Na FERDNANDA MBAMILA–DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, imekuwa ikipiga vita suala la uvuvi haramu.
Wavuvi hufanya shughuli hizo kwa kutumia tindikali na baruti kuvulia samaki kutokana na hali ngumu ya maisha kuwakumba na inawawia vigumu sana kupata vifaa vya kisasa.
Hatimaye wavuvi hao kutumia zana haribifu za kuvulia na kusababisha uharibifu wa samaki na mazingira kwa ujumla.
Pia nyenzo na vitendea kazi vya kuvulia samaki vinavyotumika hadi leo ni vya teknolojia ya muda mrefu ambavyo havina ubora na uwezo wa kuvuna samaki wengi. Hali hiyo huchochea kukosa ajira kwa vijana na hivyo kukosekana kwa bidhaa ya samaki katika nchi mbalimbali wakati rasilimali zipo nchini. Kwa upande mwingine, Serikali wangezingatia upatikanaji kwanza wa vifaa vya kisasa vya kuvulia samaki kwa wavuvi.
Vilevile Wizara ina wajibu wa kujua matatizo na maendeleo ya wavuvi kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kuwatembelea na kujua hali yao popote pale ili kuwaweka katika mazingira bora na yakiteknolojia ya utumiaji wa vifaa vya kuvulia vya kisasa kulingana na masoko ya kimataifa katika uuzwaji wa samaki.
Ingawa kwa asilimia chache sana samaki huuzwa nje ya nchi na ipo nyuma katika uzalishaji wa bidhaa ya samaki kwa wingi.
Hivyo, taifa kushindwa kufikia malengo stahiki ya mpango mkakati wa maendeleo ya nchi ya viwanda.
Hali hiyo vilevile inawakumba wavuvi wa Soko la Kimataifa la Feri kutokuwa na vifaa vya kisasa kwa ajili uvuvi wa samaki na hivyo kusababisha kutumia mbinu mbadala na haribifu ambayo inawawezesha kupata samaki kwa urahisi zaidi.
Inasikitisha kuona kuwa kwa asilimia kubwa sana ya wavuvi hapa nchini hutumia baruti kuvulia samaki.
Wavuvi hao wa Soko Kuu la Kimataifa la Feri wameiomba Serikali kuwapatia mikopo ya fedha ili waweze kununua vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuvulia samaki, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kuendesha shughuli zao kwa urahisi na salama zaidi.
Naye Naibu katibu wa Soko hilo, Abeid Bura, anasema kuwa endapo Serikali watalitilia mkazo suala hili linaweza kuwasaidia baadhi yao kuondokana na uvuvi haramu na kuingia kwenye uvuvi wa kisasa ambao utawasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya samaki na kukuza kipato.
“Changamoto kubwa tuliyonayo ni pamoja na ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya kuendesha shughuli zetu, jambo ambalo limesababisha baadhi yetu kutumia uvuvi haramu kwa ajili ya kupata samaki,” anasema Bura.
Anasema vyombo vinavyotumika sasa hivi kuvulia samaki ni vile vya kizamani ambavyo vinasababisha wavuvi kutumia njia rahisi ikiwamo ya uvuvi haramu ili kukidhi mahitaji yao.
Anasema kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali kuwapatia mikopo ambayo itawasaidia kununua vifaa vya kisasa kama vile nyavu na boti za kisasa za kuvulia samaki.
Anasema kutokana na hali hiyo, mikopo hiyo itawasaidia kupata vifaa bora ambavyo vitaweza kuongeza uzalishaji wa samaki na kuisadia Serikali kupata mapato.
Pia itaisaidia Serikali kujulikana katika soko la kimataifa kutokana na uboreshwaji wa mazingira mazuri kwa wavuvi na vifaa vya kisasa.
Hii itakuwa chachu kwa wateja wa mataifa mbalimbali kutokana na kuuziwa bidhaa bora na salama kutoka Tanzania isiyovuliwa kwa kemikali na madawa mbalimbali.