25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, January 29, 2022

ELIMU YAHITAJIKA MAFANIKIO KILIMO CHA KOROSHO

NA CHRISTINA GAULUHANGA–DAR ES SALAAM


SERIKALI imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha wakulima nchini wananufaika na mazao yao kwa kuwapatia mbegu bora na zana za kilimo za kisasa.

Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ni moja ya wilaya zilizopo nchini ambazo uchumi wake unategemea zao la korosho.

Pia wilaya hiyo ina fursa kubwa ya uwekezaji ambapo wawekezaji wamekuwa wakivutiwa na ardhi yake na kuamua kuwekeza kwa kuanzisha viwanda mbalimbali ambavyo kwa namna moja ama nyingine vimesaidia kuwainua kiuchumi wananchi wa huko.

Hapa nchini mikoa 11 na halmashauri 50 zinalima zao la korosho ambapo mikoa mitano inalima korosho za asili ambayo ni Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga.

Pia kuna mikoa mipya sita katika uzalishaji wa korosho ambayo ni Morogoro, Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya na Singida.

Mikoa hii mipya imeamua kulima korosho baada ya kuona manufaa yake kutoka katika mikoa ya asili na kuzuiwa kulima pamba kwa visingizio visivyo na msingi. Pamba ilikuwa inastawi sana katika mikoa hiyo na ilikuwa ni zao muhimu kiuchumi kwao.

Kadiri siku zinavyokwenda korosho inazidi kupanda kibiashara kwa sababu ya umuhimu na uhitaji wake katika soko la dunia na hivyo imesababisha Bodi ya Korosho Tanzania kujitahidi kutoa elimu kwa wakulima wa zao hilo. Wilaya ya Mkuranga ni mojawapo ya wilaya zilizopata fursa ya kukusanya wakulima na wadau wa zao hilo kwa ajili ya kupatiwa elimu.

Bodi ya Korosho Tanzania imefanya juhudi ya kutoa elimu kwa wadau wa zao hilo kwa kushirikiana na wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele pamoja na Taasisi ya Utafiti ya Viutilifu vya Kitropiki ya Arusha (IPRI).

Meneja wa Tawi la Dar es Salaam kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, Mangile Maregesi, anasema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa na bodi kwa wakulima wa zao hili.

Anasema wakulima wamefundishwa mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na aina ya udongo na njia ya upandaji wa mikorosho, kanuni bora za utunzaji wa shamba, utambuzi wa magonjwa na wadudu wanaoshambulia mikorosho sambamba na matumizi sahihi ya mabomba ya kupulizia dawa, viuatilifu katika zao na huduma za ugani.

Anasema kama inavyofahamika kuwa Serikali imeagiza kila kijiji kupanda miche bora 5,000 na kila kaya kupanda miche bora 30.

Anaongeza kuwa ili kufanikisha suala hilo, Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya zinazolima korosho, wameingia mikataba na wazalishaji wa miche bora ili kuweza kupata miche ya kugawa bure.

Maregesi anasema wakulima watakaonufaika na miche hiyo wakiitunza vizuri itaongeza uzalishaji wa korosho kutoka tani 265,000 zilizozalishwa msimu wa mwaka 2016/17 hadi kufikia tani 500,000 kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Sambamba na taratibu za kuhudumia zao hilo, pia wakulima walifundishwa kuzifahamu mbinu mpya za kilimo ili kuboresha zao hilo, mbinu ambazo zimepatikana kupitia utafiti uliofanywa na wataalamu ambao ni watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele kwa kushirikiana na IPRI.

Wakulima hao pia walifundishwa namna ya kutunza korosho baada ya kuvuna ili kuziwezesha kubaki na ubora kabla ya kuuzwa au kuwasilishwa kwa chama cha msingi na kuwezesha kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo.

Anasema kupitia mafunzo haya, washiriki wanatakiwa kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ili kuliwezesha zao hilo kuongeza uzalishaji na ubora sambamba na kuinua hali za wakulima kwa kuwaondoa katika umasikini.

Anasema katika mafunzo hayo, mada mbalimbali zitatolewa ambapo pia wakulima watafundishwa kilimo hicho kwa nadharia na vitendo ili waweze kuelewa vizuri kwa kuwapeleka katika moja ya shamba lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 2000 lililopo Kitongoji cha Magawa wilayani hapo, shamba ambalo kwa muda mrefu liliharibika.

Maregesi anaongeza kuwa, kufuatia hatua hiyo Serikali kupitia Bodi ya KoroshoTanzania imejipanga kuhakikisha pembejeo za korosho kwa msimu ujao wa mwaka 2017/18 kwa wakulima zinawafikia kwa wakati kwani mpaka  sasa tani 2,890 za Salfa ya unga
na lita 30,000 za viatilifu vya maji zimeshawasili katika Bandari ya Dar es Slalaam na mbegu zinatarajiwa kuanza kutolewa mwezi ujao.

Aidha, anasema awamu nyingine ya mbegu inatarajiwa kuwasili mapema iwezekanavyo ili kuwawezesha
wakulima kupata mbegu kwa wakati.

“Katika msimu uliopita wa mwaka 2016/17, upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za ruzuku za zao la korosho ulikuwa wa kuridhisha kutokana na kupatikana kwa fedha za ushuru wa mauzo nje ya nchi kwa wakati kulikowezesha uagizaji wa pembejeo nao pia ufanyike kwa wakati,” anasema Maregesi.

Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Filbeto Sanga, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa wazalendo na mabalozi wazuri kwa wengine.

Sanga anasema mafunzo yanalenga kuinua ubora wa zao hilo.

“Kupatikana kwa fedha za ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi kwa wakati kuliwezesha uagizaji wa pembejeo ufanyike kwa wakati mwafaka na hivyo kumfikia mkulima kabla ya muda wa kupuliza dawa kwenye mikorosho haujafika,” anasema Sanga.

Anasema kiasi cha pembejeo kilichoagizwa kilikuwa cha kuridhisha mpaka sasa, bado vipo viuatilifu vilivyobaki katika maghala ya Mwendapole Kibaha, Naliendele Mtwara na Mtwara Mjini.

Anasema katika msimu wa mwaka 2017/18, Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa pembejeo za korosho zinawafikia wakulima kwa wakati kwani mpaka sasa tani 2,890 za salfa yaunga na lita 30,000 za viuatilifu vya maji zimeishawasili katika
Bandari ya Dar es Salaam.

Mtafiti wa masuala ya kilimo ambaye ndiye aliyekuwa mkufunzi wa wakulima katika mafunzo hayo, Dk. Shamte Shomari, anawataka wakulima kuzingatia kanuni na taratibu za kilimo wanazopatiwa ili kupata mazao yenye ubora na kuepuka kulima kiholela.

Anasema ulimaji holela unaweza kusababisha mkulima kushindwa kupata mazao ya kutosha kulingana na ukubwa wa shamba alilolima.

Anasema elimu aliyowapatia wakulima kuhusu ulimaji bora wa zao la korosho ikizingatiwa, itawaondoa katika umasikini na kuwawezesha kujiendeleza zaidi kwa kuongeza kipato.

Mohamed Athuman ambaye ni mmoja wa wakulima, ameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wakulima mara kwa mara.

Anasema utoaji wa elimu kwa wakulima utaliwezesha Taifa kukua kiuchumi na wakulima kuondokana na umasikini.

Anasema kuchanganyikana wakulima katika mafunzo hayo kumewapa uwezo wa kubadilishana mawazo na mbinu za ulimaji bora wa zao hilo katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Anasema elimu ya stakabadhi ghalani imesaidia wakulima wengi kuongeza kipato na ili kuwezesha wakulima wengi, ipo haja kwa Serikali kutilia mkazo elimu hiyo.

Athuman anasema kupitia utaratibu wa stakabadhi ghalani, wakulima wengi wameweza kunufaika kwa kujipatia fedha za kutosha kupitia mazao yao pamoja na kwamba wapo baadhi yao ambao hawakuwa na elimu hiyo. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
177,227FollowersFollow
532,000SubscribersSubscribe

Latest Articles