27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

AIRTEL MBIONI KUINGIA DSE

Shermarx Ngahemera


MSEMO kuwa kutangulia si kufika na mwendapole hajikwai unajidhihirisha kwenye suala la kuingia soko la hisa kati ya Kampuni za Airtel na Tigo ambao wanatakiwa kisheria kujiunga kwa shuruti ikiwa itifaki na masharti yakizingatiwa.

Sheria inataka kampuni za simu kujiorodhesha na DSE ili hisa zake kwa asilimia 25 ziuzwe kwenye soko hilo ili wananchi waweze kununua na kumiliki sehemu ya biashara hizo na kufaidi matunda ya uwekezaji kwenye biashara ambayo inaonekana kutengeneza faida kubwa kwa wenye mali.

Kipenga kilipopigwa kujiorodhesha ilianza kampuni kubwa kuliko zote za simu nchini ya Vodacom Tanzania kwa kuachia asilimia 25 ya hisa kwa kudai apate Sh billioni 476 katika toleo la awali (IPO) ambapo hisa moja iliuzwa kwa Sh 850.

Kampuni ya TIGO ambayo ina kesi mahakamani katika masuala yake ya umiliki, ilifuatia kwa kuweka nia na sasa ni Airtel ambayo inaonekana kuwa karibu kupita baada ya kuruka vihunzi vya awali vya wenye mali kupitisha azimio la kukubali kuuza hisa na kujiunga na DSE. Ni habari njema kwa kila Mtanzania kwani inatoa nafasi kubwa ya kushirikishwa kwenye uchumi wa nchi.

Airtel au kwa jina lake la Bharti Airtel inamilikiwa na mfanyabiashara wa India, Mittal Ambani na Serikali ya Tanzania ikiwa na hisa 40 wakati Ambani ana hisa 60. Taarifa za kuaminika zinasema wamekubaliana kuwa kila mmoja wao aachie asilimia 12.5 kuuzwa kwenye soko kadiri ya Sheria ya EPOCA inavyotaka.

Wanahisa walikutana Ikulu na kuamua kuachia asilimia 12.5 kila mmoja wao na jina litakuwa Airtel Company Plc na limeshasajiliwa na Brela na hivyo kukidhi haja ya ushiriki na kinachosubiriwa ni uchapishaji wa Matarajio ya Toleo (IPO Prospectus) yanayotayarishwa na uongozi wa Airtel yatapitishwa kwanza na DSE, halafu Mamlaka ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ambayo ndio itakayotoa kibali cha uuzaji na ununuzi wa hisa hizo sokoni. Ni utaratibu mrefu lakini ni salama kwa wale ambao wanaowekeza mitaji yao kwani lazima ihakikishwe kuwa ni salama na hakuna longo longo.

Kampuni zinatakiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha faida husika ili wanahisa wapate gawio. “Yote haya ni kumlinda mteja anayenunua hisa hizo kuwa kuna uhakika mkubwa wa kupata faida ingawa biashara ina hatari nyingi vilevile ambapo nia nzuri inaweza kwenda kombo kutokana na mwenendo wa soko husika,” kinasema chanzo chetu cha habari kutoka DSE.

Hali hiyo imetokea kwenye mauzo ya Hisa za Vodacom ambayo pamoja na kusubiriwa kwa hamu kubwa na wawekezaji, matarajio ya Kampuni hiyo hayakwenda vizuri hadi muda wa ziada ulipoongezwa. Vodacom Tanzania matarajio yake hayakufikiwa kirahisi kuuza hisa zake za toleo la awali (IPO) Sh bilioni 476 sawa na Dola za Marekani milioni 213.

Kilichotokea hisa lulu za Vodacom Ingawa ilikuwa bado kupata hesabu kamili juu ya hatima ya mauzo hayo, kulijaa matumaini kuwa vikwazo vya awali vilitolewa na wengi kupata uwezo wa kununua hisa hizo za kihistoria katika soko kwa ukubwa wa toleo la mauzo, kiwango na kiasi kilichosajiliwa kama bei ya awali ya hisa.

Si kawaida kwa hisa za awali DSE kuongezewa muda wa mauzo yake rasmi ya ufungaji kabla ya kuorodheshwa, tayari ishara zilionesha kwamba mambo si bambam. Mauzo ya hisa milioni 560 za Vodacom yalianza Machi 9, mwaka huu na yalitarajiwa kufungwa Aprili 19, huku bei ya kila hisa ikiwa ni Sh 850.

Kwa mujibu wa waraka wa matarajio, Vodacom Tanzania Plc ina thamani ya Sh trilioni 1.9. Mkurugenzi Mtendaji wa Orbit Securities ambao ni washauri wa uwekezaji na wasimamizi wakuu wa mauzo ya hisa za Vodacom, Laurean Malauri, alionyesha imani yake ya kufanikisha uuzaji huo kwa mafanikio yatakuwepo baada ya muda wa nyongeza.

Japokuwa hakutaja kiwango kilichopatikana wakati huo, Malauri amekubali kwamba ukubwa wa thamani ya hisa hizo pamoja na kukosekana kwa ukwasi miongoni mwa Watanzania waliolengwa kwenye mauzo hayo ni changamoto za msingi.

“Serikali ilitoa upendeleo pekee kwa Watanzania tu kunufaika na hisa za kampuni za simu katika matoleo ya msingi (primary market) na kuzuia wawekezaji kutoka nje ya nchi ambao wanachangia kiwango kikubwa kwenye biashara ya hisa DSE ikiwamo wale kutoka EAC na SADC,” alibainisha Malauri.

Hali hiyo inatoa ishara kwa Serikali na wadau wote kuhakikisha kwamba kunakuwepo na mtazamo mwingine kisera ili kuzuia mkwamo kwani bado kuna zaidi ya kampuni nyingine 8 za simu na mawasiliano pamoja na migodi mingi zinatakiwa kuuza hisa zake kama alivyofanya Vodacom fedha zitatoka wapi? Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles