27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAMIA WAMUAGA GWIJI WA HABARI 

Na ASHA BANI – DAR ES SALAAM


MAMIA ya waombolezaji wamejitokeza kwa wingi jana kuaga mwili wa aliyekuwa gwiji wa habari, marehemu Chrysostom Rweyemamu maarufu Mwalimu (64) nyumbani kwake Mbweni kwa Masanja, Dar es Salaam.


Mwili wa Rweyemamu, ulifanyiwa ibada katika Kanisa la Mtakatifu Raphael Malaika Mkuu na kusafirishwa kwenda kijijini kwao Iyunga, Wilaya Muleba mkoani Kagera kwa mazishi ambayo yanatarajia kufanyika kesho.


Ibada hiyo, iliongozwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Rafael Malaika Mkuu, Father Dino.
Ibada ya kuaga mwili wa marehemu ilianza saa 12:50 mchana na kufuatia salamu mbalimbali za rambirambi kutoka kwa taasisi, vikundi na wafanyakazi wenzake.

 

SALAMU
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga kwa niaba ya familia, alisema marehemu ameacha watoto watatu, mjane na wajukuu wawili.


Alisema Rweyemamu alifanya kazi katika taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Elimu na Utamaduni, Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ) na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd tangu ilipokuwa ikijulikana kama Habari Cooperation.
Mukajanga alisema kuwa baadae Rweyemamu aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Maarifa Media Trust (MAMET) ndani ya Habari Cooperation.


Alikuwa kiongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), msuluhishi wa kesi katika Baraza la Habari (MCT) na Mwenyekiti wa Majaji wa Tuzo za Uandishi Bora na Umahiri (EJAT).

 

SALAMU MBALIMBALI
Katibu wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Henry Muhanika, akimwakilisha Mwenyekiti wake, Regnald Mengi, alisema tasnia ya habari imepoteza mwandishi maarufu na muhimu kutokana na kufanya uchambuzi wa kuelimisha jamii mara kwa mara.


“Marehemu amefanya kazi nzuri, kuna watu lazima wajivunie kwa kuwa ameacha urithi mkubwa kwetu,” alisema Muhanika.

MCT
Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la Habari, Jaji Thomas Mihayo, Mukajanga alisema wamepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa mshauri na pia msuluhishi na kwamba mara ya mwisho alikuwa Mwenyekiti wa Majaji wa Tuzo za Uandishi Bora na Umahiri (EJAT).

 

KIBANDA
Naye Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, alisema Rweyemamu ameacha pengo ambalo linakosekana neno sahihi la kusema.


Alisema kuwa alikuwa kazini kwa takribani miaka 18, akiwa mmoja wa viongozi alioshirikiana na waandishi wa habari nguli kama Dk. Gideon Shoo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu wakati wa Serikali ya awamu ya nne, Salva Rweyemamu na Jenerali Ulimwengu.


“Pamoja na hao, ndio wametufanya sisi kutembea kifua mbele leo hii… wapo magwiji wengine waliotangulia mbele za haki, kama si hawa tasnia ya habari isingefika hapa tulipo sasa,” alisema Kibanda.
Aliahidi kuendelea kufanya kazi pale alipoishia Rweyemamu, licha ya ukweli  kwamba anajua nafasi yake aliyoiacha itapwaya.
“Tunaendelea kufanya kazi alipoishia, tunajua patapwaya, tutaendelea kusifu mengi na si moja kwa kazi yake na urithi mzuri aliotuachia,” alisema Kibanda.

 

WADAU WA TASNIA
Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Masawe, alisema anamfahamu vizuri marehemu kwa muda mrefu katika tasnia ya habari.


Alisema ni mtu ambaye alikuwa anafanya kazi zake kwa uweledi, ndiyo maana watu wengi wamejitokeza kumuaga.
“Nilishirikiana naye vyema, ni mtu mzuri tuliyeshirikiana naye vizuri hapa mtaani, alikuwa anapenda ibada bila kukosa, tumepoteza jirani mwema kabisa,” alisema Kanali Masawe.

 

EDDA SANGA
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Edda Sanga, alisema anamfahamu marehemu kutokana na kushirikiana naye mambo mbalimbali ya kikazi.


Alisema aliwahi kufanya naye kazi akiwa mwalimu wa TSJ kwenye mtandao wa EJAT, akiwa mwenyekiti.
“Nilikuwa naye katika kundi la majaji akiwa mwenyekiti, pia ni mtu aliyependa kazi yake kama mboni ya jicho lake, ameondoka, tuliobaki tunatakiwa kumuenzi,” alisema Edda.

 

ULIMWENGU
Mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kijamii, siasa na elimu, Jenerali Ulimwengu, alisema marehemu alikuwa mtu muhimu na mwenye mchango mkubwa katika kufundisha na kulea vijana katika tasnia ya habari.
Alisema alikuwa hasiti kuona mwandishi anakosea na kumrekebisha, hivyo si rahisi kupata mtu wa kuziba pengo lake.

SALVA
Naye Salva Rweyemamu alisema tasnia imepoteza mtu muhimu na maarufu, aliyekuwa na uwezo wa kipekee.

MUSHI
Mwandishi mkongwe, Deo Mushi, alisema marehemu alikuwa mtu wa hekima, aliyemfundisha mambo mengi alipokuwa akifanya naye kazi miaka 10 iliyopita.


 “Marehemu aliwahi kunirudishia makala yangu ambayo niliandika ya siasa, akaniambia hii makala ipo ovyo ovyo, haina mbele wala nyuma, akanirekebisha vizuri na ikapata tuzo, nakumbuka ilikuwa na kichwa cha habari ‘kwa nini Mwai Kibaki awe rais 2002’,” alisema Mushi. 


Rweyemamu alifariki dunia Jumamosi saa 2:30 usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Awali mtoto wa marehemu, George Chrysostom alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na uvimbe tumboni na alifanyiwa upasuaji vizuri, lakini hali ilibadilika ghafla na kupoteza uhai.


Alisema daktari aliyekuwa akimtibu kabla ya kufikwa na mauti, aliwaeleza kuwa baba yao alianza kupata shida ya kupumua ghafla hatua iliyosababisha kupoteza uhai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles