASOMAJI wapenzi pasi na shaka mmeisikia Bajeti hivi punde, kila mmoja bado anasema lake, wapo wanaoipigia mayowe ya kuipongeza na wapo wanaoizomea.

Hiyo ndiyo dunia, Waswahili wanasema aliyekuzomea jana kesho atakushangilia, unaweza kubadili ukaanza na vyovyote upendavyo.

Kwangu Abiria wa Mwendo kasi, Bejeti hii imenilazimisha nitulize akili na pengine nithubutu kufanya maamuzi magumu.

Nayaita maamuzi magumu maana yanaweza kuniweka mbali na mpenzi wangu niliyekuwa karibu naye kwa miaka mingi.

Niliyempa nafasi kubwa ya maamuzi katika maisha yangu, nikawa sioni wala sisikii juu yake.

Nikampa nafasi ya kunipeleka puta kwa hiyari yangu, iwe asubuhi, usiku jioni au magharibi mimi niko naye.

Licha ya kunipa masharti kama nikikosa pesa nisimguse, lakini wapi umuhimu wake ulinifanya hata nikope ili niwe naye sambamba.

Huyu ni mpenzi Bia aliyenilaghai kwa kubadilisha majina pia kujibadili leo awe wa moto kesho wa baridi na huu ndiyo waraka wake:-

Hallo Mpenzi Bia

Mpenzi umenifanya nikumbuke jinsi nilivyofahamiana na wewe miaka mingi iliyopita, mwanzo sikukupenda nilikuchukia kabisa hata mdomoni mwangu hukuninogea hata kidogo.

Nililiona penzi lako ni chungu, linalobadilisha akili yangu kutoka utimamu hadi kuwa majununi.

Lakini hukuacha kurudiarudia vishawishi vyako, ulinidanganya nianze na moja, kisha mbili baadaye nikakuhitaji bila kuwa na idadi.

Ulivyoona nimekuzoea ukaanza kuniyumbisha, kunidhalilisha na kunifanya niwe mtumwa kwako, hivi leo nitakuachaje?

Sikuthubutu kulala bila wewe, sikujali kutembea usiku bila hofu ninapotoka kukutana na wewe, nilishindwa hata kuita mama pale penzi lako lilipozidi kichwani mwangu.

Mpenzi Bia hakuna jambo gumu kwa mtu mwenye akili timamu kama kulala kwenye matope, lakini uliponivuruga akili nililala tena usingizi wenye ndoto nzuri.

Tukiwa pamoja mpenzi Bia wewe unakuwa na kuliko fedha, maana nilikupenda sana, hata siku nyingine uliponimalizia hata nauli ya daladala na kesho yake nikaenda kibaruani kwa miguu, sikukuchukia bali nilizidisha mapenzi kwako.

Bia mpenzi siku nyingine ulinigomea hata kwenda kazini, ulinidanganya saa sita ya mchana nikaiona saa kumi alfajiri hivyo nikajua muda bado, lakini sikukuacha.

Wakati mwingine ulinidanganya kuwa mimi nina nguvu za kuweza kumpiga hata Tyson kumbe wapi, niliponyanyua mguu kumpiga mtu teke nilianguka mwenyewe!

Katika ugomvi unaoongoza kibaruani kwangu, wewe unahusika kwa asilimia 80, lakini hata siku moja sijakutupa.

Kwako mpenzi Bia ulinipa ujasiri usiokuwa na usalama kwangu, kwani unishauri nimtukane mtu yeyote hata polisi, lakini inapotokea mimi kupigwa virungu wewe mwenzangu unakaa pembeni, ngeu napata mie.

Ni mapenzi ya hali ya juu niliyokupa mpenzi Bia kama vile kupanga matumizi ya mshahara wangu, huku wewe ukizidi kuliko eneo jingine lakini yote haya nimeyavumilia.

Ubaya zaidi umekuwa mwenye wivu kwani kila ninapotaka kutoa pesa ili ninunue chakula nile uligoma, ulitaka niendelee kukutumikia wewe tu bila kujali kesho nitaamkaje?

Najua yapo mengi sana siwezi kuyamaliza lakini kubwa ni hili la kubadilika thamani kila mwaka, huku ukijua kipato changu kipo palepale.

Mpenzi Bia huna huruma na mimi sijasikia hata siku moja ukinishauri nikuache hasa kutokana na umri ili nijijenge maisha ya baadaye.

Pamoja na kuwa mimi ndiyo mtafutaji pekee na wewe mtumiaji lakini ulipenda niendelee kukutumikia mpaka uzeeni.

Baada ya kutafakari zaidi nimeamua kuandika waraka huu ili uniruhusu nikae pembeni ili niwatafute marafiki wasiokuwa na gharama kubwa kama maji au soda…Nasubiri majibu yako.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here