Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
BENKI ya Kimataifa ya Biashara (ICB), imetangaza kuuza biashara zake hapa nchini.
ICB iliyoanzishwa mwaka 1997 inapanga kuuza asilimia 100 ya biashara zake.
Benki hiyo ina matawi matano katika Jiji la Dar es Salaam ambayo ni Jamhuri, Ubungo, Vijana, Lumumba na Mikocheni ambako imekuwa ikihudumia wajasiriamali wadogo, wa kati na wafanyabiashara wakubwa.
Tangu juzi kumekuwa na matangazo ya kuuzwa kwa benki hiyo kwenye vyombo vya habari, huku sababu za uamuzi huo zikiwa bado hazijulikani.
Moja ya tangazo lililochapishwa jana kwenye gazeti moja la kila siku (si Mtanzania), linaonyesha kuwa benki hiyo inapanga kuuza biashara zake kwa asilimia 100.
“Wawekezaji wanakaribishwa kujipatia umiliki wa asilimia 100 wa benki yenye kibali kamilifu na iliyojiimarisha kibiashara.
“Benki imejikita katika kuhudumia wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs). Benki ina sifa nzuri na iliyosambaa sokoni ikiwa na wafanyakazi wenye ujuzi na utaalamu pamoja na huduma kwa njia ya kielektroniki,” ilisema sehemu ya tangazo hilo.
MALAWI, MSUMBIJI, ZAMBIA
Julai 2013, ICB pia iliuza biashara zake katika nchi za Malawi, Msumbiji na Zambia.
First Merchant Bank (FMB), ilinunua hisa zote za ICB Malawi, asilimia 70 ya hisa za ICB Msumbiji na asilimia 62 ya hisa za ICB Zambia.
Mkurugenzi Mtendaji wa FMB, Dheeraj Dikshit, alikaririwa na vyombo vya habari wakati huo akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kupandisha hadhi ya benki hiyo katika nchi hizo.
BOT
MTANZANIA lilimtafuta Mkurugenzi Usimamizi wa Benki kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kenedy Nyoni, ambaye alisema kuwa anafuatilia suala hilo.
“Sheria inazungumza kuhusu mabadiliko ya wamiliki wa benki ambayo yanapaswa yapate baraka za BoT. Nitafuatilia kujua zaidi kwa sababu jambo linalokwenda kwa umma lazima liwe na taarifa za uhakika,” alisema Nyoni.