25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAFUNZO YA UALIMU YAIMARISHE UWEZO WA WALIMU

Na Christian Bwaya


KATIKA makala ya wiki iliyopita, nilijaribu kuonesha changamoto ya maandalizi ya walimu waliobobea katika kuibua udadisi kwa wanafunzi.  Ugumu wa kutafsiri mtalaa unaanzia kwenye mafunzo ya ualimu yasiyomfanya mwalimu kuwa mbunifu, mahiri mwenye uwezo wa kuibua udadisi kwa wanafunzi wake.

 

Wakufunzi na wahadhiri hutumia mbinu za kimazoea kuwaandaa walimu wanaotarajiwa kutumia mbinu shirikishi. Hatuwezi kumkaririsha mwalimu tarajali chuoni tukategemea atafanya kinyume chake akienda shuleni. Tunahitaji kuwasaidia walimu tarajali kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujifunzaji.

 

Mafunzo yawe ya vitendo

Suluhisho la pili ni kuyafanya mafunzo ya ualimu yawe ya vitendo zaidi ya nadharia za darasani. Hapa tuna maana ya kumwezesha mwanafunzi kuelewa na kutumia dhana za kitaaluma na kipedagogia kwa vitendo.

Hivi sasa mafunzo ya ualimu yametawaliwa na nadharia. Wakufunzi wanafundisha kwa namna ambayo mwanafunzi anayeandaliwa kuwa mwalimu hawezi kubobea. Kwa mfano, tunavyo vyuo vingi vya ualimu ambavyo havina maabara wala vifaa vya maabara.  Mwanafunzi wa sayansi, anayeandaliwa kuwa mwalimu, anamaliza mafunzo ya ualimu bila kukanyaga maabara.

Mwalimu huyu anapoondoka chuoni baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu, anakuwa hana uhakika wa maarifa aliyojifunza. Wakufunzi walitumia muda mwingi kumbushia maarifa ya kidato cha tano na sita, wakagusia masuala ya pedagogia ambazo wao wenyewe hawazitumii, mwalimu akahitimu.

Mhitimu huyu wa ualimu anabaki katika giza linapokuja suala la kuwawezesha wanafunzi wake kujifunza kwa vitendo. Kama ni mwalimu wa Kemia, hajui afanyeje kuandaa vifaa na kemikali zinazohitajika katika masomo ya vitendo. Hatuwezi kuendelea na mtindo huu tukategemea matokeo tofauti.

Tunahitaji vyuo vya ualimu viweke msisitizo mkubwa katika mafunzo kwa vitendo. Vyuo viwe na maabara na vifaa vya kutosha kwa ajili ya kufanya majaribio. Sambamba na kuwa na wakufunzi waliofuzu, wanahitajika watalaamu wa maabara watakaosaidia kuwezesha ujifunzaji huu kwa vitendo. Hakuna sababu inayoweza kuhalalisha mafunzo ya ualimu kuwa katika namna ilivyo hivi sasa.

 

Kuimarisha mazoezi ya ufundishaji

Kama sehemu ya mafunzo ya ualimu, mazoezi ya kufundisha ni sharti la kufuzu kwa mwanafunzi wa ualimu. Katika mafunzo ya miaka miwili kwa ngazi ya Stashahada, mwanafunzi anahitaji kutumia majuma yasiyopungua 10 akifundisha katika mazingira halisi ya shule.

Utaratibu wa sasa wa mazoezi ya kufundisha unakabiliwa na hitilafu kadhaa. Iliyo kubwa, kwa maoni yangu, ni kutumia muda wa mafunzo hayo kwa vitendo kama mtihani wa kutoa alama kwa mwanafunzi badala ya zoezi la kumwezesha mwanafunzi kuboresha uwezo wake wa kufundisha. Mkufunzi au mhadhiri anayekwenda kumtathmini mwanafunzi kwa mtazamo wa ‘kihakimu’, hawezi kuwa na muda wa kutoa mrejesho utakaotumika kumjenga mwanafunzi kuimarisha uwezo wake wa kazi.

Kadhalika, ni kawaida kwa zoezi hili la kuwatahini wanafunzi kufanywa na mkufunzi au mhadhiri mmoja ambaye wakati mwingine, kwa sababu zake, anaweza kutaka kutahini wanafunzi 15 kwa siku moja. Katika mazingira ambayo mhadhiri au mkufunzi hana muda wa kutosha kufanya kazi hiyo nyeti, inawezekana ndani ya muda wa dakika zisizozidi 20 akafanya tathmini iliyopaswa kufanyika katika kipindi cha dakika 80. Matokeo yake ni kwamba taarifa anayoandaa kutathmini uwezo wa mwanafunzi wake inaweza isiakisi uwezo halisi uliooneshwa na mwanafunzi.

Tunapendekeza kuboresha mrejesho wa tathmini anayofanyiwa mwanafunzi. Mwanafunzi anayekwenda kwenye mazoezi ya vitendo afanyiwe tathmini za mara kwa mara zinazomwezesha kujipima na kujirekebisha mpaka atakapofikia kiwango kinachohitajika. Kwa kufanya hivi kipindi cha mazoezi ya kufundisha kitakuwa sehemu ya kujifunza kweli kweli badala ya kuwa wakati wa kupima uwezo pekee na kutoa alama.

Katika kukabiliana na changamoto ya idadi ya wakufunzi na wahadhiri, tunaweza kutumia mfano wa utaratibu unaotumiwa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Walimu wa shule za sekondari hupatiwa mafunzo maalum ya mbinu shirikishi za ufundishaji. Baada ya mafunzo hayo ya muda mfupi, walimu hawa wanaofanya kazi katika shule zinazotumiwa kwa mazoezi ya ufundishaji, hufanya kazi kama ‘waangalizi’ wa zoezi hili muhimu kabla wahadhiri hawajafika kufanya kazi yake.

Utaratibu huu una faida mbili. Kwanza, mwanafunzi anaangaliwa kwa karibu na mtu aliye kwenye mazingira yake na hivyo tathimini anayofanyiwa inakuwa na uhalisia zaidi. Pili, mwanafunzi anakuwa na fursa ya kutumia maoni ya ‘mwangalizi’ kurekebisha makosa yake kabla hawajafanyiwa tathmini ya ufundishaji na wahadhiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles